Serikali ya Tanzania yashinda kesi Marekani

Muktasari:
- Serikali ya Tanzania imeokoa Dola milioni 55 za Marekani (zaidi ya Sh100 bilioni) baada ya kushinda kesi iliyofunguliwa katika mahakama ya Colombia nchini Marekani na familia ya Vipula Valambhia dhidi ya Tanzania.
Morogoro. Serikali ya Tanzania imeokoa Dola milioni 55 za Marekani (zaidi ya Sh100 bilioni) baada ya kushinda kesi iliyofunguliwa katika mahakama ya Colombia nchini Marekani na familia ya Vipula Valambhia dhidi ya Tanzania.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Aprili 24, 2021 na wakili mkuu wa Serikali, Gabriel Malata mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya elimu na ustadi wa kazi kwa mawakili wa Serikali.
Amesema uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa Aprili 19, 2021 baada ya familia ya Valambhia kushindwa kutokana na hoja mbalimbali zilizotolewa na mawakili wa Tanzania ikiwemo ya familia hiyo si raia wa Marekani na hivyo kukosa sifa ya kufungua kesi nchini humo.
Amebainisha kuwa kesi hiyo ilikuwa inahusu Serikali ya Tanzania kuingia mkataba wa ununuzi wa vifaa na familia hiyo, na ilitekeleza majukumu yake kulingana na mkataba lakini familia hiyo iliona kuna upungufu katika utekelezaji wa mkataba huo.
‘’Familia ilichokifanya kwa kile ilichoamini kwamba ni halali kwa upande wao ikaamua kwenda kufungua kesi, katika kufungua kesi huko wakadai kulipwa kiasi cha dola milioni 55 ambayo ni sawa na zaidi ya bilioni mia za Tanzania,” amesema.
Ameeleza Serikali ilipeleka ushahidi wake kwamba mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo kwa kuwa wahusika si raia wa nchi hiyo.
Amesema mahakama ya Colombia ikakubaliana na hoja za Serikali ya Tanzania, “baada ya hapo hawakuridhika na kuomba idhini ya kufanya marejeo ya kesi katika mahakama ya juu ndani ya mahakama za Marekani na hapo Serikali ilipambana nao na kushinda tena.”
Amesema kesi zilizofunguliwa nje ya nchi zilikuwa nne, kwamba Serikali imeshinda mbili na mbili zinaendelea.