Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUMU: Mtandao hatari wa wahamiaji haramu

RIPOTI MAALUMU: Mtandao hatari wa wahamiaji haramu

Dar/mikoani. Usafirishaji wa wahamiaji haramu ni biashara inayofanywa na mtandao hatari unaokwepa mitego mbalimbali ya Serikali na kuwawanufaisha kwa rushwa wahusika.

Licha ya wengi wao kukamatwa, baadhi yao huikwepa mikono ya Serikali na kufikia malengo yao na kufanya shughuli ya kuwadhibiti kuwa ngumu.

Hata wale wanaokamatwa, Serikali imekuwa inabeba mzigo wa gharama kuwahudumia magerezani huku Jeshi la Uhamiaji likiendesha operesheni mbalimbali kabiliana na changamoto hiyo.

Uchunguzi wa gazeti hili katika mikoambalimbali, umebaini jinsi mtandao huo unavyohusisha baadhi ya watendaji katika vyombo vya dola, waendesha bodaboda, mgambo, maofisa wa uhamiaji na viongozi kadhaa wakiwamo wa vijiji kwenye maeneo husika.

Katika kuifanikisha, njia mpya za panya zimekuwa zikiibuka kila kukicha ili kuwakwepa polisi au maofisa uhamiaji waaminifu wanaopambana na mtandao huo.

Wahamiaji hao wengi wao wanatoka nchi za Ethiopia, Eritrea na Somali wakipitia Tanzania hasa ka mikoa ya Kilimanaro, Arusha na Tanga lengo likiwa ni kwenda Afrika Kusini.

Mkoa wa Kilimanjaro pekee unatajwa kuwa na njia zaidi ya 350 za panya katika vijiji vya mpakani na Kenya katika wilaya za Rombo, Moshi na wilaya ya Mwanga mkoani, huku Tanga ikiwa na njia zaidi 50.

Wakati mikoa hiyo ikitajwa kama uchochoro kwa wahamiaji haramu kutoka Somalia na Ethiopia, mikoa ya Morogoro, Songwe, Dodoma, Morogoro, Manyara na Iringa inatajwa kama njia za kupita kuelekea Tunduma mkoani Songwe kama lango la kutokea kwenda Afrika Kusini.

Inaelezwa biashara hiyo ya kusafirisha wahamiaji haramu ni ya pili kwa kuwaingiza donge nono wanaojihusisha nayo baada ya dawa za kulevya.

Ingawa Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) linasema mhamiaji mmoja hulipa kati ya Dola 1,600 za Marekani hadi Dola 3,000 kusafirishwa kutoka maeneo ya mpaka wa Tanzania na Kenya hadi Tunduma, inaelezwa wengine hulipa hadi Dola 5,000.

Katika uchunguzi huo, gazeti hili limebaini japokuwa Jeshi la Polisi na Uhamiaji wanafanya kazi kubwa kudhibiti biashara hiyo, baadhi ya askari wanashiriki katika mitandao hiyo wakishirikiana na mgambo na viongozi wa vijiji na vitongoji katika njia wanazoingilia.

Wachache hao, wamegeuza biashara hiyo kama mradi wa kujiingizia kipato na ndio husaidia hata kutoa siri za doria.

Mathalan, katika uchunguzi huo, imebainika bodaboda wanaowavusha wahamiaji hao kupitia njia za panya hulipwa kati ya Sh20, 000 na Sh50, 000 kwa kichwa, wakati wamiliki wa nyumba wanakofikia hulipwa hadi Sh100, 000 pamoja na gharama za chakula.

“Hii ni biashara kubwa sana na ndio maana unaona polisi na uhamiaji wanawakamata kila siku lakini wanaofanikiwa kuvuka nao ni wengi. Ukiniuliza nitakwambia ni (biashara) ya pili kwa ukubwa baada ya dawa za kulevya,” anasema mtoa habari wetu.

Chanzo hicho cha habari kililidokeza gazeti hili kuwa kutokana na ukwasi wa biashara hiyo, baadhi ya polisi na maofisa uhamiaji, wanashiriki kuwafundisha ujan ja wale ambao magari yao au pikipiki zimekamatwa zikiwa na wahamiaji hao zisitaifishwe.


Askari, mgambo watajwa

Uchunguzi katika njia wanazozitumia kuingilia mkoani humo, umebaini baadhi ya polisi wa Himo na Mwanga na mgambo wanatajwa kugeuza biashara hiyo kama mradi.

