Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh1.3 trillioni kukwamua kaya maskini Tasaf awamu ya tatu

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wanahabari baada ya kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili namna mpango wa tatu wa kunusuru kaya maskini utakavyotekelezwa

Muktasari:

  • Kaya mpya 900,000 zinatarajiwa kuingizwa katika mpango wa tatu wa kunusuru kaya maskini (PSSN III) unaotarajia kuanza mwakani, ikiwa ni baada ya mpango wa pili kukamilika Septemba 2025.

Dar es Salaam. Wakati Sh1.3 trilioni zikitarajiwa kutumika katika mpango wa tatu wa kunusuru kaya maskini (PSSN III) chini ya Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wadau wameshauri mpango huo sasa kufungamanishwa na mifumo ya kidigitali ili kuweka urahisi katika ufuatiliaji.

Matumizi hayo ya kidigitali yatasaidia kuepusha wanufaika kupewa fedha taslimu na kuhakikisha fedha inafika kwa mlengwa kama ilivyokusudiwa.

Kati ya fedha ambazo zinatarajiwa kutumika, zaidi ya Sh786.28 bilioni zinatarajiwa kutolewa na Benki ya Dunia (WB) na kiasi kinachobakia zaidi ya Sh524.19 bilioni zikitarajiwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha wadau wa maendeleo, wawakilishi wa balozi mbalimbali, mawaziri, Mwakilishi wa Benki ya dunia kujadili namna mpango wa tatu utakavyotekelezwa. Mkutano huo uliratibiwa na Wizara ya Fedha.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Tasaf, Shedrack Mziray amesema mpango wa pili wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa sasa unatarajia kufikia ukomo Septemba 2025 hivyo tayari Serikali iliandaa andiko la mpango wa tatu.

“Baada ya kuandaa andiko tuliona ni muhimu kukaa na wadau wa maendeleo kuangalia namna mpago huu utaendelezwa pamoja na sera nzima ya hifadhi ya jamii,” amesema Mziray.

Amesema mpango wa tatu unatarajia kuongeza kaya mpya 900,000 zitakazo hudumiwa kwa miaka mitano.

“Lakini tunafikiria, kumekuwa na changamoto tunapoibua hizi kaya zinakaa muda mrefu kwenye huu mpango, nia ni kuwaondoa kwenye umaskini, hatuwezi kuingiza kaya tunaipa huduma halafu inakaa milele hii imekuwa ni moja ya changamoto.

Sasa tumekubaliana tukiingiza kaya inakaa miaka mitatu ili waanze kujipanga,” amesema Mziray.

Mpango huu unakuja wakati ambao kaya milioni 1.3 nchi nzima zinanufaika na mpango wa pili ambao unaelekea ukomo na kupitia tathmini iliyofanywa miaka miwili iliyopita walibaini kaya 400,000 maisha yao yameboreka hivyo waliondolewa katika mpango.

“Sasa tunapokwenda mwaka mmoja wa kukamilisha tutakuwa na kaya takribani 950,000 tutakazokwenda nazo na tutakapoanza mpango mpya kaya ambazo haziwezi kufanya kazi kama walemavu na wazee tutaendelea nao kutokana na hali zao,” amesema Mziray.

Wakati hili likisemwa, Waziri wa Fedha na Mipango upande wa Zanzibar, Dk Saada Mkuya ametaka mpango wa Tasaf ufungamanishwe kwenye mifumo ya kidigitali, ili kuweka urahisi wa kuona fedha imetoka wapi, imekwenda wapi na imetolewa lini.

“Tofauti na sasa inawapa fedha taslimu wanaweza kutumia wasijue, pia Tasaf inasaidia wazee sana ukimpa mkononi anaweza kunyanganywa, tufungamanishe mpango wa Tasaf na mifumo ya kidijitali ili kuweka urahisi kuona fedha imetoka wapi, imekwenda wapi, imetolewa lini ametoa nani,” amesema Dk Mkuya.

Amesema jambo hilo litawasaidia hata wanufaika kuwa na ari ya kuendelea kutumia mifumo mbalimbali ya kifedha ambayo pia wataitumia kuweka akiba.

“Na hii itafanya ujumuishaji wa huduma za kifedha kuongezeka na kama nchi itaweza kujua watu wangapi wanatumia mifumo ya kifedha,” amesema Dk Mkuya.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema mpango huu unakuja wakati ambao nchi ina matumaini ya kuona kiwango cha umasikini kimepungua kupitia utafiti utakaotolewa wa mwaka 2024.

“Utafiti wa awali unaonyesha kuwa umasikini umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2018 na sasa tunaendelea na utafiti wa mwaka 2024 ambayo itatupa namba mpya. Na hatua mbalimbali ambazo zimefanyika tunaamini tutapata takwimu mpya ambazo zitaonyesha umasikini umepungua,” amesema Dk Nchemba.

Akizungumzia mpango wa tatu unaoandaliwa, Dk Nchemba amesema kati ya mambo yatakayozingatiwa ni uwepo wa miradi ya maendeleo jumuishi ambao utawawezesha wananchi wa kipato cha chini kwenda sambamba na dira ya maendeleo ya Taifa 2050.

“Mpango wa tatu tunaoutaka ni ule utakaokuwa jumuishi kama na dira ya maendeleo ya Taifa 2050 inavyosema kuwa mtu yeyote asiachwe nyuma hivyo itahusisha shughuli za uzalishaji ambao hautabagua sehemu ya jamii kwa kuzingatia makundi maalumu,” amesema.

Mwakilishi mpya wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Natham Belete amesema alithibitisha kuwa walipokea ombi jipya kutoka Wizara ya Fedha la ufadhili kwa awamu inayofuata ya mpango wa Tasaf lenye thamani ya takriban dola milioni 300.

“Kwa sasa, tuko kwenye mazungumzo ya kina na mamlaka kuhusu awamu hii mpya ya msaada, na nina uhakika kuwa tutaweza kutoa ufadhili unaoendelea kwa programu hii muhimu kwani Benki ya Dunia inabaki na dhamira ya kusaidia Tanzania kupitia msaada wa kiufundi, kifedha, na suluhisho bunifu,” amesema Belete.