Russia yajipanga kuwekeza kilimo cha ndizi, chai na kahawa

Balozi wa Russia nchini Tanzania, Andrey Avetusyan akizungumza katkka maadhimisho ya siku ya Kitaifa ya Russia katika maonyesho ya Sabasaba
Muktasari:
- Uwekezaji wa Russia nchini Tanzania unalenga kuongeza wingi wa bidhaa za zinazouzwa nchini humo
Dar es Salaam. Kampuni kutoka nchini Russia zimekuja Tanzania kutafuta fursa za uwekezaji katika kilimo hususani cha ndizi, kahawa na chai huku zikionyesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea.
Kwa sasa Tanzania inauza bidhaa za Sh17.008 bilioni katika soko la Russia huku ikinunua bidhaa za Sh475.69 bilioni.
Hayo yameelezwa leo Juni 10, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Russia yaliyofanyika katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Balozi wa Russia nchini, Andrey Avetisyan amesema anaamini kampuni kutoka nchini kwake alizoambatana nazo zitamaliza mazungumzo kwa kusaini mikataba ya ushirikiano ya muda mrefu.
Amesema kama ubalozi upo tayari kusaidia wafanyabishara wa Russia katika kuanzisha ushirikiano, kuwekeza Tanzania na kuzalisha bidhaa kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda nchini kwao.
Mbali na jambo hilo ambalo litaongeza wingi wa bidhaa za Tanzania zinazouzwa Russia, pia utawezesha bidhaa za Russia kuendelea kuingia katika soko la Tanzania hivyo kupunguza urari wa biashara.
“Mazao ya kilimo ndiyo bidhaa kuu inauzwa sana Russia kampuni nyingi ambazo zinanunua bidhaa hizo wameona ubora wa mazao yanayozalishwa na wamekuja ili waweze kiwekeza katika kilimo,” amesema Andrey.
Amesema kampuni hizo zina nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa ndizi, kahawa, chai na wanaweza kusaidia kuongeza thamani ya kilimo cha Tanzania kwa kuzalisha mbolea nchini.
Russia ni muuzaji mkubwa wa mbolea nchini Tanzania hali inayotengeneza soko la uhakika jambo ambalo anaeleza utayari wa nchi yake katika kuwekeza.
“Tunaamini kuwa kampuni zetu za kuzalisha mbolea zitakuja kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea nchini Tanzania,” amesema Andrey.
Hili linafanyika wakati ambao uuzaji wa mazao ya chakula nje ya nchi unazidi kuongezeka huku chai na kahawa ikiwa miongoni mwa mazao yanayouzwa sana nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Serikali imeamua kuja na siku maalumu za nchi mbalimbali ili kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi hizo.
“Kupitia siku kama hii na mikutano ambayo sekta binafsi ya Tanzania na Russia wanakutana wanajadili mbinu mbalimbali. Hii ni nafasi yetu kuwakaribisha Russia waje kuwekeza katika kilimo, madini, biashara, utalii na hata sekta ya michezo na sanaa,” amesema Msigwa.
Ametumia nafasi hiyo kuwaita wawekezaji katika sekta ambazo hazijatumika nchini huku akiwahakikishia mazingira ya uwekezaji.
“Tunapohimiza uwekezaji huu kama Watanzania na sisi tunapata kuona fursa zilizopo kwenye nchi zao na kushirikiana nao, katika hili tunapata mitaji na teknolojia itakayosaidia kuboresha uzalishaji wetu na njia zetu za kibiashara,” amesema Msigwa.
Russia imepiga hatua katika teknolojia wakati ambao Tanzania bado inatumia teknolojia ndogo katika uzalishaji, hivyo kuwapo kwa ushirikiano huo ni moja ya njia ya kuimarisha uzalishaji.