Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani: Wanasheria wa Tanzania waangalie soko la dunia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa Siku ya Maendeleo ya Kitaaluma ya Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSoL).

Muktasari:

  • Asema biashara za kimataifa na teknolojia zinahitaji wataalamu wenye ujuzi unaovuka mipaka ya nchi.

Dar es Salaam. Wakati biashara za kimataifa na matumizi ya teknolojia yakibadili kwa kasi tasnia ya sheria duniani, wanafunzi wa sheria nchini wametakiwa kujijengea uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa badala ya kujikita kwenye fursa zilizopo ndani ya mipaka ya Tanzania pekee.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alipokuwa akizungumza katika Siku ya Maendeleo ya Kitaaluma ya Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSoL), akisisitiza umuhimu wa kuandaa kizazi cha wanasheria wenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira ya utandawazi.

Amesema maendeleo ya uchumi wa dunia yameifanya taaluma ya sheria kutegemea zaidi uelewa wa mikataba ya kimataifa, uwekezaji na biashara zinazohusisha nchi nyingi kwa wakati mmoja.

“Biashara nyingi zinazofanyika sasa zinahusisha zaidi ya nchi moja. Hii ina maana kuwa mwanasheria wa leo lazima awe tayari kufanya kazi katika mazingira ya kimataifa na kuelewa mifumo mbalimbali ya kisheria,” amesema Ridhiwani.

Amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kunufaika na mabadiliko hayo kutokana na eneo lake la kimkakati na nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi kadhaa za Afrika Mashariki na Kusini.

Ameeleza kuwa nchi zisizo na bandari, zikiwemo Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hutegemea miundombinu ya Tanzania katika shughuli za biashara na usafirishaji wa mizigo, jambo linalofungua fursa kwa wataalamu wa sheria kutoa huduma za kisheria kwa wateja kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema wanasheria wa Tanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kujitanua katika maeneo ya sheria za biashara za kikanda, uwekezaji, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na huduma nyingine zinazohitaji utaalamu unaovuka mipaka ya taifa.

Sambamba na hilo, Ridhiwani amesema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya utoaji haki kwa kutumia teknolojia ili kuongeza ufanisi na kurahisisha huduma za mahakama.

Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya mahakama ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuifanya sekta ya sheria kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.

“Tunajenga mfumo wa kisasa wa utoaji haki unaotumia teknolojia na unaowezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi na kwa wakati,” amesema.

Aidha, amewataka wanafunzi kutumia muda wao wa masomo kujifunza zaidi ya yale yanayofundishwa darasani kwa kufuatilia mwenendo wa sheria za kimataifa, biashara za kikanda na matumizi ya teknolojia katika taaluma yao.

“Dunia inabadilika kwa kasi. Ili kubaki kuwa muhimu na wenye ushindani, lazima mjenge uwezo wa kufikiri kimataifa na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazovuka mipaka ya nchi,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia taaluma, Profesa Rose Upor, amesema Siku ya Maendeleo ya Kitaaluma imeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha wanafunzi na mazingira halisi ya kazi wanayotarajia kuyaingia baada ya kuhitimu.

Amesema pamoja na mafunzo ya darasani kuwapa wanafunzi maarifa ya kisheria na misingi ya maadili ya taaluma, bado wanahitaji kupata uzoefu kutoka kwa wataalamu walioko katika sekta hiyo ili kuelewa changamoto na matarajio ya soko la ajira.

“Tunatambua kuwa mafanikio ya mwanafunzi hayategemei ufaulu wa darasani pekee. Ni muhimu pia kukuza umahiri wa kitaaluma, ujuzi wa mawasiliano, uongozi wa kimaadili na uzoefu wa kivitendo unaohitajika katika mazingira ya kazi ya sasa,” amesema Profesa Upor.

Amesema taaluma ya sheria ni miongoni mwa sekta zinazobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, ukuaji wa mifumo ya kidijitali na kuongezeka kwa mahusiano ya kibiashara duniani.

Kwa mujibu wake, baadhi ya huduma za kisheria na taratibu za mahakama sasa zinafanyika kwa njia ya mtandao, hali inayowalazimu wanafunzi kujifunza ujuzi mpya unaoendana na mahitaji ya zama za kidijitali.

Profesa Upor amesema dunia ya sasa inahitaji wahitimu wenye uwezo wa kutumia teknolojia, kufikiri kwa ubunifu na kufanya kazi katika mazingira yenye ushindani mkubwa.

Aidha, amesema chuo kitaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu, serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha wahitimu wanapata maandalizi yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema lengo la chuo siyo kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kitaaluma pekee, bali pia viongozi na wataalamu wanaowajibika kwa jamii na wanaozingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.