Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za watu kumi kuhukumiwa kunyongwa

Tanga. Yalikuwa ni mauaji kikatili, ndivyo unavyoweza kuelezea tukio alilofanyiwa mlinzi wa Ofisi ya Kijiji cha Lulago, Wilaya ya Kilindi, Mbwana Salim, aliyechinjwa na kundi la waumini wa Ansuar Sunna wenye msimamo mkali, wakitaka wenzao wawili waliokuwa wanashikiliwa humo waachiwe.

Kabla ya tukio hilo, Oktoba 22, 2013, watu wawili, Juma Omary Mtana na Rajabu Omary Mtana ambao ni ndugu, walikamatwa na kuwekwa mahabusu katika ofisi ya kijiji hicho kwa madai ya kupigana na mwenyekiti wa kijiji na sungusungu.

Kiini cha mtafaruku huo ilielezwa ni kutokana na wawili hao kugoma kulipa ushuru wa mauzo ya iliki na katika mtafaruku huo, mgambo wa kijiji walijeruhiwa na kisha ndugu hao wawili wakakamatwa na kuwekwa mahabusu.

Siku iliyofuata, kundi la waumini wa madhehebu ya Answar likihusisha watu takribani 20, walifika kijijini saa 11 asubuhi wakiwa na bunduki, fimbo na mapanga kwa lengo la kuwaokoa wenzao, na miongoni mwao mmoja alimshambulia mgambo huyo kwa fimbo.

Mgambo huyo, kulingana na ushahidi, alianguka chini na mmoja wa watu hao aliyekuwa na panga alimkata shingo kwa nyuma na kusababisha kifo chake papohapo, huku wengine wakiendelea kumpiga kwa fimbo miguuni na mmoja akamkata tumboni.
Kiongozi wao aliwaamuru kuchukua ‘sunna’, akimaanisha kuendelea kumkata kwa mapanga katika maeneo yote ambayo tayari alikuwa amekatwakatwa na wengi katika kundi hilo walitekeleza amri hiyo kabla ya kutawanyika.
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wahusika walitoweka kijijini hapo na wengine walibakia, wakiwemo waliokamatwa siku hiyohiyo na wengine siku iliyofuata. Watuhumiwa wengine walikamatwa baada ya mwezi mmoja katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Miongoni mwa waliokamatwa, 20 walifunguliwa mashtaka ya mauaji ya kukusudia na juzi Mahakama Kuu chini ya Jaji Mfawidhi Latipha Mansour iliwatia hatiani 10 miongoni mwao na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni pamoja na Haji Omary Mtana, Khalid Sekintu, Omary Said, Toba Sekintu, Abdallah Mrisho, Mnyamisi Saidi, Abdulrahman Hassan, Juma Mtana, Ramadhan Mngumi na Jawa Mtana.
Mahakama hiyo iliwaachia huru washtakiwa kumi, akiwemo Ramadhan Miraji maarufu kwa majina ya Abu Mohamed au Master ambaye upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake pasipo kuacha mashaka.

Washtakiwa hao awali walisomewa mashtaka ya ugaidi ambayo baadaye yalibadilishwa na kuwa ya mauaji ya kukusudia.
Washtakiwa tisa waliachiwa katika maamuzi madogo baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu.

Hii ni hukumu ya pili katika miaka ya karibuni kwa Mahakama Kuu kuwahukumu watu wengi kunyongwa hadi kufa baada ya ile ya Desemba mwaka jana, iliyohusisha watu 11 baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua mwanaharakati wa mapambano dhidi ya ujangili wa tembo, raia wa Afrika Kusini, Wyne Dereck Lotter.
 

Ushahidi wa tukio

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka aliieleza kuwa waumini wa Answar Sunni walikuwa wakitishia amani Kijiji cha Lulago tangu mwaka 2012 baada ya Haji Omari Mtana kugoma kulipa ushuru kwa madai hawezi kuilipa Serikali ya makafiri.

Viongozi wa kijiji wakatuma mgambo kwenda kumkamata na ndugu yake Juma Omary Mtana lakini wakawashambulia mgambo pamoja na viongozi wa kijiji.

Alisema polisi walijulishwa na walifika na kuwachukua ndugu hao wawili na kuwapeleka Kituo cha Polisi Songe kilichopo Kilindi na baada ya hapo wafuasi wa Answar Sunna walijikusanya kambi za Lwande na Lulago na kwenda ofisi ya kijiji.

Walikuwa wamebeba silaha za moto, mapanga na fimbo na walipofika ofisi ya kijiji walimshambulia mlinzi (mgambo) aliyekuwa analinda na kumuua papo hapo.

