Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Bila sheria za wazi, haki haiwezi kupatikana

Muktasari:

  • Rais Samia amesema bila sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa haki za raia unatoweka au unakuwa hauna uhakika na kusababisha uvunjifu wa amani.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema upatikanaji wa haki unatokana na sheria zilizo wazi, zinazofahamika na zinazoendana na wakati tuliopo.

Amesema sheria ni kioo cha ustaarabu wa Taifa bila ya sheria zilizowekwa wazi, zinazofahamika na zinazoendana na wakati tulionao basi haki haiwezi kupatikana.

Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa Serikali ni sheria, Rais Samia amesema hakuna kitu kinaitwa Serikali bila sheria na sheria zikishaundwa ni lazima zifuatwe na zitekelezwe.

Akizungumza leo Jumatano, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa toleo hilo jipya la juzuu za sheria zitakazoanza kutumika Julai mosi, 2025, Rais Samia amesema marekebisho hayo yanalenga kuendeleza misingi ya utawala bora na utawala wa sheria nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kurahisisha utoaji wa haki.

Amesema tukio hilo ni matokeo ya kazi kubwa na ya kitaalamu iliyofanywa kwa juhudi, weledi na mshikamano wa taasisi za kisheria zikiongozwa na ofisi ya mwandishi mkuu wa sheria chini ya ofisi ya  mwanasheria mkuu wa Serikali.

“Si hivyo tu, bila ya sheria kuwa wazi hata uhakika wa ulinzi wa haki za raia unatoweka au unakuwa hauna uhakika na kusababisha uvunjifu wa amani, aidha shughuli za uchumi kufanyika kwa mashaka pasipokuwa na sheria za kueleweka,” amesema.

“Hata mwekezaji akija cha kwanza anauliza sheria zetu zinasemaje sasa kama zipo vipande vipande wanakuwa na mashaka wanakosa imani.

“Nyote mnafahamu sheria ni kioo cha ustaarabu wa Taifa, bila sheria zinazofahamika, zilizowekwa wazi na zinazoendana na wakati haki haiwezi kupatikana,” amesema.

Rais Samia amesema bila sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa haki za raia unatoweka au unakuwa hauna uhakika na kusababisha uvunjifu wa amani, pia shughuli za kiuchumi hufanyika kwa shaka pasipokuwa na sheria zinazoeleweka.

“Mwekezaji akija anataka kujua sheria zetu zinasemaje, sasa kama ziko vipande vipande anapata shaka na anaweza kukosa imani. Kukamilika kwa toleo hili ni hatua muhimu katika ustawi wa maendeleo ya Taifa,” amesema.

Hii ni mara ya pili katika historia ya Tanzania kufanya urekebu wa sheria, shughuli kama hiyo ilifanyika mwaka 2002 na ilihusisha marekebisho ya sheria 415 na toleo hilo jipya linahusisha marekebisho ya sheria 446.

“Serikali ilikuwa ikitoa fedha kwa ajili ya urekebu wa sheria sikuwa nafahamu ni kiasi gani ila leo ndiyo nimejua Sh10 bilioni zimetumika kwenye urekebu wa sheria. Tunajivunia zaidi kwa sababu kazi hii imefanywa na wataalamu wa ndani na sheria hizi zimechapwa na mchapishaji wa hapa nchini Mkuki na Nyota, safari hii kila kitu kimefanyika hapa nchini na hii ni fahari kwetu,” amesema.

Amesema uandishi wa juzuu za sheria ni jambo muhimu litakalorahisisha kazi sio tu kwa  wanasheria, mawakili, mahakimu na majaji bali hata wanaotumia sheria katika utekelezaji wa kazi zao.

“Toleo hili linakwenda kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi na sheria zote kuu 446 zimehusishwa kwenye mabadiliko haya. Sasa hakuna haja kwa wanasheria kuambizana kurejea vifungu vya sheria zilizofanyiwa mabadiliko, sasa sheria zote zimeandikwa upya zipo pamoja katika mpangilio mzuri,” amesema.