Taarifa hizo zinadai kuwa kwa sasa wahamiaji hao huingia nchini kupitia maeneo ya Madarasani na Kitobo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kisha husafirishwa hadi eneo la Mnoa na Kileo wilayani Mwanga na wachache huhifadhiwa Himo.

“Wanapoingia wanakuja hadi hapa Mnoa, hapo ndio mgawo hufanyikia na kila mtu anaenda na njia yake. Hapo jukumu la kuwasafirisha linabaki la mawakala ambao hutumia usafiri wa pikipiki,” alidokeza mgambo mmoja wa Himo.

“Kila kichwa (mhamiaji) kinalipa Sh50, 000 kwa bodaboda kutoka mpakani hadi Kisangiro na Kileo na sasa hivi hawasafirishi kundi kubwa la watu 20 au zaidi. Hapana. Wanabeba watatuwatatu kwenye pikipiki,” alidai.

Kulingana na vyanzo mbalimbali, baada ya kufikishwa Kileo na Kisangiro, wahamiaji hao husafirishwa wachache wachache hadi Chalinze, Morogoro, Iringa hadi Mbeya ambako husubiri maelekezo ya kwenda hadi mpaka wa Tunduma.

Chanzo kingine kilieleza kuwa kadri Jeshi la Uhamiaji na Polisi wanavyozidisha operesheni Kilimanjaro, ndivyo biashara hiyo inavyolipa kwa kuwa mhamiaji humlipa wakala hadi Dola 5,000 (Sh11 milioni) kutoka mpakani hadi Tunduma.

“Polisi wa Mwanga (baadhi) ndio wanakula kidari (nyama iliyonona). Hao wa Himo ni kama wananusishwa tu. Hapa Mnoa kuna wakati mgambo ndio wanatumika kukusanya. Yaani kama ni mavuno basi hiki ni kipindi cha mavuno,” alidai.

Kutokana na ukubwa wa biashara hiyo, baadhi ya mawakala wamebuni mbinu mpya za kutumia magari ya kifahari (mashangingi) yanayotumiwa na viongozi wa Serikali ili kuvighilibu vyombo vya usalama visishtukie dili hilo.

Matumizi magari ya kifahari katika biashara hiyo lilianza kujitokeza Februari 14, 2022 ambapo polisi mkoa Kilimanjaro kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji walikamata wahamiaji 11 wakiwa katika Toyota Land Cruicer VX.

Hali ikiwa hivyo Kilimamnajro, njia za panya 26 kati ya 50 zilizopo Tanga ni miongoni kwa changamoto zinavyovikabili vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na wimbi la wahamiaji hao.

Licha ya kuwa wimbi la wahamiaji haramu kutoka nchi hizo limepungua kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2022, njia za panya zimebaki ni changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi na Serikali na vyombo vya usalama.

Katika njia za panya 50, njia 26 zinazotumiwa na wahamiaji hao zipo Mkinga kutokana na kuwa na vipenyo visivyo rasmi na mapori makubwa yanayotumika kuwaficha wakati wilayani Handeni wanatumia misitu ya Kabuku na Tengwe.

Tanga mjini kuna maeneo ya Pongwe na Kilapula ambako wahamiaji haramu wanahifadhiwa kwenye mapori wakisubiri kusafirishwa kupitia Muheza na Korogwe.

Maeneo ambayo matukio ya wahamiaji haramu ni kidogo ni ya Lushoto na Kilindi. Watu wanaotajwa kuwa mawakala wa kusafirisha wahamiaji hao wakionekana kuwa na maisha mazuri siku hadi siku licha ya kutokuwa na biashara nyingine halali.

Mkoani Arusha nako, wahamiaji haramu ambao wanaingia kupitia mpaka wa Namanga, pia wamekuwa wakitumia njia za panya na bodaboda nyakati za usiku.

Baada ya kuimarishwa ulinzi mpakani, wahamiaji hao, huvushwa usiku na bodaboda kupitia njia za panya hadi eneo la Oldonyosambu wilaya Arumeru ambako hupakiwa katika magari.

“Hii ni biashara kubwa na ina mtandao mkubwa na hawa wakifika Afrika Kusini wanaenda huko Ulaya,” alisema Mkazi mmoja wa Namanga aliyeomba kuhifadhiwa jina.

Mkazi mwingine wa Mji wa Namanga ambaye kwa sababu za kiusalama tunahifadhi jina lake, alisema baada ya Serikali kuimarisha ulinzi, sasa wahamiaji wachache, kama ilivyo maeneo mengine, wamekuwa wakivushwa usiku na pikipiki maarufu kama bodaboda.