Kulingana na uchambuzi wa ushahidi huo, shahidi huyo alikuwepo eneo la tukio na alishuhudia tukio lote na aliweza kuwatambua baadhi ya wale walioshiriki na aliwataja kwa majina na kufafanua yupi alifanya nini na nani alimchinja Salim.

Shahidi wa nne wa upande wa mashtaka hakutofautiana sana na shahidi wa tatu katika ushahidi wake, bali aliongeza kuwa baada ya marehemu kuwa amechinjwa, mshtakiwa wa 17, Sheikh Mhadu aliwaagiza wafuasi hao kuchukua sunna.

Katika kutoa amri hiyo, Sheikh Mhadu alisikika akitamka kwa sauti “Kila mmoja aje achukue sunna…,” na kutokana na amri hiyo, watu hao walienda kumkata marehemu maeneo ambayo tayari yalikuwa na majeraha.
Alienda mbali na kumtaja ‘Master’ kwamba ndiye alikuwa na bunduki na alifyatua risasi juu ili wanakijiji wasimwokoe Salim.

Shahidi wa tano na sita walitoa ushahidi unaofanana wa namna kundi hilo lilivyotekeleza mauaji hayo, lakini shahidi wa sita alisema aliposikia wanasema Takbir na wengine wanaitikia Allah Akbar alienda kujificha umbali wa kama mita 30.
 

Uchambuzi wa jaji

Jaji Latipha alisema ushahidi wa mashuhuda hao wanne, uliwataja waziwazi na kuwatambua washtakiwa 10 isipokuwa mshtakiwa wa 16, Ramadhan Miraji ‘Master’ ambaye baadhi walimwita Master na wengine Abu Master.

“Utambuzi wa mshtakiwa wa 16 haukuwa wazi na ni wa mashaka na hivyo kumpa faida mshtakiwa. Hakutambuliwa kikamilifu na hivyo hakuwa miongoni mwa wale waliokuwepo katika mkusanyiko ule usiokuwa wa halali,” alieleza Jaji.

“Washtakiwa wengine wote walionekana, kujulikana na kutambuliwa na mashuhuda. Hakuna sababu ya kutozingatia ushahidi wa mashuhuda hao walioona kila kitu, tena mchana kweupe wakati mauaji yakifanyika,” alisisitiza Jaji Latipha. Alisema ushahidi mwingine uliokuwa na thamani ni wa maungamo ya mshtakiwa wa 19, Juma Mtana ambaye katika maelezo yake, alikiri kuwepo eneo la tukio, kushiriki mauaji na kuwataja watu wengine aliokuwa nao.

Kulingana na ushahidi huo, jaji alisema washtakiwa walikwenda eneo la tukio wakiwa na silaha na lengo moja la kuwashambulia watumishi wa Serikali.
“…walimshambulia marehemu bila huruma kwa kutumia fimbo na mapanga na kulikuwa na mapigo kadhaa, na baada ya kumuua walitoroka na kwenda kujificha Morogoro, Dodoma na wengine walibakia kijijini,” alisema.

“Walikuwa na nia ovu, hivyo haijalishi nani alifanya nini katika ghasia hizo. Kwa kuwa walikuwepo na kwa kuwa imethibitishwa washtakiwa wote walijikusanya na kwenda eneo la tukio basi walikuwa na lengo la pamoja kutenda kosa.
“Ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa mzito na madhubuti na hapakukosekana muunganiko. Dosari ndogo ndogo katika ushahidi wa Jamhuri hazileti mashaka yoyote kuwa ushahidi wao ulikuwa ni mzito,” alieleza Jaji.

Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji alisema adhabu wanayostahili kwa kitendo walichofanya ni kunyongwa hadi kufa, hivyo akawahukumu washtakiwa 10 adhabu hiyo ya kifo huku akimwachia huru mmoja, ‘Master’, kwa kukosekana ushahidi.
 

Hukumu waliomuua Lotter

Desemba mwaka jana Mahakama Kuu iliwahukumu watu 11 adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua Wyne Dereck Lotter.

Jaji Leila Mgonya aliyesikiliza kesi hiyo alisema ushahidi wa mashahidi 32 wa upande wa mashtaka na vielelezo walivyotoa mahakamani vilithibitisha makosa dhidi ya washtakiwa bila kuacha mashaka yoyote.

Raia wawili wa Burundi walikuwa miongoni mwa watu waliohukumiwa kunyongwa kwa mauaji hayo, yaliyodaiwa kusababisha mshtuko kwa wapambanaji wa ujangili nchini na jumuiya ya kimataifa.

Lotter, aliyekuwa na umri wa miaka 51 aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 16, 2017 katika makutano ya Barabara za Chole na Haile Selassie, Masaki, Dar es Salaam wakati akipelekwa hotelini na teksi muda mfupi baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JNIA).