Rais Samia asimulia ajira yake ya kwanza serikalini

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea tuzo ya pongezi na shukrani kutoka TAPSEA na TRAMPA iliyokabidhiwa kwake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Hemed Suleiman Abdulla wakati wa mkutano wao wa Kitaaluma.

Zanzibar. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Mei 27, 2023 amesimulia safari yake ya kuwa Rais ilivyoanzia katika nafasi ya mtunza kumbukumbu ambayo ilikuwa ajira yake ya kwanza serikalini.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) na Chama cha Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) kilichofanyika visiwani Zanzibar.

"Mimi nilianza kazi kama muweka kumbukumbu. Ni taasisi ninayoijua vizuri na ndiyo maana nawathamini lakini nikiwa muweka kumbukumbu nilifanyakazi kwa karibu zaidi na makatibu mahsusi,"amesema Samia.

Aidha, Rais Samia amesema mkutano huo ni wa kipekee kwani kwa mara ya kwanza umewaweka pamoja makatibu mahsusi na watunza kumbukumbu na nyaraka kwa mafunzo maalum.

Akizungumzia kauli mbiu ya mkutano huo inayosema 'Nidhamu, uadilifu na utunzaji siri sehemu za kazi ni chachu ya maendeleo kitaaluma' amesema hivyo vyote vinazaa ufanisi katika kuleta maendeleo.

Mwaka 2022 Rais Samia alitoa maagizo kuwe na mkutanao wa pamoja wa kada hizo na ufanyike Zanzibar kwa kuwakutanisha pamoja Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka.

Samia amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuzungumza na waajiri kutoa ruhusa ya wafanyakazi kwenda katika mafunzo ili kujifunza vitu vipya na kutanua wigo wa taaluma zao.

"Hii ndiyo fursa pekee kwa kada hizi kutoka nje ya ofisi zao wakitoka ni wakati wa likizo lakini likizo wanaenda kijijini kwa wazee na kule hawapati kupumziko kwa sababu ya matatzo tele,"amesema.