Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Miundombinu kutoungana kikwazo biashara Afrika

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Azindua barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa kilomita 107.14  

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuitumia vyema fursa ya ujenzi wa miundombinu hasa barabara kufanya biashara na nchi jirani, kwa kuwa si nchi nyingi barani Afrika zinapata fursa hiyo.

Amesema changamoto kubwa inayolikabili Bara la Afrika ni nchi zake kutounganishwa na miundombinu ya barabara tofauti na ilivyo Tanzania ambayo inaungana na baadhi ya mataifa jirani, hivyo ni muhimu kutumia fursa hiyo kufanya biashara.

Rais Samia amesema hayo leo Julai 16,2024 alipokuwa akizindua barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Rukwa.

“Watanzania tumepiga hatua kubwa kwenye kujiunganisha ndani ya nchi na na nchi nyingine. Changamoto kubwa tuliyonayo Bara la Afrika ni kujiunganisha, hii inasababisha ugumu kwenye kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe.”

“Tuna hiari ya kuweka mizigo kwenye meli tupeleke Ulaya lakini siyo ndani ya Afrika kwa sababu hatujaungana. Sisi tuna barabara hizi zinatuunganisha na nchi jirani, tuzitumie kufanya biashara,” amesema.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 107.14   imejengwa kwa thamani ya Sh150. 5 bilioni inatarajiwa kutatua tatizo kubwa la usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Rais Samia amesema kabla ya kuwepo barabara hiyo usafiri kuelekea bandarini ulikuwa unachukua hadi siku nzima lakini baada ya kujengwa ni saa mbili tu.

“Kubwa zaidi ni kwamba barabara hii na bandari zinatuunganisha na nchi jirani za Zambia, DRC na Burundi hii maana yake tunakuza utendaji wa biashara, tunakuza biashara kati yetu na nchi jirani. Mazao mnayolima yanapata urahisi wa kwenda kwenye nchi jirani,” amesema.

Amesema, “miundombinu hii tunayoiweka inatumia fedha nyingi, lazima iwe na kazi za kufanya, barabara isafirishe watu na bidhaa. Ni lazima tuzalishe bidhaa ili barabara na bandari zetu zifanye kazi. Tutakwenda kufanyia kazi suala la meli ya mizigo katika bandari hii,” amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amesema usanifu na ujenzi wa mradi wa barabara umetekelezwa kwa pamoja na Kampuni ya China Railway Seventh Group na New Century Company Limited ya China.

"Mradi huu ulikamilika Aprili 2024 na kugharimu Sh150.5 bilioni zikihusisha ujenzi, ushauri na fidia," amesema.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali pia inajenga barabara ya Matai-Kasesya (kilomita 50) ili kuboresha zaidi usafiri na usafirishaji na nchi jirani.

Rais Samia pia alizindua vihenge na maghala ya kuhifadhia mazao akiwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao yote kwa sababu  yamekuwa biashara.

“Rukwa ni kanda pekee inayojitegemea katika kilimo, ununuzi na uhifadhi wa nafaka. Hii ni kwa sababu wakulima mnalima kwa jitihada kubwa. Hili tulilolifanya leo (jana) ni kunusuru nguvu ya mkulima, zamani baada ya mavuno chakula kingi kilikuwa kinaharibika na kupotea kwa kutokuwa na hifadhi za maana, lakini sasa tunajenga maghala na vihenge vya namna hii ili wakulima mnapovuna Serikali tuweze kununua na kuhifadhi kwa haraka,” amesema.

Aliwaomba wakulima kutouza mazao yao kinyemela kwa kile alichoeleza kufanya hivyo ni kuinyima Serikali mapato.

Alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere na wakuu wa wilaya kufuatilia kwa ukaribu na kuhakikisha kila anayeuza mazao nje ya nchi anafanya hivyo akiwa na kibali na ameyanunua kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakua (NFRA).

“Ombi langu kwenu wakulima mnapaswa kutambua kuwa chakula mnachokilima ni mali ya Watanzania, lakini Serikali yenu inatoa ruzuku kwenye mbolea, inalipa huduma za ugani hii yote ni gharama ambayo tunatarajia itarudi tutakapouza chakula nje ya nchi,” amesema.

Rais Samia pia aliweka mawe ya msingi katika Chuo cha Veta mkoani Rukwa, uwanja wa ndege Rukwa, chuo cha ualimu na alizindua jengo la Halmashauri ya Kalambo.