“Serikali inafanya kazi nzuri kuwadhibiti lakini nimeelezwa kuwa sasa wachache wanavuka usiku tena kwa malipo kati ya Dola 20 hadi 50 (Sh45, 000 na Sh112, 500 za Tanzania) Kwa vijana wa bodaboda,” alieleza mtoa habari huyo.

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Edward Mwenda alisema mpaka wa Tanzania na Kenya una vituo rasmi vya kuingilia viwili lakini una njia za panya 350.

Alisema katika njia hizo za Panya 350, 65 ni kubwa ambazo zinapitisha magari na kutokana na uwazi mkubwa wa eneo la mpakani, changamoto ya kudhibiti eneo kubwa mpakani inakuwa kubwa.

Hata hivyo, alisema katika kipindi cha mwaka 2021, wahamiaji haramu 425 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa, Waethiopia walikuwa 157 na Wasomali 42 na wote walichukuliwa hatua mbalimbali.

Kwa kipindi cha Januari hadi Mei, 2022 walikamatwa wahamiaji 107, kati yao kutoka Ethiopia walikuwa 41, Kenya 39 na Somalia 12 na mataifa mengine 15, pamaoja na Watanzania watatu waliokuwa wakiwasafirisha.

Vyombo vya usafiri vilivyotaifishwa kwa kipindi hicho ni magari mawili -- Toyota Land Cruiser, Alteza na pikipiki mbili huku magari mengine mawili ambayo ni Toyota Landcruizer na Alphard pamoja na pikipiki moja yakiendelea kushikiliwa.

Hata hivyo, alisema moja ya changamoto ni baadhi ya wananchi kutokuwa waadilifu ambao hushiriki kusafirisha na kuwahifadhi wahamiaji haramu.

“Katika ukanda wetu wa Sadc (Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika) na Afrika Mashariki tunapaswa kuwa na mbinu za pamoja za kukabiliana na suala hilo, maana kwa sasa tuna msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu katika magereza yetu,” alieleza Mwenda.

Mathalan, alisema mwezi Mei gereza kuu la Karanga la mjini Moshi lilikuwa lina wafungwa na mahabusu raia wa kigeni 369, na wengi kati ya hao ni raia kutoka Ethiopia na wamejaa kwa sababu wanakamatwa kila wakati.

Akizungumzia mikakati, alisema ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma, kufanya doria na kutafuta taarifa za kiintelejensia ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama.

“Wahamiaji haramu wanabadilisha mbinu kila siku na moja ya mbinu waliyo nayo kwa sasa ni kutumia usafiri wa bodaboda, lakini tumeweka msisitizo na kupambana zaidi na mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu,” alisisitiza.

“Tunaelewa biashara ya wahamiaji haramu katika mpaka wetu wa Tanzania na Kenya ina mtandao mkubwa. Mtandao ule unaanzia nchi wanakotoka mfano Ethiopia au Somalia, nchi wanazopitia hadi nchi wanazokwenda,” alisema.

Akizungumzia taarifa za uwepo wa baadhi ya askari kuhusika kusafirisha wahamiaji haramu, Mwenda alisema askari kama huyo ni msaliti na kwamba hawawezi kuwa na mzaha na mtu kama huyo.

“Sisi kama jeshi la uhamiaji na vyombo vya ulinzi tukipata taarifa za askari polisi kuhusika na usafirishaji wa wahamiaji haramu, tunazifanyia kazi kwa haraka sana, kama miongoni mwa askari wetu wanaweza kuwa wachache wasio waaminifu wanahusika na usafirishaji wa wahamiaji haramu tunachukua hatua mara moja”

“Hatuna mzaha wala simile na jambo kama hili, tunaposikia miongoni mwetu kuna watu wachache wanashirikiana na wahamiaji haramu tunalichukulia hilo kama ni usaliti hivyo hatuwezi kulivumilia.”

Kwa upande wake Cleth Mumwi, kamishina msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Songwe, anasema hata mkoani humo tatizo la wahamaiaji haramu lipo.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wamewakamata wahamiaji haramu 205 wakiwemo 64 kutoka Ethiopia na 11 Somalia.

Mumwi alisema idara yake imekuwa ikiwakamata raia hao katika mitego mbalimbali ambapo pia wamekamata magari matatu ambayo yalikuwa yakitumika kuwasafirisha.

Wakati maofisa hao wakieleza hayo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido ulipo mpaka wa Namanga katika Mkoa wa Arusha, Nurdin Babu akizungumza na Mwananchi kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, alionya watu ambao watabainika kusaidia wahamiaji haramu kuingia nchini, akiahidi kuchukuliwa hatua kali.

