Rushwa ni kilio uombaji zabuni

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango (wa pili kushoto), akipokea tuzo ya shukurani  kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),  Angelina Ngalula, kwa kutambua mchango wa mheshimiwa rais katika  mafanikio ya  sekta binafsi nchini. Hafla hiyo ilifanyika wakati wa maadhimisho ya siku ya Sekta Binafsi jijini Dar es Salaam juzi. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki. Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

Wakati Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ikimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mamlaka za usimamizi kwa kuboresha mazingira ya biashara nchini, Serikali imewaonya wafanyabiashara kuepuka rushwa wanapoomba zabuni, kwani vitendo hivyo ni jinai inayostahili adhabu kali.


Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ikimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mamlaka za usimamizi kwa kuboresha mazingira ya biashara nchini, Serikali imewaonya wafanyabiashara kuepuka rushwa wanapoomba zabuni, kwani vitendo hivyo ni jinai inayostahili adhabu kali.

Ingawa ulipaji kodi umeongezeka miongoni mwa wafanyabiashara, Serikali imesema kuna mambo machache yanayochangia kupoteza fedha za umma.

Angalizo hilo lilitolewa juzi usiku na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwenye uzinduzi wa siku ya sekta binafsi Tanzania (TPSD) alikomwakilisha Rais Samia, aliyetunukiwa tuzo ya heshima kwa kusimamia uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara nchini kwa miaka miwili aliyodumu ikulu.

Kati ya vitu alivyosema haviko sawa, ni ukwepaji kodi. Dk Mpango alisema ingawa kuna ushirikiano mzuri wanaoupata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha kuwawezesha kukusanya zaidi ya Sh2 trilioni kila mwezi, bado kuna wafanyabiashara wanakwepa kodi hivyo akawakumbusha kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa sheria.

Hata kwenye uombaji zabuni, eneo ambalo Serikali inatumia fedha nyingi za bajeti, Makamu wa Rais alisema kuna utaratibu unavunjwa kutokana na ushawishi wa fedha.

“Baba wa Taifa alituonya kuhusu rushwa ambayo ni adui wa haki. Naomba sisi sote tushirikiane kwenye mapambano dhidi ya rushwa, kwani kuna wafanyabiashara wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Serikali kutoa rushwa hasa kwenye kuomba zabuni,” alisema Dk Mpango.

Akizungumza na wafanyabiashara hao waliowakilishwa na vyama vyao vya kisekta, Dk Mpango alisema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kulinda mazingira, ingawa haifanyi vizuri kuchangamkia fursa na rasilimali za kimataifa.

Katika kuboresha hali hiyo, aliitaka sekta binafsi nchini kushirikiana na ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia mazingira, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na ofisi za ubalozi kuchangamkia rasilimali fedha zilizopo kimataifa, akitolea mfano biashara ya hewa ya ukaa, fedha zinazotolewa na Mfuko wa Green Fund, urejelezaji taka na miradi ya aina hiyo.

“Serikali imekusudia kufanya kazi na sekta binafsi katika miradi mbalimbali, mfano kwenye kilimo na ujenzi wa barabara. TPSF kaeni chini na Wizara ya Fedha kuona namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki kutekeleza miradi ya ubia. Jukwaa hili mnalianzisha leo naamini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, ni jambo zuri, ila Serikali ingependa kuona mnaziwezesha kampuni zinazochipukia ili kuwashirikisha Watanzania wengi zaidi kujenga uchumi wa nchi na kukuza kipato,” alisisitiza.

Katika mkakati wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini, Dk Mpango alimwagiza Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kuzichukulia hatua mamlaka zitakazoonekana zinakwamisha utekelezaji wa mapendekezo ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (blueprint).

Akieleza sababu za kumtunuku Rais, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula katika miaka miwili ya uongozi wake, amefanya mapinduzi yaliyorahisisha biashara na uwekezaji sambamba na kuufufua uchumi, licha ya changamoto za vita vya Ukraine na janga la Uviko-19, huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa tofauti na ilivyo katika mataifa mengine duniani.

“Mazingira ya biashara yameboreshwa na kuimarishwa, sasa yanatabirika, hivyo kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani hata nje. Uhusiano kati ya sekta binafsi na Serikali nao umeimarika kwa kuboresha sera na sheria, hivyo kuchochea kukua kwa uchumi,” alisema Angelina.

