Rais wa Indonesia kufanya ziara ya siku mbili Tanzania

Rais wa Indonesia, Joko Widodo
Muktasari:
- Rais wa Indonesia, Joko Widodo atafanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania na ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili ukitarajiwa kuongezeka zaidi na kuchochea fursa za biashara na uwekezaji.
Dar es Salaam. Rais wa Indonesia, Joko Widodo anatarajiwa kuwasili nchini leo Agosti 21, 2023 kwa ziara ya siku mbili yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
Rais Widodo atapokelewa kesho Agosti 22, 2023 na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo watakuwa na mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo ya pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Indonesia.
Akizungumzia ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema mazungumzo ya viongozi hao yatajikita katika maeneo ya afya, nishati, madini, uchumi wa buluu, biashara na uhamiaji.
"Tunatarajia kwamba hati za makubaliano pia zitasainiwa kesho, sitazitaja kwa sasa lakini zitakuwa kwenye maeneo hayo niliyoyaeleza," amesema Waziri Tax.
Amebainisha kwamba baada ya mazungumzo yao, Rais Samia atamwandalia mgeni wake chakula cha mchana, kisha Rais Widodo atatembelea Ubalozi wa Indonesia hapa nchini na baada ya hapo ataondoka nchini.
Waziri Tax amebainisha kwamba uhusiano wa Tanzania na Indonesia ulianza mwaka 1955 wakati wa mkutano wa Bandung uliozikutanisha nchi za Asia na Afrika kupigania ukombozi.
"Kupitia mkutano huo, nchi hizi zilikubaliana kushirikiana ili kujikomboa katika utawala wa kikoloni na huo ndio ukawa msingi wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (Nam)," amesema Waziri.
Ameongeza kwamba uhusiano wa kidiplomasia ulianza mwaka 1964 baada ya Indonesia kufungua ubalozi wake hapa Tanzania na Agosti 2022, Tanzania nayo ilifungua ubalozi wake nchini Indonesia.
Amesema wamekuwa wakishirikiana katika kilimo ambapo mwaka 1996, Indonesia ilianzisha Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima Vijijini kilichopo Mkindo mkoani Morogoro.
Mwaka huu, amesema wanaendelea kushirikiana katika miradi mitano kwenye sekta za kilimo, uzalishaji viwandani na ujenzi na kupitia ziara ya Rais Widodo wataimarisha uhusiano huo.
"Kupitia mazungumzo ya viongozi wetu, tunatarajia kwamba tutaimaisha zaidi ushirikiano ambao umekuwepo kwa muda mrefu kwenye sekta mbalimbali," amesema Dk Tax.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Macocha Tembele amesema Indonesia kuna fursa kubwa kwenye bidhaa za kilimo kama vile korosho, pamba, tumbaku, soya pamoja na madini.
"Fursa zipo nyingi kule hasa kwenye bidhaa za kilimo na madini, lengo la ushirikiano huu ni kufungua fursa zaidi kwa watu wetu kuweza kufanya biashara na wenzao wa Indonesia," amesema Balozi Tembele.
Uhusiano wa Tanzania na Indonesia uliasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Indonesia, Surkano.
Ziara ya Rais Widodo ni ya pili kwa kiongozi wa kitaifa wa Indonesia kutembelea Tanzania, ziara ya kwanza ilifanyika Desemba 1991 ambapo Rais wa pili wa taifa hilo, Suharto alitembelea Tanzania, ikiwa imepita miaka 32.