Ripoti: Umaskini chanzo cha uhalifu nchini

Muktasari:
- Ripoti ya Jeshi la Polisi inaonyesha matukio ya kuwania mali yaliongezeka kwa asilimia 7.6 kutoka 21,767 mwaka 2022 hadi 23,414 mwaka 2023.
Dar es Salaam. Umaskini umetajwa kuwa moja ya sababu ya kuongezeka matukio ya uhalifu, watu wakilazimika kutumia njia zisizo halali kujipatia kipato.
Hayo yamo kwenye ripoti ya takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani ya mwaka 2023.
Ripoti hiyo iliyochapishwa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyokusanya taarifa kutoka Jeshi la Polisi Tanzania inaeleza hadi Desemba 2023, matukio ya jinai 607,102 yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio 574,881 yaliyoripotiwa mwaka 2022. Hiyo ni sawa na ongezeko la makosa 32,221.
Kati ya matukio yaliyoripotiwa mwaka jana, makubwa yalikuwa 53,640 na madogo 553,462 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022 ambapo matukio makubwa yalikuwa 54,123 na madogo 520,758.
Kati ya madogo, makosa ya kuwania mali ndiyo yaliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ambayo ni 258,488, makosa dhidi ya binadamu yakifuata kwa kuwa 171,858, huku yale yaliyofanywa dhidi ya maadili yakiwa 123,116.
Mchanganuo wa matukio
Kwa mujibu wa ripoti, matukio ya kuwania mali yaliongezeka kwa asilimia 7.6 kutoka 21,767 hadi 23,414 mwaka 2023.
Matukio hayo ni yanayohusu wizi wa silaha, unyang’anyi katika barabara kuu, unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, wizi, wizi wa pikipiki, magari na mifugo, kuchoma nyumba moto na uhalifu wa kifedha.
Katika kundi hili, uvunjaji ulibeba asilimia 51.57 ya matukio yote yaliyoripotiwa, wizi wa pikipiki ukifuata kwa kuwa na matukio 3,861, wizi wa mifugo ukirekodi matukio 3,762 na unyang’anyi wa kutumia nguvu ukiwa na matuko 1,327.
Kwa upande wa makosa dhidi ya binadamu ambayo yanahusisha mauaji, kubaka, kulawiti, wizi wa watoto, kutupa watoto na usafirishaji haramu wa binadamu yaliongezeka hadi kufikia 13,748 mwaka 2023 kutoka 11,118 mwaka uliotangulia.
Ubakaji ulikuwa kinara kwa kurekodi ongezeko la matukio mengi kutoka 6,827 mwaka 2022 hadi kufikia 8,691 mwaka jana.
Ubakaji ulifuatiwa kwa karibu na ulawiti ambao uliongezeka kwa asilimia 56.9 hadi kufikia 2,488 kutoka makosa 1,586 mwaka 2022.
Mauaji yalirekodiwa kupungua kutoka makosa 2,464 mwaka 2022 hadi 2,303 mwaka jana.
Makosa dhidi ya maadili ya jamii 15 kati ya 16 yaliyoainishwa yalionekana kupungua idadi kasoro moja la kukamatwa na bomu ambalo mwaka 2022 lilikuwa moja na mwaka 2023 yalikuwa matatu.
Matukio katika kundi hili kwa ujumla yalipungua kwa asilimia 22.4 kutoka 21,238 mwaka 2022 hadi matukio 16,478 mwaka uliofuatia.
Yalikoripotiwa
Tathmini ya jumla inaonyesha makosa madogo yamejitokeza zaidi katika mikoa ya kipolisi ya Kinondoni (57,404), Mwanza (47,220), Ilala (36,806), Temeke (34,500) na Morogoro (30,474).
Mikoa au vikosi vyenye idadi ndogo ya makosa katika kundi hili ni Tazara (70), Wanamaji (97), Bandari (109), Viwanja vya Ndege (129) na Reli (186).
Kuhusu mikakati
Katika ripoti hiyo, Jeshi la Polisi limeweka bayana mikakati yake, ikiwemo kuhamasisha jamii hususani vijana kushiriki shughuli halali hasa za ujasiriamali, ili wajipatia kipato.
“Pia kuzishawishi taasisi za fedha zipunguze urasimu wa upatikanaji wa mikopo nafuu na kupunguza riba kubwa zinazotozwa katika mikopo hiyo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo, ikizungumzia matukio ya makosa ya kuwania mali.
