Serikali yaeleza mkakati kudhibiti vifo vya wajawazito

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenye mkutano wa tisa wa bunge jijini Dodoma, Novemba 1, 2022.
Muktasari:
- Serikali imetaja mikakati ya kumaliza vifo vya wanawake wanaokufa kwa njia ya upasuaji siku chache baada ya kujifungua kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya huduma za afya.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Christina Mnzava amehoji ni nini chanzo cha vifo kwa wanawake wanaokufa kwa njia ya upasuaji siku chache baada ya upasuaji.
Akijibu swali hilo la msingi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema wizara yake ilifanya ufuatiliaji wa vifo vitokanavyo na uzazi kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.
Amesema ufuatiliaji huo umeonesha kuwa vifo ambavyo vilisababishwa na matatizo ya dawa za ganzi/nusu kaputi na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ni 58 sawa na asilimia 3.3 mwaka 2018, vifo 80 (4.8) mwaka 2019, vifo 65 (4.0) mwaka 2020 na vifo 65 (4.1) mwaka 2021.
Amesema sababu kuu za vifo hivyo ni nne ambazo ni ajali ya dawa za ganzi/nusu kaputi, kupoteza damu wakati au baada ya upasuaji, tatizo la damu kuganda na maambukizi ya bakteria baada ya upasuaji.
Amesema wizara kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma inatekeleza mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya huduma za Afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa katika eneo la utoaji ganzi au nusu kaputi na upasuaji kwa usalama kwa kuzingatia miongozo.
Awali, Dk Mzava amesema ufuatiliaji umeonyesha mwaka jana ni asilimia 4.1 walifariki dunia baada ya kujifungua baada ya operesheni kuna utafiti gani umefanyika kufahamu ni kwanini wakinamama wanapoteza maisha muda mfupi baada ya kujifungua kwa upasuaji.
Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo kusomesha wataalam, kujenga zahanati 288, magari ya kubebea wagonjwa 663 ili kupunguza vifo vya wanawake na watoto