“Mara kadhaa tumezungumza na wananchi wa Namanga wasiwasaidie hawa wahamiaji na kama wanataka kuingia nchini wanapaswa kufuatia taratibu za kisheria, tofauti na hivyo wajue lazima tu tutawakamata,” alisema Babu.


Dodoma haijaachwa nyuma

Kwa Mkoa wa Dodoma ambao ndio makao makuu ya nchi, hali ya biashara ya wahamiaji haramu nako imezidi kushamiri siku hadi siku kwani kila takribanmiezi mitatu ni lazima wakamatwe huku ikielezwa kuwa wengi hufanikiwa kuvuka salama.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili ukihusisha taarifa za siri za watoa habari ndani ya mifumo, wahamiaji hao wamekuwa wakipita katika barabara ya Kondoa-Chemba- Dodoma licha ya kuwepo geti katika eneo la Mtungutu.

Pia wamekuwa wakitumia barabara za Mtera na Chilonwa ambako hakuna mwingiliano wa magari mengi wala macho mengi ya vyombo vya usalama.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Chemba ambaye anadai baadhi ya askari ambao huwekwa katika geti la Mtungutu wamekuwa wakipokea rushwa ili kupitisha wahamiaji hao.

“Pale gari ni lazima lisimame likaguliwe lakini kila mara wanapita na ninakuhakikishia wahamiaji haramu wanapita sana katika hii njia na wanafanikiwa kufika mpaka wanapoenda,” anasema mtoa taarifa huyo.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa njia wanazotumia ni barabara ya vumbi kutoka Arusha, kupitia katika vijiji vya Njoro, Kiteto, Ngusero, Mkoka na kutokea barabara ya lami katika eneo la Narco na kuendelea na safari.

Njia nyingine ni ya lami kutokea Kondoa kupitia Kelema, Paranga, Chemba, Kambi ya Nyasa, Kidoka, Haneti, Chenene, pori la Mtungutu, Zamahero, Mayamaya, Zanka Mzakwe na huingia Dodoma Mjini na kuelekea Mbeya na Njombe.

Wakiwa mkoani uchunguzi umebaini wahamiaji hao husafirishwa kwa magari yakiwemo malori au Canter na pikipiki kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Kwa mujibu wa watoa taarifa wetu, kwenye magari hukaa kwenye maboksi au kufichwe kwenye bidhaa mbalimbali ama nyanya, mahindi ambazo hupangwa kwa kuwazunguka.

Hivi karibuni jijini Dodoma, Jeshi la Polisi lilimkamata Joachim Joseph (38) akidaiwa kuwasafirisha wahamiaji haramu 16 wa Ethiopia kutoka Moshi kupitia Dodoma kwenda Mbeya na baadaye Afrika Kusini akitua namba za Shirika la Umma (SU).

Usafiri mwingine waoutumia ni mabasi ambapo hupanda wawili au watatu wakiwa na anayewasafirisha na hufanya hivyo katika njia ambazo hakuna mwingiliano mkubwa wa magari na hakuna ukaguzi wa mara kwa mara.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Bahati Mwaifuge alisema wameweka mikakati ya kuongeza idadi ya askari katika maeneo mbalimbali katika Mkoa huo wa Dodoma.

Anaitaja mikakati mingine ni kuwa na doria za mara kwa mara, kufanya misako na kutoa elimu kwa wananchi na kuwa kwa sasa kila wilaya wana ofisi ambazo wananchi wanaweza kwenda kutoa taarifa.

Alipoulizwa licha ya mikakati hiyo mbona Chemba bado wahamiaji hao wanaendelea kukamatwa kila baada ya miezi mitatu, alisema wameweka kituo Mtungutu kukabiliana nao lakini bado kuna changamoto ya njia za panya.

“Na mtu wa Uhamiaji yupo pale. Unajua hizi njia za panya ni nyingi, ukizuia huku wanatafuta zingine. Mfano Chilonwa tulikamata wahamiaji haramu kule hakuna gari inayofika, tuliwakamata Wasomali watano wamejificha porini,” alisema.

Hata hivyo, ofisa huyo aliikumbusha jamii kuwa suala la ulinzi ni la kila mwananchi na wanatakuwa kutoa taarifa pindi wanapoona sura hazieleweki katika maeneo yao.

“Tusiwe wakarimu kupitiliza. Mhamiaji anaweza kukaa nchini akapata vitu hakutakiwa kuvipata, mfano uongozi. Akiishi nchini atapata haki za Mtanzania au ni gaidi amekuja kujificha labda ni mpelelezi haya ni lazima tuyajue,” alisema.


