Ridhiwani ayapa neno mabaraza ya ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akifurahia jambo na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibindu, Khamis Kaungu (kulia) wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kwaikonje
Muktasari:
Naibu Wazirii wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amesema malalamiko mengi ya wananchi ya migogoro ya ardhi yanatokana na baadhi ya mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata kutotenda haki.
Chalinze. Naibu Wazirii wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amesema malalamiko mengi ya wananchi ya migogoro ya ardhi yanatokana na baadhi ya mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata kutotenda haki.
Pia, amesema kuwa kazi ya mabaraza hayo ni kusuluhisha migogoro ya ardhi na sio kutoa hukumu.
Ridhiwani amebainisha hayo kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Vigwaza wilayani Chalinze katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kutolea majibu.
Amesema kuwa katika ofisi yake amekutana na malalamiko mengi ya migogoro ya ardhi huku wananchi wakawalalamikia viongozi wa mabaraza hayo kutotenda haki.
"Nataka niwaambie ndani ya ofisi yangu nimekutana na malalamiko mingi ya ardhi na nimegundua mabaraza yetu mengi ya ardhi yamekua kumbe hayatendi haki katika maeneo kadhaa na watu wanayalalamikia hayatendi haki na bahati mbaya wasimamizi wa sheria hatutoi tafsiri ya kisheria nini mabaraza hayo yanatakiwa kufanya" amesema Ridhiwan
Ridhiwani ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze amewataka wenyeviti wa mabaraza hayo kusimamia dhana ya kuanzishwa kwa mabaraza hayo na wasimamie vikao vya usuluhishi na sio kuwa watoa maamuzi ya malalamiko yanayowasilishwa ili kupunguza migogoro kwenye maeneo yao.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri huyo pia alizungumzia kuhusu kulipwa fidia kwa wananchi wanaotoa maeneo yao kupisha miradi mbalimbali ya maendeleo, akiwatoa hofu wale ambao watatakiwa kutoa maeneo yao kupisha miradi mbalimbali watalipwa kwa mujibu wa sheria.
Ridhiwani ametoa rai kwa wananchi kutokuwa vikwazo pale ambapo Serikali inataka kufanya miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
"Naomba watu wote kwanza muelewe kuwa Serikali haina lengo la kuumiza mtu na pia naomba watu kwanza muelelwe ardhi yote tuliyonayo ni mali ya umma na amekabidhiwa Rais hivyo Seriakali inapotaka kufanya maendeleo inafanya kwa niaba yetu tusiwe vikwazo" amesema Ridhiwan
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Vigwaza wameiomba Serikali kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi ili kusaidia kumaliza migororo ya ardhi.