Serikali yaeleza kwa nini inatafiti ukosefu wa nguvu za kiume

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile
Muktasari:
Dk Ndugulile amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu na pia kujua ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kwa kiasi gani nchini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile ametaja sababu za Serikali kufanya utafiti wa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume kuwa linatokana na baadhi ya waathirika kutafuta suluhisho la tatizo hilo kinyemela na hivyo kukosekana taarifa sahihi.
Dk Ndugulile amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu na pia kujua ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kwa kiasi gani nchini.
Dk Ndugulile alisema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikitilia mkazo afya ya uzazi kwa wanawake na tafiti nyingi zimekuwa zikihusu upande huo mmoja.
Alisema mpaka sasa bado haujafanyika utafiti kuhusu hali ya afya ya uzazi kwa wanaume, japokuwa tatizo hilo linazungumzwa miongoni mwa wanajamii.
“Bado hatujafanya utafiti wa kina kujua tatizo hili ni kubwa kwa kiasi gani. Suala hili ni gumu kulisemea kwa maana ukiangalia takwimu ya uzazi Tanzania kwa maana ya ongezeko la watu na idadi ya kina mama kukua unaona kabisa kwamba bado hatuna shida,” alisema.
Hata hivyo, alisema takwimu za sayansi duniani zinaonyesha kuwa wanaume wengi wana matatizo ya nguvu za kiume, sababu kubwa ikiwa ni mtindo wa maisha.
“Tatizo hili sisi wenyewe tunachangia kwa kula bora vyakula na si chakula bora hasa vyenye mafuta kwa wingi na sukari. Hivi vinachangia sana katika magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kupungua kwa nguvu za kiume. Pia, kutofanya mazoezi, matumizi ya vilevi ikiwamo pombe na sigara navyo ni visababishi vikuu,” alisema Dk Ndugulile na kuongeza kuwa kuku wanaofugwa kwa kutumia dawa mbalimbali huathiri walaji.
Dawa za nguvu za kiume
Wakati Wizara ya Afya jana ikitangaza kuzisajili dawa tano za asili ikiwamo ya Ujana iliyothibitishwa kutibu tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, imebainika kuwa zipo dawa ambazo si za asili za kutibu tatizo hilo katika maduka ya dawa.
Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza alisema dawa ambazo zimesajiliwa baada ya kuchunguzwa na kuonekana zinafaa kutumiwa na binadamu ni za aina mbili, “Sildenafil pamoja na Tadalafil zinazotoka nchi za nje, zimechunguzwa na TFDA na kuonekana hazina sumu wala madhara kwa watumiaji, hizi zinapatikana maduka mbalimbali ya dawa za binadamu,” alisema Simwanza.
Utafiti uliofanywa na daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Henry Mwakyoma aliwahi kufanya utafiti kuhusu ukosefu wa nguvu za kiume na ugumba.
Alisema, ukosefu wa nguvu za kiume ni kukosa uwezo wa kufanya tendo la ndoa na ugumba ni uwezo hafifu wa mbegu za mwanamume kuzalisha.