Sh580 bilioni za EU kuboresha upatikanaji maji jijini Mwanza

Mkuu wa Mashirikiano Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Marc Stalmans akizungumza baada ya kutembelea mradi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji cha Butimba jijini Mwanza kilichojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na jumuiya hiyo kwa zaidi ya Sh70 bilioni. Picha na Damian Masyenene
Muktasari:
- Zitaongeza upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa jiji hilo ambalo mahitaji yake kwa siku ni lita milioni 172 wakati uzalishaji wake ni lita milioni 138 kwa siku.
Mwanza. Umoja wa Ulaya (EU) unatarajia kutoa zaidi ya Sh580 bilioni kufadhili awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba cha maji Butimba, jijini Mwanza.
Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa jiji hilo na maeneo ya jirani.
Ahadi hiyo imetolewa leo Alhamisi, Aprili 10, 2025 na Mkuu wa Ushirikiano wa EU nchini Tanzania, Marc Stalmans wakati wa ziara ya wataalamu kutoka nchi wanachama wa EU, waliokuja kutathmini utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo, ambayo iligharimu zaidi ya Sh70 bilioni.
Awamu ya kwanza ya mradi huo iliyokamilika Desemba 2024, ilihusisha ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba ambacho kinazalisha lita milioni 48 kwa siku.

Kituo hicho kimeongeza uwezo wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) kuzalisha maji kutoka lita milioni 90 hadi zaidi ya lita milioni 138 kwa siku.
Kabla ya mradi huo, Mwauwasa ilitegemea chanzo cha Kapri Point pekee, ambacho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 kwa siku, huku mahitaji halisi yakiwa ni lita milioni 172 kwa siku.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua mradi huo, Stalmans amesema EU kupitia mpango wa Green and Smart Cities SASA, imefikia hatua ya kutoa fedha za kufanikisha awamu ya pili kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza.
"EU imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu unaosimamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), chini ya mpango wa LVWATSAN, unaolenga kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika Ziwa Victoria. Kuna kila dalili ya kuendelea kufadhili awamu inayofuata," amesema Stalmans.
Ameongeza kuwa, "Mradi huu unaonyesha mafanikio makubwa. Ingawa bado mahitaji hayajafikiwa kikamilifu, kazi iliyofanyika ni ya kupongezwa. Wiki iliyopita, EU ilifikia hatua nzuri ya kutoa EURO 200milioni, sawa na zaidi ya shilingi 580bilioni kwa ajili ya awamu ya pili."
Mbali na kuboresha maisha ya wakazi kwa kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama, Stalmans amesema mradi huo utasaidia pia kupunguza uchafuzi wa maji katika Ziwa Victoria.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Nelly Msuya ameishukuru EU kwa msaada wa awamu ya kwanza ulioongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 90 hadi milioni 138 kwa siku.
"Kwa sasa, tunakabiliwa na upungufu wa lita milioni 34 tu, ukilinganisha na upungufu wa awali wa lita milioni 82 kwa siku," amesema Msuya.
Amesema Mwauwasa kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji safi na salama.
"Nia yetu ni kuona ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo kama EU unaendelea kuleta matokeo chanya katika huduma ya maji," ameongeza.
Mkazi wa Buhongwa, Joyce Sule ametoa wito kwa Mwauwasa kuhakikisha miundombinu ya usambazaji wa maji inaboreshwa ili kupunguza upotevu wa maji, hasa kutokana na uchakavu na ongezeko la watu.

Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza anayeshughulikia Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Patrick Karangwa amesema utekelezaji wa programu ya Green and Smart Cities SASA utachangia kukuza uchumi na kuboresha maisha kupitia miundombinu bora ya huduma mbalimbali ikiwemo masoko, machinjio na mialo ya Ziwa Victoria.
"Serikali, kwa kushirikiana na vyuo kama VETA na FETA, itaendesha mafunzo ya kiufundi kwa vijana, ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kuunda ajira zaidi kwa jamii," amesema Karangwa.