Rais wa Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023, leo Jumatano Aprili, 23, 2025, Ikulu Chamwino, Dodoma.

Kwa upande wa Mahakama amesema matarajio ni kuwa toleo hilo jipya la sheria litapunguza muda unaotumika kwenye kufanya utafiti ili kupata uhakika wa sheria inavyosema, hivyo kurahisisha utoaji wa uamuzi.

“Pia, juzuu hizi za sheria zilizorekebishwa ni muhimu katika kuongeza uwazi na kuzidi kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao. “Aidha, ni nyenzo muhimu itakayosaidia kupunguza matumizi mabaya ya madaraka na kuziba ombwe la kisheria lililokuwa likitumika kuchochea rushwa,”amesema Rais Samia.

“Vilevile kuwekwa vyema kwa sheria hizi kutajenga mazingira mazuri ya kukuza imani kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika kuimarisha shughuli za kiuchumi nchini.

“ Sheria hizi zikipatikana kwa urahisi na zikifahamika vyema kwa wananchi zitapunguza uwezekano kutokea makosa kwa kisingizio cha kutojua sheria.”


Sheria zitaendelea kurekebishwa

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye marekebisho ya sheria kuendana na mahitaji yanavyojitokeza.

Amemuelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari kuwa urekebu wa sheria unapaswa kufanyika ndani ya miaka 10 na kadiri mabadiliko ya sheria yanavyofanyika ni muhimu kuandikwa upya na kuwekwa kwenye marekebisho ya kila mwaka.

“Niliangalia takwimu za mwenendo wa kasi wa kutunga na kurekebisha sheria nchini, nimeona katika zoezi la urekebu wa sheria mwaka 2002 idadi ya sheria zilizofanyiwa urekebu zilikuwa 415, mwaka 2023 zimeongezeka kidogo na kufikia 446.

“Hata hivyo, ili kupata picha kamili inabidi kuangalia takwimu za sheria mpya zilizotungwa, zilizofutwa na zilizotungwa upya kuanzia mwaka 2002 hadi 2023. Takwimu hizo zinaonesha sheria 171 zilifanyiwa mabadiliko makubwa kati ya sheria 446,” amesema Rais Samia.

“Pia, takwimu za mabadiliko ya sheria kati ya mwaka 2002 hadi 2023 tunaona jumla ya marekebisho 1039 yalifanyika kwenye sheria mbalimbali, hii ni kuonesha kwamba jinsi nchi yetu inavyofunguka na kuleta maendeleo kunahitajika pia mabadiliko ya sheria zetu ili kulinda utawala bora na haki na masilahi ya jamii na Taifa kwa jumla,” amesema Rais Samia.


Alichokisema AG

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa toleo hilo, Johari amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa urekebu walibaini baadhi ya maboresho yanahitaji kufanyika kwa njia ya marekebisho ya sheria ya Bunge.

“Wizara ya Katiba na Sheria iliandaa muswada kwa ajili ya kutungwa kwa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali yalitokana na zoezi la urekebu. Niishukuru sana wizara kwa kufanikisha hili maana ndilo lilituwezesha kuendelea na utekelezaji wa mradi,”amesema.

Johari amesema mradi wa urekebu wa sheria umelenga kufanya majumuisho ya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazofanywa na Bunge la Tanzania kuwa kitu kimoja ili kurahisisha upatikanaji na usomwaji wa sheria hizo na utumiaji wake.

“Hii ni kazi ya msingi inayolenga kuuhisha, kuboresha na kurahisisha matumizi ya sheria za nchi yetu, kwa  kufanya hivi tunahakikisha sheria zetu zinabaki kuwa hai, zinaendeana na wakati na zinaeleweka kwa urahisi kwa wananchi wote, zoezi hili linahusisha sheria zote kwa kujumuisha marekebisho yaliyofanyika tangu toleo la mwisho mwaka 2002,” amesema Johari.