Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu ‘Mshirika’ wa Mackenzie kufutiwa mkutano Arusha

Waumini wa mchungaji Ezekiel Odero wakiwa wanaendelea na maombi kabla ya  kuamriwa na Serikali  kusitishwa ibada hiyo jijini Arusha jana. Picha Mussa Juma

Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha jana ilifuta mkutano wa injili ambao mhubiri Ezekiel Odero wa Kanisa la New Church la Kenya, alitarajiwa kuhubiri.

Odero anatajwa kuwa mfuasi wa mhubiri Paul Mackenzie, anayedaiwa kusababisha vifo vya waumini wake zaidi ya 340 nchini Kenya.

Mhubiri Odero akishirikiana na mwenzake Soni Nabii wa Tanzania, waliandaa mkutano huo katika uwanja wa shule ya msingi Ngarenaro uliopewa jina siku tatu za kubadilishwa na Mungu, uliokuwa uanze jana hadi Julai 16.

Wakati mamia ya watu wakiendelea na maombi jana saa tano asubuhi, kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Arusha ilisitisha kibali cha mahubiri hayo.

Polisi waliofika kwenye eneo hilo waliwaondoa wakiwataka kutawanyika.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini alitoa sababu nne za kuzuia kibali ambacho awali kilitolewa na jiji hilo.

Alisema kimesitishwa baada ya utaratibu kutofuatwa kwa kuwa ofisi yake haikuwa na taarifa.

"Utaratibu wa barua zote za Jiji ni lazima zianzie kwa Mkurugenzi, lakini kilichotokea ni kuwa barua ilikuwa inashughulikiwa na ofisa utamaduni na hadi kutoa kibali kwa niaba yangu bila mimi kujua," alisema.

Alisema alipaswa kupelekewa barua ya maombi ya uwanja, yeye kujadiliana na maofisa wengine wa Serikali na ndipo kibali kitoke.

Sababu ya pili alisema Odero ametajwa kwenye tuhuma za vifo vya waumini nchini Kenya, hivyo kumkaribisha huenda kungesababisha sintofahamu.

Nyingine ni eneo alilopewa kufanyia mkutano kuwa la shule na wanafunzi walikuwa wakiendelea na mitihani.

Sababu ya nne ni kutokana na hofu ya kusambaa ugonjwa wa matumbo ambao umeibuka katika baadhi ya maeneo jijini hapo.

"Kwa umati wa watu pale tungeweza kupata janga jingine la ugonjwa wa matumbo," alisema.

Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema hatambui kibali walichopewa wahubiri hao kwa kuwa eneo walilopewa ni la shule na kwamba alipowasiliana na uongozi wa shule ulisena hauna taarifa. Hata hivyo, anasema jana mchana alipata taarifa za kusitishwa mkutano.

Baadhi ya waumini waliowasili na magari kutoka Kenya na wengine wilaya za jirani walilalamika kusitishwa kwa kibali cha mkutano huo.

Jana Odero hakuwa tayari kuzungumzia sintofahamu hiyo, kutokana na kuwa katika mashauriano na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Arusha na Mkoa.

Hata hivyo, juzi akizungumza na waandishi wa habari alisema hana ushirikiano na mchungaji yeyote aliyesababisha vifo vya waumini.

Alisema amekuja Arusha kuwaponya wagonjwa kupitia maombi ambayo angetoa na aliomba watu wenye matatizo kufika uwanja wa shule ya msingi Ngarenaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema baada ya kupata taarifa za mkutano huo lilikuwa linazifanyia kazi. Hadi jana saa moja usiku muhubiri huyo alikuwa akiendelea na majadiliano na viongozi wa Jiji.