Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaingilia kati foleni Mbeya

Muonekano wa barabara ya mchepuko katika eneo la Shamwengo, Kata ya Inyala jijini Mbeya, iliyotajwa kuwa mwarobaini wa foleni kwenye barabara kuu ya TANZAM pamoja na kusaidia kupunguza ajali. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Yaanza ujenzi wa barabara ya mchepuko Shamwengo kupunguza ajali, mradi utakaogharimu Sh1.5 bilioni.

Mbeya. Hatua ya Serikali ya kuingilia kati changamoto ya msongamano wa magari na ajali katika eneo la Shamwengo imeanza kuzaa matunda baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya kuanza ujenzi wa barabara ya mchepuko inayolenga kupunguza foleni kubwa ya malori pamoja na ajali zilizokuwa zikigharimu maisha ya wananchi.

Mradi huo unaotekelezwa katika Kata ya Inyala, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, unahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa mita 800 kwa gharama ya zaidi ya Sh1.5 bilioni, zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya ujenzi na uchukuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mei 15, 2026, Mwakilishi wa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Justine Mrope, amesema ujenzi huo umetokana na maagizo ya Serikali kufuatia tathmini ya maeneo hatarishi yenye msongamano wa magari na ajali.

Amesema eneo la Shamwengo lilibainika kuwa miongoni mwa sehemu korofi zaidi kutokana na mteremko mkali unaochangia msongamano wa malori na ajali za mara kwa mara.

“Tulipokea maelekezo kutoka kwa waziri mwenye dhamana akituelekeza kufanya tathmini ya maeneo yote yenye changamoto ili kupata suluhisho la kudumu. Shamwengo imeonekana kuwa eneo hatarishi zaidi,” amesema Mrope.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo, barabara ya mchepuko itatumika kwa magari yanayoingia mjini Mbeya, huku njia ya sasa ikibaki kwa magari yanayotoka kuelekea Dar es Salaam na mikoa mingine, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Seleman Bishanga, amesema Serikali pia inaendelea na maandalizi ya mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi, yenye urefu wa kilometa 29.

Amesema tayari Serikali imemuagiza mkandarasi kurejea maeneo muhimu, ikiwemo madaraja mawili na eneo la Iwambi ambalo limekuwa likikumbwa na ajali mara kwa mara.

“Mheshimiwa Rais ameielekeza Serikali kuhakikisha tatizo la foleni ya malori linapungua. Ndiyo maana tumeanza kufungua barabara za pembezoni sambamba na maandalizi ya barabara ya njia nne,” amesema Bishanga.

Ameongeza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha usalama barabarani na kupunguza msongamano wakati mradi mkubwa wa njia nne ukisubiri utekelezaji.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Shamwengo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itakuwa suluhisho la muda mrefu la changamoto iliyodumu kwa miaka.

Mkazi wa eneo hilo, Hamis Namwinga, amesema kabla ya mradi huo barabara hiyo ilikuwa chanzo cha ajali na foleni kali zinazodumu kwa saa kadhaa, hasa nyakati za jioni.

“Magari yalikuwa yanakwama kwa muda mrefu hadi saa mbili au tatu, na wakati mwingine ajali zilikuwa za mara kwa mara. Hii imekuwa changamoto kubwa sana kwa miaka,” amesema Namwinga.

Ameongeza kuwa eneo hilo lilikuwa likishuhudia ajali takribani tatu hadi nne kwa wiki, baadhi zikiwa na madhara makubwa ya vifo na majeruhi, hivyo kuomba kasi ya ujenzi iongezwe ili kukamilisha mradi mapema.

Kwa miaka ya hivi karibuni, eneo la Shamwengo limekuwa likitajwa kama mojawapo ya maeneo hatarishi zaidi katika Mkoa wa Mbeya kutokana na msongamano wa malori na ajali, hali iliyosababisha Serikali kuchukua hatua za haraka za ujenzi wa miundombinu mbadala.