Serikali kuwalipa posho, kuwalinda mashahidi mahakamani

Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania, Dk Pindi Chana akizindua miongozo mitatu ikiwamo mwongozo wa kumjali na kumlinda shahidi leo Jumatano Septemba 27, 2023.
Muktasari:
- Serikali imezindua miongozo mitatu inayotoa mwelekeo wa kulinda mashahidi kabla na baada ya kutoa ushahidi, kuongeza kasi ya ushirikiano wa taarifa za ushahidi kimataifa na kuongeza udhibiti na uratibu wa mali zinazotokana na uhalifu.
Dar es Salaam. Una hofu ya usalama katika ushahidi? Huna sababu tena ya kujenga wasiwasi baada ya Serikali kuweka wazi mwongozo wa kuwajali na kuwalinda mashahidi kabla na baada ya kutoa ushahidi mahakamani.
Kwa sasa mtoa taarifa aliyejitambulisha kutoa ushirikiano, atahakikishiwa kutunziwa siri ya taarifa zote alizotoa. Pili, atasafirishwa kwa gharama za Serikali kutoka mahali aliko na kuhifadhiwa katika makazi yenye faragha bila kuathiri uhuru wake wakati wa utoaji wa ushahidi.
Pia, mwongozo huo unaelekeza kuwajali watu wenye mahitaji maalumu kabla na baada ya kutoa ushahidi bila kuathiri utu wao.
Waathirika, wakiwamo waliofanyiwa vitendo vya ubakaji au kujeruhiwa vinginevyo wanahakikishiwa usalama usiosababisha madhara zaidi na kuathiri uhuru wao wakati wa ushahidi mahakamani na baada ya kutoa ushahidi watawekewa mazingira ya kufuatiliwa usalama wao.
Mwongozo huo chini ya Sheria ya Ulinzi wa Mtoa taarifa na mashahidi Sura 446 ulikuwa ni sehemu ya miongozo mitatu iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana.
“Shahidi wamekuwa wakiogopa kutoa ushahidi kwa sababu mazingira yote yanakuwa yakionyesha anaonekana kwenda kutoa ushahidi, kwa hiyo mwongozo huu umeweka ulinzi wa kutosha kuhakikisha anatoa ushirikiano kwa kulinda usalama wake,” alisema Dk Pindi.
Dk Pindi alitoa wito kwa Watanzania wote kutokuwa na hofu tena wanapohitajika kutoa ushahidi mahakamani, akisema ushahidi husaidia kupunguza matukio ya uhalifu nchini.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Slyvester Mwakitalu, alisema mwongozo huo kuanzia hatua ya upelelezi, shahidi ataanza kuhusishwa ili kuwezesha viwango vya uchunguzi na mashtaka kabla ya kuamua kufungua shtaka au la.
“Kwa hiyo miongozo hii itakuwa msaada mkubwa katika kurahisisha, kuongeza ufanisi wakati wa mashtaka na kuimarisha mfumo wote wa hakijinai.”
Julai mwaka huu, Tume ya Kuboresha mfumo wa Hakijinai iliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeiteua Januari mwaka huu kwa lengo la kuimarisha mfumo huo.
Miongozo mingine
Pia kuna mwongozo wa utaifishaji, urejeshaji na usimamizi wa mali zinazotokana na uhalifu chini ya Sheria ya Mazalia ya uhalifu Sura 256 unaotoa nafasi ofisi ya DPP kukabidhi mali zote zilizotaifishwa kwa Katibu mkuu Wizara ya Fedha kwa ajili ya hatua zaidi baada ya kesi kufikia ukomo mahakamani.
Kuhusu mali zinazoharibika, mwongozo huo unaelekeza mali ziuzwe na fedha ziwekwe katika akaunti maalumu ili kesi itakapomalizika mshtakiwa akabidhiwe endapo atashinda au zibaki Serikalini.
Pili, mali zote zilizopatikana kwa njia ya ubadhirifu wa mali za umma au vifaa zote zilizotumika katika kutenda uhalifu zitataifishwa baada ya kuthibitisha mahamakani.
Mwongozo mwingine wa tatu uliozinduliwa ni mwongozo unaoweka utaratibu wa kusaidia kupata ushahidi kutoka mataifa mengine nje ya nchi au Tanzania kutoa ushahidi katika mataifa mengine.
Mwongozo huo utakuwa ukitekelezwa kuakisi matakwa ya Sheria ya Ushirikiano wa Kisheria katika masuala ya Jinai Sura 254 na Sheria ya Urejeshaji wa wahalifu Sura 368.
Miongozo hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashtaka(DPP), ulihusisha pia taasisi zote husika katika mfumo wa hakijinai Tanzania ikiwamo Takukuru, Jeshi la Polisi, Wizara ya Fedha.
Dk Pindi alisema miongozo hiyo itasambazwa kwa mifumo mbalimbali ili kuwafikia watanzania wote ikiwamo taasisi taasisi za mashtaka zote ngazi za halmashauri nchini, tovuti zote wizara, walalamikaji huku ikiwa sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea mikoani.
Kwanini miongozo
Kabla ya kuzindua, Dk Pindi alisema pamoja na kuwepo kwa sheria husika, ilionyesha uhitaji mkubwa wa kuanzisha miongozo hiyo ili kuongeza ufanisi zaidi katika ushirikiano wa shahidi.
Kuhusu mwongozo unaoweka taratibu za ushirikiano wa kimataifa Mwakitalu alisema licha ya sheria kutoa mwelekeo katika ukusanyaji wa ushahidi na vielelezo lakini yako maeneo hayakubainishwa. “Kwa mfano namna ya kupokea na kutoa ushahidi nchi zinazoomba, muda wa uchunguzi.”