Rais Samia kushiriki uzinduzi kampeni za Odinga uenyekiti AU

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki uzinduzi wa kampeni za Raila Odinga kugombea uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) huko Nairobi, Kenya.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa wakuu wa nchi watakaoshiriki uzinduzi wa kampeni za uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), unaowaniwa na Raila Odinga.
Ushiriki wa Rais Samia katika kampeni hiyo ni baada ya kualikwa na Rais wa Kenya, William Ruto kwenda katika taifa hilo kwa ziara ya kikazi.
Taarifa ya ziara ya mkuu huyo wa nchi kwenda Kenya, imetolewa leo Jumanne, Agosti 27, 2024 na kusaniwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia amesafiri leo kwenda nchini Kenya kwa ziara hiyo ya kikazi ambayo pia itahusisha kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo.
"Hafla hiyo itafanyika ikulu ya Nairobi na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi mbalimbali," imeeleza taarifa hiyo.
Nafasi anayowania Odinga aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, ni kama inamwondoa kabisa katika ulingo wa siasa za ndani ya taifa hilo.
Odinga amekuwa akishiriki kuwania nafasi ya urais wa nchi hiyo mara kadhaa bila mafanikio.
Endelea kufuatilia Mwananchi.