Mikoa mingine hali ikoje

Ukiacha mikoa wanapoingilia, mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania ndiko wanakotokea, hasa Songwe.

Chanzo kutoka Tunduma kimelieleza Mwananchi kuwa wahamiaji hufika mkoani hum o wakitokea mikoa ya Mbeya, Morogoro, Iringa, Manyara, Dodoma na Njombe kabla ya kuvuka kupitia mpaka wa Tunduma na vichochoro vingine kuingia Zambia kuelekea Afrika ya Kusini.

Kwa Mkoa wa Morogoro ambao ni njia au mapito, njia kuu na maeneo wanayokamatwa sana ni barabara za Chalinze -Msata, Turiani, Kilosa, Mikumi, wakitokea Bagamoyo Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam Manyara na Dodoma.

Vyombo vinavyotumika kuwasafirishia ni pamoja na pikipiki, magari binafsi, magari ya mizigo yakiwemo matanki ya mafuta na mabasi ya abiria.

Ofisa uhamiaji mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji, Joseph Kasike alisema wahusika wakuu wa biashara hiyo ni Watanzania wakishirikiana na baadhi ya raia wa kigeni hasa kutoka Malawi, Kenya, Zambia, Somalia, Ethiopia na Afrika ya Kusini huku vyanzo vya fedha zinazotumika kuwapokea, kuwahifadhi na kuwasafirisha hutoka kwa wafanyabiashara ambao si rahisi kuwafahamu.

“Inasemekana fedha hizo hukabidhiwa kwa mawakala wa usafirishaji na mara nyingi utumia mawasiliano yasiyo rasmi na kwa njia ya siri,” alisema Kasike.

Wakati tatizo la wahamiaji haramu likionekana kukithiri katika maeneo mengi, Jeshi la Umahiaji limesema linaweka mikakati madhubuti kulitokomeza.

Akizungumzia takwimu za miaka mitano Kasike alisema jumla ya watuhumiwa 2,608 walikamatwa na kati yao 621 walifikishwa mahakamani katika mkoa wa Morogoro pekee.

Pia alisema mikakati ya kupambana nao ni kuanza kwa kampeni ya ‘Mjue jirani yako’ inayolenga kuwapa elimu wananchi kujua madhara ya wahamiaji haramu.

Alisema wanaimarisha doria na kufanya msako wa mara kwa mara, kuongeza nguvu kazi kwa kuendelea kuajiri askari wa kutosheleza mahitaji, kufungua ofisi na vituo vya uhamiaji kuanzia ngazi za kata na wilaya.

Kasike alisema changamoto wanazokabiliana nazo kama mkoa ni uhaba wa vitendea kazi kama magari na pikipiki, upungufu wa askari na uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na biashara ya wahamiaji haramu.

Aidha, ofisa huyo alisema mpaka sasa idadi ya vyombo vya usafiri vilivyokwishataifishwa ni magari matano, Funny Cargo (1), Chaser (1), Nissan Teranno (1) na Noah (2) pamoja na pikipiki mbili aina ya SunLg.

Kasike anaungwa mkono na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Paul Mselle alisema uahamiaji haramu ni changamoto wanayoifanyia kazi.

“Watu wanaokamatwa waliowengi ni raia wa Ethiopia ambao hawana vibali vya kuwaruhusu kuingia na kwa sababu hawazingatii utaratibu wowote na pili hawazingatii hata hati ya kuwaruhusu kupita kama ya kuwa na viza,” anasema.

Alisema watu hao wanaopita kutoka pembe ya Afrika hawana uhalali na wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya Watanzania wanaingia kwa makubaliano ya kibiashara kwamba wakiwavushwa kunakiwango fulani cha fedha wanakubaliana kupewa.

“Changamoto kubwa inatupata pale unapopambana na watu wenye fedha nyingi kutaka kufanikiwa lengo lao, lakini kama idara kwa kushirikiana na mamlaka zingine tumekuwa tukifanya kazi kubwa bila kulala kuhakikisha wanawakamata licha ya kwamba wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali,” alisema.


Uhamiaji wajipanga

Mselle alisema wameboresha sheria zote za uhamiaji ya mwaka 2016 ambapo mtu yeyote atakayebainika kumsafirisha mhamiaji haramu adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 jela au faini Sh20 milioni.

“Kama kuna chombo chochote kilitumika kumsafirisha mhamiaji na ikabainika chombo hicho kita taifishwa pamoja na nyumba inayotumika kuwahifadhi,” alisema.