Ndani ya miaka hii miwili ya uongozi wa Rais Samia, alisema vikwazo vya uuzaji bidhaa za Tanzania nje ya nchi vimeanza kuondolewa na sasa masoko ya kikanda na kimataifa yanapatikana, likiwamo Soko Huru la Afrika (AfCTA), huku wamachinga wakitengewa maeneo ya kufanyia biashara na benki zikishusha riba ya mikopo.

Akizungumzia namna Tanzania ilivyojipanga kunufaika na soko la AfCTA lenya zaidi ya watu bilioni 1.2, Dk Ashatu Kijaji alisema Tanzania inakamilisha taratibu za kuingiza bidhaa zake huko, ambazo zitakamilika Juni mwakani.

“Maandalizi tunayoyafanya ni uzalishaji endelevu ili upatikanaji uwe wa wakati wote. Tumeshajifunza ubora unaohitajika. Juni mwakani tutaingiza bidhaa tisa na tutahakikisha zitapatikana kwa zaidi ya miaka mitano pindi tutakapoingia. Waliofanikiwa katika biashara walishirikiana. Naomba tushirikiane kuondoa vikwazo vilivyopo na vitakavyojitokeza kuiinua Tanzania,” alisema Dk Kijaji.


Maoni ya wadau

Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa ni matokeo ya kutoutumia vyema mfumo wa kuomba zabuni serikalini (Taneps).

“Tunao mfumo wa kuomba zabuni serikalini, lakini bado kuna rushwa, maana yake mfumo ama unaingiliwa au unachezewa. Kinachohitajika ni kuhakikisha mfumo wenyewe unapokea na kutoa majibu bila mtu kuingilia kati,” alisema.

Vilevile, alishauri utaratibu wa kuwapata wazabuni kwa mfumo wa kumtumia mzabuni mmoja bila kumshindanisha na wengine (single source) udhibitiwe kwa kuimarisha usimamizi kuhakikisha zabuni zinazotolewa zinakuwa na thamani ya fedha.

“Tusipofanya hivyo, jengo lililopaswa kujengwa kwa Sh100 milioni litakamilishwa kwa Sh80 milioni hivyo kukosa ubora unaotakiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovic Utouh alisema rushwa ni kati ya makosa yenye historia ndefu ambayo imekuwapo vizazi na vizazi, hivyo ni muhimu kwa Serikali kuongeze ukali kwa kila tukio litakalothibitika.

“Anayepata zabuni kwa kutoa rushwa ni lazima afidie kiasi alichokitoa kwenye utekelezaji na hapa anayeumia ni mwananchi anayelipa kodi. Mradi huo utatakiwa ukarabatiwe au ujengwe upya ndani ya muda mfupi, hivyo fedha nyingi kutumika kwa kitu kilekile. Ili kufidia, atalazimika kuitekeleza zabuni hiyo chini ya kiwango,” alisema Utouh.

Ripoti mbalimbali, ikiwamo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) hata ya CAG zimeabainisha miradi na huduma kadhaa zenye viashiria vya rushwa.

Uchambuzi wa ripoti za CAG, taasisi ya Wajibu inayoongozwa na Utouh unaonyesha maeneo yenye viashiria vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu wa fedha za umma yameongezeka kwa miaka mitatu mfululizo.

Katika uchambuzi huo wa ripoti za mwaka 2020/21 ya Wajibu, dalili hizo zimeonekana kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa mpaka kwenye mashiriaka ya umma zilizopelekea Serikali kushindwa kukusanya mapato yaliyoainishwa kwenye bajeti na kufanya matumizi yasiyo na tija kisera na kijamii.

“Jumla ya viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kwa mwaka 2020/21 vilikuwa Sh4.59 trilioni, sawa na asilimia 15 ya matumizi yote ya Serikali ambayo ni Sh31.37 trilioni. Kasoro nyingi zilionekana zaidi katika ununuzi wa umma na usimamizi wa mikataba,” inasomeka sehemu ya uchambuzi wa Wajibu.

Kiasi hicho, kiliongezeka kutoka jumla ya Sh1.77 trilioni kilichobainika mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la asilimia 159.

Kwa mwaka 2020/21, Wajibu inasema Serikali Kuu ilikuwa na ongezeko kubwa zaidi kwa viashiria hivyo kuongezeka kwa asilimia 218 kutoka Sh560.19 bilioni mwaka 2019/20 hadi Sh1.78 trilioni mwaka 2020/21, sawa na asilimia 38.81 ya jumla yote ya viashiria vya rushwa.