Rostam agusia umuhimu wa elimu Tanzania

Muktasari:
Mbunge wa zamani wa Igunga mkoani, Tabora Rostam Aziz amedai kuwa mfumo wa elimu wa sasa una changamoto inayosababisha uwepo wa wawekezaji uchwara, wanaochukuliwa fursa za wazawa katika maeneo mbalimbali.
Unguja. Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz amedai mfumo wa elimu bado una changamoto inayosababisha uwepo wa wawekezaji uchwara, akishauri kuwepo kwa mabadiliko katika sekta hiyo ili wananchi kutambua fursa zilizopo.
Rostam amesema hayo jana Jumamosi Oktoba 22, 2023 katika mkutano wa kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
Katika mkutano huo, uliofanyika mjini Unguja Rostam ambaye ni mbunge wa zamani wa Igunga alikuwa akizungumzia mada ya ‘elimu kama msingi wa kukuza uchumi na kuzalisha utajiri wa Taifa.’
“Bila elimu madhubuti ndio maana tunapata wawekezaji uchwara, anakuja hapa nchini anakwenda huko kijijini kufungua biashara ambazo zingefanywa na wazawa. Mtu huyo anajiita mwekezaji, hatuwezi kufika popote, lazima tuwe makini na jambo hili,” alisema Rostam.
Alisema ili kukwepa wawekezaji wa namna hiyo, hakuna njia nyingine yoyote ya kufanya bali isipokuwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu itakayowasaidia kuzitambua fursa zinazowazunguka na kuzifanyia kazi.
“Hayo yatafikiwa iwapo kutafanyika mageuzi katika sekta ya kielimu.Tunahitaji mapinduzi katika kuwaanda na kuwafundisha watoto wetu na namna ya kuwapata walimu wanaowafundisha.
“Lazima tuangalie mitalaa kama inakidhi mahitaji yetu. Kukua kwa uchumi kunahitaji ujuzi tofauti na viongozi na watunga sera waangalie tunahitaji kitu ili kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu itakayotoa ajira kwa wananchi,”amesema Rostam.
Akizungumzia kuhusu Maalim Seif, Rostam alisema kiongozi huyo hakuwa mtu wa kawaida na hilo, lilidhihirika alipokutana naye katika mazungumzo yao.
Alisema Maalim Seif alikuwa na dira na ndoto zake za kuona Zanzibar inakuwa kitovu cha biashara katika nchi za Afrika.
“Ili kumuenzi Maalim Seif hakuna budi kuhakikisha yale aliyoyaamini katika kuleta mabadiliko ya uchumi kwa Wazanzibari kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo wa elimu ili kumuandaa mwanafunzi katika kuzitambua fursa badala ya kuwa mtumikishwaji.
Rostamu alitolea mfano wa nchi ya Singapore iliyofanikiwa kwa kupiga hatua za kimaendele, akisema chanzo cha mafanikio hayo ni kuwekeza katika sekta ya elimu bora.
Hata hivyo, Rostam alisema licha ya sekta binafsi kushirikishwa lakini haiwezi kuachiwa mzigo huo bali Serikali inatakiwa mstari wa mbele na kuhakikisha uwekezaji ndani ya sekta hiyo unafanywa.
“Elimu inatoa ujuzi, weledi na kuleta mitaji ili kupata uchumi imara lazima tufanye mabadiliko ya kisera, mitalaa na mifumo yetu,” amesema
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Zanzibar aliungana na maelezo ya Rostam akisema wa aina ya mfanyabiashara huyo wanapaswa kusikilizwa na Serikali.
“Kama ulivyosema Rostam tunahitaji Zanzibar tunahitaji mapinduzi kwenye sekta ya elimu. Ujumbe wako ni mzuri naomba ungepeleke pia makabarasha hayo Serikali,” alisema Mwalimu.