Alieleza mkakati mwingine wa idara hiyo ni kutoa elimu ya uhamiaji haramu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii hadi chini kupitia kwenye kata na vijiji.

“Katika mikutano yote inayofanyika tunatoa elimu ya uraia na kuna maofisa maalumu kila kata ambao shughuli yao ni kutoa elimu ya uhamiaji haramu na madhara yake,” alisema.

Alisema katika kuwafikia Watanzania wengi zaidi alisema wamekuwa wakitoa elimu kwenye maonesho mbalimbali nchini ambayo idara hiyo imekuwa ikishiriki ikiwemo maonyesho ya Sabasaba, Nanenane, Siku ya Sheria na Siku ya Uhamiaji wanayoifanya kila ifikapo Desemba 18 ya kila mwaka.

“Monyesho ya biashara yanayofanyika kila mkoa na tumekuwa tukipata fursa ya kutoa huduma zetu zote wanazotoa ikiwemo kibali cha ukaazi na udhibiti wa mipaka kupitia majukwaa hayo,” alisema.

Alisema mkakati mwingine wamekuwa wakifanya doria na misako kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama huku akieleza mafanikio makubwa yamepatikana na wanaokamatwa wanaongeza. Mfano alisema mwaka 2020 walikamata wahamiaji 18,580 na mwaka 2021 walikamatwa 24,561 na mwaka huu kati ya Januari na Julai wamekashamatwa wahamiaji 14,568.

“Pia, idara kwa kushirikiana na vyombo vingine tumekuwa tukiweka vizuizi vingine barabarani na kufanya upekuzi kubaini kama kuna wahamiaji haramu au watu waliopo nchini kinyume na sheria na hatua zote zimekuwa zikitupatia mafanikio,” alisema.


Kuhusika kwa watumishi

Mselle alisema iwapo mtumishi wa jeshi hilo atabainika anasafirisha wahamiaji haramu sheria itachukua mkondo wake.

Alisema katika mikoa ya mipakani ambayo ni kinara kwa wahamiaji haramu ikwamo Tanga na Kilimanjaro wameongeza udhibiti zaidi na hata wale wanaosafirisha kwa njia ya bodaboda wameweka vizuizi katika njia kuu.

“Ndio maana kuna maeneo mengine hawawezi kuvuka utasikia wamekamatwa. Mikoa ya Morogoro, Dodoma au Iringa na mfumo ulivyo hata ukifanikiwa kuvuka pointi moja ukifika sehemu nyingine lazima utakamatwa kabla ya kuivuka nchi,” alisema.

Aliwapongeza wananchi baada ya kuelimika kupitia elimu wanayotoa wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwa kutoa taarifa ya uwepo wa wahamiaji haramu nchini hasa kwa watu waliopo maeneo ya mipakani.

“Na wananchi ni walinzi wa kwanza katika maeneo yao na wamekuwa wakitusaidia kutupatia taarifa na ushirikiano huo tumekuwa tukiufanyia kazi na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu.


Mkakati mpya

Kwa mujibu wa Mselle, Uhamiaji pia imenzisha mkakati mpya uliopewa jina la ‘Mjue jirani yako’ na wamekuwa wakitoa elimu hiyo nchi nzima kwa kuzingatia mfumo wa zamani wa mjumbe wa nyumba 10 ambapo kila mgeni akifika lazima taarifa itolewe.

“Tumerudisha mfumo huo kwa sababu utamaduni huo umeanza kutoweka hata kwa wenye nyumba wanaopangisha wapangaji wenye nyumba wanapaswa kumjua kwa kuzingatia taarifa zake ni raia wa nchi gani,” alisema.


Zanzibar nako hali tete

Akizungumza hivi karibuni mjini Unguja, mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu (ATC), Adatus Magere alisema wameandaa mpango kazi wa kitaifa na kufanya marekebisho madogo ya sheria katika kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu.

Magere alisema pia mpango huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano hayo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali na wapo katika mchakato wa kuanzisha majukwaa ya ushirikiano na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

“Jumla ya kesi 11 za usafirishaji haramu wa binaadamu zilizohusisha wahalifu 33 zilifunguliwa kwa kipindi cha 2021/2022 na kati ya kesi hizo, sita zimetolewa hukumu,” alisema

Alisema kesi hizo zilijumuisha waathirika wakiwemo watoto wa chini ya umri wa miaka 18, hata hivyo waathirika 171 walipatiwa huduma muhimu kama makazi, chakula na matibabu.

