Rufaa waliotumwa na afande kusikilizwa kesho

Watuhumiwa wa kesi ya ubakaji na ulawiti wakiingia mahakamani leo Agosti 21, 2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Rufaa ya Kesi ya kina Nyundo na wenzake ya kupinga adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kuanza kusikilizwa kesho Juni 3, 2025 Mahakama Kuu Dodoma.
Dodoma. Rufaa dhidi ya adhabu ya kifungo cha maisha gerezani iliyotolewa kwa washtakiwa wanne waliokutwa na hatia kwenye kosa la kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam, aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la X itaanza kusikilizwa kesho Juni 03, 2025.
Wakata Rufaa katika kesi hiyo ni aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Wakata rufaa hao walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Septemba 30, 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam kwenye mahakama iliyoendeshwa kwa faragha.
Mbali na kifungo hicho cha maisha warufani hao pia walitakiwa kumlipa binti huyo kiasi cha Sh1 milioni kila mmoja kutokana na majeraha waliyomsababishia.
Akizungumza na Mwananchi, Wakili wa warufani hao, Godfrey Wasonga amesema taratibu zote za kukata rufaa zimeshakamilika na kesi hiyo itaanza kusikilizwa kesho Juni 3, 2025 Mahakama Kuu ya Dodoma mbele ya Jaji Amir Mruma.
Wasonga amesema wana sababu 33 za kukata rufaa ikiwemo ya upande wa mashitaka kutothibitisha kosa bila kuacha shaka, kutofanyika kwa gwaride la utambuzi kwa washtakiwa, hati ya mashitaka kuwa na dosari na kutojitosheleza kwa ushahidi wa mtandao.
"Tuna sababu 33 ambazo zimetufanya tukate rufaa na kesho kesi hiyo itaanza kusikilizwa mbele ya Jaji Mruma tuna uhakika haki itatendeka," amesema Wasonga.
Warufani hao walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani Agosti, 2025 baada ya video zao kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wakimfanyia ukatili wa binti huyo kwa madai kuwa walitumwa na mtu waliyemtaja kwa jina la afande.