Serikali yataka waajiri kuzingatia sheria namba tisa

Muktasari:
- Sheria hiyo inaweka takwa la kisheria kwa waajili wenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha kuwa asilimia tatu ya wafanyakazi hao ni watu wenye ulemavu.
Njombe. Serikali imeahidi kuendelea kusimamia kikamilifu suala la upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu hapa nchini, huku ikitaka waajili kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi wao ni watu wenye ulemavu.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Novemba 23, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wakati akifunga maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe kitaifa ambayo yamefanyika hapa mkoani Njombe.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 hususani kifungu namba 31 ambacho kinamtaka kila mwajiri mwenye wafanyakazi wanaozidi 20 kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi hao ni watu wenye Ulemavu.
"Kwa hiyo hilo tutalisimamia kwa dhati sheria namba tisa ya mwaka 2010 kifungu namba 31 ya watu wenye ulemavu inataka mwajiri mwenye watu zaidi ya 20 asilimia 3 wawe watu wenye ulemavu," amesema Ndalichako.
Amesema Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora zimekuwa zikishirikiana katika ajira ambazo zinatolewa na wamekuwa wakizingatia asilimia tatu ya watu wenye ulemavu kupata ajira.
Amewataka watu wenye ulemavu hapa nchini kuchangamkia fursa za ajira ambazo zimekuwa zikitolewa kwani wengi wao wamekuwa hawajitokezi kuomba ajira hizo.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi, Cyprian Luhemeja amesema vyama vya ulemavu visiishie kuwa chama chenye ulemavu bali kiwe chama kinachochagiza maendeleo na uchumi.
"Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza utaratibu wa kuwa na kanzi data ya walemavu wote nchini na tumeshaanza mkoa wa Mara tunakuja muda si mrefu kuzindua lengo letu sasa kila mkoa na ofisi ya wenye ulemavu, aina ya ulemavu, vikundi mnavyojiunga navyo na kazi mnazozifanya" amesema Luhemeja.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kwenye kundi la watu wenye mahitaji maalum mkoa huo una zaidi ya watu 6400 lakini watu wasioona ni 1000 huku wakike ni 400 na wakiume ni 600.
"Mheshimiwa Waziri Nikuhakikishie kwamba pale ambapo serikali itatoa muongozo kuhusu zile hela za asilimia kumi inayowahusu watu wenye uhitaji maalum sisi wenye mamlaka za serikali za mtaa tutatekeleza na tutafanya miradi ambayo siku moja tutakualika kuja kuona" amesema Mtaka.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), Omary Mpondelwa amesema chama hicho kimeendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa miongozo ya chama hicho ya kuendelea kushawishi huduma bora kwa watu waioona ili kuweza kufikia malengo ya chama.
"Yale ya kuhakikisha kwamba wasioona wanapata mafunzo mbalimbali ikiwemo elimu, ushirikishwaji na kupashana habari" amesema Mpondelwa.