Naibu Waziri wa Maendeleo Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Zanzibar, Anna Athanas Paul alisema jukumu la kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu si suala la mtu mmoja bali kila mmoja anapaswa kupambana nalo ili kuondosha uhalifu huo.

“Nchi yetu imekuwa ni lango kubwa la usafirishaji haramu na ndio maana Serikali inataka kufanya utafiti wa jambo hili, lengo ni kujua kwa upana wake na baada ya kufanya tafiti hizo tutajua Zanzibar usafirishaji haramu wa binadamu upo kwa kiasi gani,” alibainisha.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Abeda Rashid alisema, “kutokana na Zanzibar kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoathirika na tatizo hilo, hatuna budi suala hili kuwekwa katika mtalaa wa elimu maana wanaoumia ni watoto wadogo.”


Ushirikiano polisi, uhamiaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno alisema wamekuwa wakishirikiana na wananchi ambao wamekuwa wakitoa taarifa za watu wanaoshindwa kuzungumza Kiswahili katika maeneo yao.

“Chemba pale watu wa Uhamiaji tunakaa nao kwenye lile geti tunashirikiana kwa pamoja. Tunafanya doria maeneo mbalimbali na ‘intelegensia’ wanafuatilia ikiwemo katika maeneo ya pembezoni mwa barabara,” alisema Otieno.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kamanda wa polisi mstaafu ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi ngazi mbalimbali hadi ngazi ya wilaya wamekuwa wakinyooshewa vidole husika katika biashara hiyo.

Alisema baadhi ya askari wanaokuwa katika mageti baadhi kazi yao huwa ni kuwalinda wahamiaji haramu hao waweze kupita bila kupata shida yoyote.

Pia, uchunguzi wa Mwananchi umeonyesha biashara hiyo inafanywa na watu wenye fedha na wamekuwa wakijipatia kipato kikubwa na pia baadhi ya viongozi wenye dhamana fulani fulani wanatajwa kuwa na mkono katika biashara hiyo.


Viongozi wa vijiji, mitaa wajitetea

Mwenyekiti wa mtaa wa Mindu Manispaa ya Morogoro eneo ambalo kuliwahi kukamatwa wahamiaji haramu wakiwa wamehifadhiwa tayari kwa kusafirishwa, alisema pindi wanaopata taarifa tu wamekuwa wakitoa taarifa Uhamiaji ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa dhidi ya waliowahifadhi au wahamiaji wenyewe.

“Lakini kilichosaidia sasa hivi kuna elimu inatolewa kwetu kama viongozi na wananchi kwa ujumla hii imesaidia watu kuwa waoga,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Kambi ya Nyasa, Hassan Sogoi anasema ugumu wanaokutana nao hadi kushindwa kuthibiti upitaji wao ni kutokujua ndani ya malori kuna nini.

“Usafiri wao mkubwa ni malori na wanaweka vitu, mfano magunia ya mahindi au matenga ya nyanya na hapa ni njia kuu ya kwenda Dodoma na Arusha. Kuna wafanyabiashara wengi ni vigumu kujua, najuaje ndani kuna wahamiaji haramu,”anasema Sogoi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemba, Bashir Yusuph anasema ugumu mwingine wanaokutana nao ni wahamiaji hao kupita usiku wakati wao kama viongozi na raia wema wakiwa tayari wamelala.


Mahabusu zazidiwa

Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa kuna mlundikano wa watu kwenye mahabusu na kwamba watu hao wanaojulikana kama “wasafirishwaji” ambao hawana kosa lolote -- si wafungwa wala mahabusu.

Kwa mfano, mkuu wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba alisema katika mkoa wake, “tuna mahabusu na wafungwa zaidi ya 2,053 lakini kati ya hao, 946 ni wageni kutoka nje na kati ya hao, 853 ni hao wasafirishwaji.

“Hawa wamemaliza vifungo vyao, hawana kosa lolote, si mahabusu, si wafungwa, wanasubiri kurudi kwenye mataifa yao. Lakini kwenye mataifa hayo hakuna jitihada zozote za kuja kuwachukua.

“Kwa hiyo, kunakuwa na mlundikano mkubwa, matokeo yake hata wale wafungwa waliopo, wanaofanya shughuli za uzalishaji mali, wanazidiwa kwa ajili ya kuwalisha hawa ambao wanakaa bila kazi yoyote,” alisema.

Mgumba alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumza na viongozi wenzake kwenye mataifa wanayotoka wahamiaji hao ili waheshimu sheria za kimataifa kwa kuwasafirisha watu wao kutoka hapa nchini.

