Saba wafariki baada ya kula kasa, wamo watoto sita

Muktasari:
- Watu sita wa familia tofauti wamefariki dunia mkoani Pwani kwa kula samaki aina ya kasa anayesadikiwa kuwa na sumu.
Mafia. Watu saba wamefariki dunia baada ya kula samaki aina ya kasa anayesadikiwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Bweni na Kanga Wilayani Mafia Mkoani Pwani.
Watu hao wanatoka kwenye kaya nne tofauti kijijini humo na walifariki kwa nyakati tofauti Machi 12 mwaka huu mara baada ya kula samaki hao.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa kipolisi Rufiji, Canute Msacky amesema kati ya watu hao saba waliopoteza maisha ni watoto sita.
Kamanda Msacky ametaja majina ya waliokufa ni Mohamed Makame umri miezi Saba, Minza Hatibu (miezi kumi), Ally Seleman (miezi nane), Ramadhan Karimu (miezi nane), Abdala Nyikombo (miaka 4), Makame Nyikombo (miaka tisa) pamoja na Salima Mjohi (miaka 28).
"Ni kweli tukio lipo ni watoto sita wa kuanzia miezi saba na mtu mzima mmoja ndio wamefariki, na taarifa za awali ni kwamba wamekufa baada ya kula samaki aina ya kasa anayesadikika kuwa na sumu, na hawa watu walipoteza maisha kwa nyakati tofauti tofauti kuanzia usiku majira ya saa Moja Machi 12 "amesema Kamanda Msacky.
Ameongeza kuwa miili ya marehemu wote imeshafanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika hospitali ya Wilaya ya Mafia na tayari wameshakabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Kuhusu chanzo cha tukio hilo, amesisitiza kuwa bado kinaendelea kuchunguzwa.
Aidha Kamanda Msacky ameeleza tayari watuhumiwa watatu wanashikiliwa na Jeshi hilo kwa mahojiano zaidi.
"Tumefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa mahojiano zaidi ambao nao wamelazwa hospitali ya wilaya hapa Mafia baada ya kuzidiwa wakiwa chini ya uangalizi wa Jeshi hilo kwani nao walikula nyama ya samaki huyo" ameongeza
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mafia limetoa wito kwa wavuvi kuacha tabia ya kuvua samaki aina hiyo ya kasa ambao ni nyara za Serikali.
Kamanda Msacky ameshauri wafuate kanuni na sheria za uvuvi wa samaki hao kwani Polisi wataendelea kuchukua hatua kali kwa wavuvi wasiofuata taratibu na sheria za nchi.