Serikali yaahidi neema mgodi wa dhahabu Irasanilo

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa akiweka jiwe la Msingi katika jengo la soko la madini lililojengwa wilayani Butiama na wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi  wa dhahabu wa  Irasanilo uliopo wilayani humo. Picha na Beldina Nyakeke.

Muktasari:

Mgodi wa dhahabu wa Irasanilo uliopo katika eneo la Buhemba wilaya ya Butiama umezalisha zaidi ya Kilo116.473 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh3.373 bilioni katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu.

Butiama. Mgodi wa dhahabu wa Irasanilo uliopo katika eneo la Buhemba wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara umezalisha zaidi ya Kilo 116.473 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh3.373 bilioni katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2022.

 Kutokana na uzalishaji huo, Serikali imepata zaidi ya Sh235.95 milioni kama mrabaha katika kipindi hicho.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumapili Desemba 4, 2022 mgodini hapo na meneja wa mgodi huo, Isaya Daudi alipokuwa akitoa taarifa kwa Naibu waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa aliyefanya ziara mgodini hapo.

Meneja huyo amesema mgodi huo unaomilikiwa na umoja wa wachimbaji wadogo wapatao 387 pia umefanikiwa kujenga soko la madini katika eneo hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh205 milioni jengo ambalo lipo hatua za ukamilishaji na kuiomba Serikali kutangaza soko hilo kuwa soko rasmi la madini la wilaya hiyo.

"Mgodi huu mbali na kuchangia pato la Serikali na kujenga soko lakini pia umetoa ajira rasmi 77 kwa wataalam mbalimbali na kuna wachimbaji wadogo zaidi ya 4,000 pamoja na akinamama 80 wanaotoa huduma kuzunguka eneo la mgodi," amesema

Amesema uzalishaji huo umefanywa katika mialo 249 iliyosajiliwa mgodini hapo baada ya Serikali kutoa leseni ndogo za uchimbaji 15 ambazo zinamilikiwa na wanachama wa umoja huo.

Akizungumza na wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Madini, Dk Kiruswa amewapongeza wachimbaji hao kwa kujenga soko hilo la madini huku akisema baada ya ukaguzi amebainijengo hilo linakidhi vigezo pamoja na thamani ya fedha.


Kuhusu ombi la kuwa soko la madini la wilaya, Dk Kiruswa amesema kwa kuanzia jengo hilo litakuwa kituo cha kununua madini wakati utaratibu ukifanyika ili kituo hicho kiweze kupandishwa daraja na kuwa soko la maindini.

"Kuna vigezo vya kufuata ili eneo liweze kuwa soko la madini na kigezo kimojwapo ni uzalishaji ingawa jengo lenyewe lina hadhi sasa malizeni kwanza ujenzi na hiki kianze kwanza kama kituo kisha tufanye ufuatiliaji ili tuone kama mnakidhi vigezo," amesema

Dk Kiruswa pia ameupongeza mgodi huo kwa kuwa wa kwanza kwa ulipaji  wa kodi za Serikali kwa migodi ya hadhi hiyo mwaka jana jambo ambalo linapaswa kuigwa na migodi mingine hasa ikizingatiwa mgodi huo umeanzishwa  miaka mitatu iliyopita.