Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SGR yasafirisha abiria milioni 2.1 ndani ya miezi saba

Muktasari:

  • Watanzania milioni 2.1 wamesafiri kwa kutumia treni ya kisasa (SGR) huku Shirika la Reli Tanzania likitangaza matumaini zaidi ya kuwepo kwa mageuzi ya ufanisi pindi treni ya mizigo itakapoanza kazi

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema ndani ya miezi saba ya huduma ya reli ya kisasa ya umeme (SGR) wamesafirisha abiria milioni 2.1.

Kadogosa amesema wanajivunia kutoa huduma hiyo huku ujenzi wa reli hiyo ambayo kwa sasa inaishia Dodoma kutokea Dar es Salaam unaendelea kuelekea Mwanza.

“Ndani ya miezi saba ya utendaji wa SGR tunajivunia kutoa huduma kwa abiria milioni 2.1, tunapoelekea kuonyesha mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita tutaeleza mafanikio zaidi,”amesema Kadogosa

Kadogosa ameyasema hayo Machi 29, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni (iftar) iliyoandaliwa na TRC.

Akitoa salamu zake, Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga aliitaka TRC kuhakikisha maeneo ambayo mechi za fainali za mashindano ya kombe la Afrika (Afcon) yatafanyika kuwepo na usafiri wa uhakika na haraka.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, akizungumza katika hafla ya iftari 

“Tukifanikiwa hili tutaweka urahisi wa watu kusafiri kwenda kuangalia mechi sehemu moja na kurudi eneo lingine au katika makazi yao, usafiri wa haraka ni muhimu sana,” amesema Bananga.

Mashindano hayo yataandaliwa na nchi tatu—Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027.

TRC ilianza huduma ya SGR rasmi Julai 14, 2024 na hadi kufikia Novemba 2024 jumla ya abiria 1,000,000 walikuwa wamesafirishwa.

“Shirika limefanikiwa kusafirisha abiria zaidi ya 1,000,000 katika kipindi cha miezi minne tangu uzinduzi wa njia za treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma mnamo Juni 2024. Idadi hiyo ni mara mbili ya abiria waliosafirishwa na treni ya zamani (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja,” ilieleza taarifa hiyo ya Fredy Mwanjala ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC aliyoitoa Novemba 20, 2024.

Aidha, katika iftari hiyo mgeni rasmi alikuwa Mufti na Shekh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ally ambaye amewataka watanzania kuendelea kuyaishi yale yaliyofundishwa katika mwezi mtukufu ambayo ni kulinda amani na kulinda ndimi zao ili zisiwaumize wengine.