“Mheshimiwa Rais, katika hili nikuombe, najua unakaa na wenzako wa mataifa mbalimbali, basi uwahimize, ni vizuri wakatii sheria za kimataifa. Wale wafungwa wanaomaliza vifungo, ni vizuri wakaharakisha mchakato wa kuja kuwachukua na warudi katika mataifa yao kwa mujibu wa sheria,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Alisema jambo hilo linasababishwa na utofauti wa sheria kutoka nchi jirani wanazopita ambapo alisema wao wakiwakamata wasafiri hao, hawawaweki magerezani kama hapa nchini, wanawapa siku saba za kurudi kwao lakini wao hawarudi, wanaingia Tanzania.

Aliongeza kuwa wapo Watanzania hawataki kufanya biashara nyingine, wao wanakwenda kununua wahamiaji haramu, kichwa kimoja Sh150,000 wanakwenda kuwauza kwa wateja wengine kwenye mikoa mingine ili kuwasafirisha kwenda huko wanakokwenda

“Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya watumishi wa umma wanatumia rasilimali za umma na kujiingiza kwenye biashara hiyo. Kwa maelekezo yako na uimara wa vyombo vya ulinzi na usalama, tumewakamata hao na hawa watumishi tutawashughulikia,” alisema Mgumba.


Wahamiaji si wakimbizi

Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataia (UNHCR), Edward Ogolla akizungumzia tatizo hilo alisema:

“Makazi mapya ya nchi ya tatu ni mojawapo ya suluhu tatu za kudumu zinazopatikana kwa wakimbizi walioimbia nchi zao. Nyingine mbili ni urejeshaji makwao kwa hiari na ushirikiano wa ndani,” alisema Ogolla.

Alisema makazi mapya yanayopatikana kwa wakimbizi kutoka nchi ya hifadhi hadi Jimbo lingine lililokubali kuwapokea na hatimaye kuwapa makazi ya kudumu, hupatikana kwa chini ya asilimia moja ya idadi ya wakimbizi duniani kote.

“Makazi mapya ni ya kipekee kwa kuwa ndiyo suluhisho pekee la kudumu linalohusisha uhamisho wa wakimbizi kutoka nchi ya hifadhi hadi nchi ya tatu. UNHCR inawatambua na kuwarejelea wakimbizi kwa ajili ya kupata makazi mapya kwa kuzingatia hatari za ulinzi zilizoongezeka.

Aliendelea kusema kuwa nchi ya Marekani limekuwa likitoa makazi mapya kwa wakimbizi kutoka Tanzania.

“Nchi nyingine za makazi mapya ni pamoja na Australia, Ubelgiji, Canada, Norway, na Uswisi.

Alipoulizwa ushiriki wa UNHCR kuwasaidia wahamiaji wanaokamatwa nchini wakielekea Afrika Kusini, alisema kuna tofauti kati ya wahamiaji na wakimbizi.

“Wahamiaji wapo katika nchi zote duniani. Ni watu ambao wanahama kutoka nchi zao za asili bila tukio lolote, kwa kawaida kwa fursa bora za kiuchumi au nyingine mahali pengine. Kwa hivyo wanaweza kurudi salama katika nchi zao za asili.

“Wakimbizi ni watu ambao hawawezi kurudi katika nchi yao ya asili kwa sababu ya woga uliojengwa na msingi wa mateso, migogoro, vurugu, au hali nyinginezo ambazo zimevuruga sana utulivu wa umma, hivyo wanahitaji ulinzi wa kimataifa.

“UNHCR inatambua juhudi za kuwalinda wakimbizi haziwezi kutekelezwa kwa kutengwa na mwelekeo mpana, sera na desturi zinazounda uhamaji duniani.

“UNHCR inafanya kazi na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba sera na desturi za uhamiaji na hifadhi za nchi hiyo zinazingatia mahitaji ya ulinzi ya wanaotafuta hifadhi, wakimbizi na watu wasio na utaifa ambao wanaweza kukamatwa kama wahamiaji haramu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa UNHCR kwa nchi za Afrika Mashariki kushughulikia watu wanaotaka kufaidika na hadhi ya tatu, alisema wanachofanya ni kutafuta suluhu zinazowawezesha wakimbizi kuishi maisha yao kwa utu na amani.

“Suluhu kama hizo zinaweza kupatikana kwa kurejeshwa kwa hiari katika nchi ya asili, makazi mapya katika nchi ya tatu au kuunganishwa katika nchi ya hifadhi,” alisema.