Hilo linaenda sambamba na kuhamasisha kuwapo mipango endelevu ya utoaji elimu kwa umma hususan ya ujasiriamali.
Kwa upande wa mauaji ambapo vyanzo vyake vimetajwa kuwa ni wivu wa mapenzi, visasi, tamaa ya mali kinyume cha sheria, ulevi, migogoro ya ardhi au mali na imani za kishirikina, Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa elimu kwa umma.
Elimu hiyo inalenga kuibadilisha jamii iachane na kujichukulia sheria mkononi, jambo litakalofanyika kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwamo za dini.
Maoni ya wachumi
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Uchumi, Dk Balozi Morwa amesema hali hiyo inachangiwa na watu kutokuwa na uhakika na kile wanachotafuta kila siku, ili kujikimu katika maisha yao.
Hiyo inasababishwa na kukosekana ajira, watu kushindwa kujiajiri baada ya kumaliza vyuo kukaa mitaani bila ajira, hali inayofanya waone maisha kwao hayana faida.
Amesema hali hiyo huwa kichocheo kikubwa cha watu kuingia katika uhalifu huku baadhi wakiona bora wafe mapema kwa sababu hawaoni matumaini.
“Katika hili umaskini ndiyo unafanya watu kujiingiza katika uhalifu, wanajua hatari ilivyo lakini kwa sababu hawaoni manufaa ambayo wanaweza kuyapata mbeleni wanaona bora hata kwenda jela kuliko kukaa mitaani,” amesema Dk Morwa.
Amesema si suala zuri kuruhusu kitu kama hicho kuendelea kutokea, badala yake kinachopaswa kufanyika ni kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya watu kujiwezesha kiuchumi.
“Usiruhusu mazingira kama haya, kama watu wanashindwa kuajiriwa na Serikali basi watengenezewe mazingira, ili kujiajiri, kama kote kumebana ni lazima watu watajiingiza katika uhalifu,” amesema Dk Morwa.
Nini kifanyike
Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude amesema hilo linaweza kudhibitiwa kwa watu kupewa elimu ya kuacha kuzaa bila ya kuwa na mipango ya namna ya kule watoto.
Amesema ile tabia ya mtu kuzaa na kudai Mungu atamjalia riziki yake imepitwa na wakati, akieleza zamani watu walikuwa wakitumia kauli hiyo kwa sababu walikuwa na mashamba wakijua watalima na kupata chakula watoto watakula.
“Siku hizi hali haipo hivyo, kuna mambo mengi ya kuzingatia ikiwemo kutafuta chakula, jambo hili halizungumzwi sana, lakini ni wakati wa watu kuwa na mipango sahihi katika uzazi,” amesema Mkude.
Kutokana na kutokuwapo na mpango mzuri katika uzazi, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipata watoto lakini hali zao za maisha si nzuri, jambo linalowafanya waendeleze mnyororo wa umaskini kwa vizazi vyao.
“Baada ya kuzaa unakuwa kiumbe kipya kama mzazi, namna ya kuishi inabadilika majukumu yanabadilika, kuwaambia watu zaeni tu, watu wanapotoshwa, elimu ya uzazi wa mpango na huduma za uzazi wa mpango pia ni vyema zitolewe,” amesema Mkude.
Ameshauri watu wapewe ujuzi kulingana na kile wanachokipenda, ili wajiajiri katika kazi za mikono kuwawezesha kupata riziki.
“Vitu kama hivi vinahitaji fedha na mipango, hivyo lazima kuwe na namna maalumu ya kuangalia watu kama hawa wanafikiwaje na wanasaidiwaje, kuna baadhi ya watu ni maskini na wana watoto ambao hawajui wanawasaidiaje na hata kusoma haijulikani watasomaje,” amesema.
Katika ngazi ya kitaifa amesema ni vyema kuhakikisha uchumi unafanya vizuri, ili maeneo ambayo yanagusa watu ikiwemo upatikanaji wa kazi ndogondogo yafikiwe.
“Usiwe uchumi unaokua katika namba na karatasi, uchumi lazima utengeneze kazi ndogondogo, ili watu waingize kipato. Uchumi ukikaa vizuri watu wapate fedha mifukoni, basi wanaopata watatoa ajira kwa wengine ili wajikwamue kiuchumi,” amesema.