Rea yakamilisha miradi minne ya umeme kwa vijiji 5,259

Mkurugenzi mkuu wa wakala wa nishati vijijini REA Mhandisi Hassan Said akizungumza na wajumbe wa kikao cha baraza la wafanyakazi REA ukilichofanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Kupelekwa kwa miradi hiyo kwenye vijiji na vitongoji hivyo kunatokana na kupokea ombi maalumu kutoka kwa viongozi wa Serikali Kuu lililotaka vijiji na vitongoji hivyo vifikiwe na umeme.
Morogoro. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Mhandisi Hassan Said ametangaza kukamilika kwa miradi minne mikubwa ya umeme inayolenga kuleta nishati katika vijiji 5,259, ikijumuisha vijiji 4,071 na vitongoji 188, katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili.
Miradi hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha vijiji na vitongoji vingi vinapata huduma ya umeme kama sehemu ya majukumu yake ya kuunga mkono maendeleo ya maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Rea, Mhandisi Said alieleza kuwa miradi hii ni matokeo ya ombi la viongozi wa serikali kuu linalohimiza kufikishwa kwa huduma ya umeme katika maeneo hayo, ili kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.
"Miradi hii ni hatua kubwa katika kufikia lengo letu la kuhakikisha nishati inafika vijijini na maeneo yaliyokuwa hayafikiki. Tunajivunia mafanikio haya, na tutaendelea kufanya juhudi kuongeza maeneo yanayohudumiwa," alisema Mhandisi Said.
Mbali na miradi hiyo, Rea pia imeanzisha mradi mwingine wa kupeleka umeme katika vitongoji vipatavyo 9,000.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza wigo wa umeme na kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati kwa wananchi wa maeneo hayo.

Wajumbe wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa wakala wa nishati vijijini REA wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kikao hicho. Picha Hamida Shariff
Katika hatua nyingine, Rea imeanzisha mradi wa ugawaji wa majiko banifu kama njia mojawapo ya kupunguza upotevu wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo umefanikiwa kufikia takribani wananchi 5,000, huku wengine 300,000 wakitarajiwa kufikiwa hivi karibuni baada ya mikataba ya usambazaji majiko hayo kusainiwa.
"Madhumuni ya mradi huu ni kuwaleta wananchi wa vijijini karibu na nishati safi ya kupikia, huku tukiwa tunapunguza matumizi ya kuni na mkaa, ambayo ni hatari kwa afya na mazingira. Majiko haya banifu yamebuniwa kwa ustadi na yana uwezo wa kutumia kiwango kidogo cha kuni na mkaa, tofauti na majiko ya zamani," alisema Mhandisi Said.
Akizungumzia changamoto za matumizi ya gesi, Mhandisi Said ameeleza kuwa, kwa wananchi wengi wa vijijini, gharama za kununua gesi ni kikwazo.
"Tunajua ugumu wa wananchi wetu kulipia huduma za gesi, na ndiyo maana majiko haya banifu yatakuwa suluhisho bora zaidi," aliongeza.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Mkoa wa Dodoma, Samweli Nyungwa, aliwashauri wafanyakazi wa Rea kutoa maoni na mawazo yatakayosaidia kufanikisha mipango ya maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unafanikiwa.
Alisisitiza umuhimu wa ufanisi katika kazi ili wafanyakazi wa Rea waweze kudai stahiki zao kwa ufanisi.
Baraza la Wafanyakazi la Rea lina jumla ya wajumbe 69 na limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyakazi na viongozi wa wakala huo.