Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia ang’aka, azijibu balozi za Umoja wa Ulaya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillius Wambura kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Moshi mkoani Kilimanjaro, leo 

Muktasari:

  • Rais Samia amezishukia balozi za mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU) yaliyotaka uchunguzi wa mauaji ya raia nchini, akisema atawachongea kwa wakuu wao wa nchi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amejibu matamko ya balozi zinazowakilisha mataifa mbalimbali nchini, yaliyotaka uchunguzi wa haraka wa matukio ya utekaji na mauaji ya watu, akisema Tanzania ni nchi huru haipaswi kuelekezwa cha kufanya kwenye mambo yake.

Katika majibu yake hayo, amewashutumu mabalozi hao akisema walichokitamka haamini kama ni maelekezo ya wakuu wa nchi zao, huku akiahidi kuwachongea kwa marais wa mataifa husika kwa kuiingilia Tanzania.

Chimbuko la majibu ya mkuu huyo wa nchi ni tamko la pamoja la balozi za mataifa 15 yanayowakilisha Umoja wa Ulaya (EU) nchini, yakilaani na kutaka uchunguzi wa haraka na huru wa matukio ya mauaji.

Balozi zilizotoa tamko hilo la pamoja ni Ubelgiji, Uingereza, Canada, Denmark, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Hispania, Sweeden na Uswisi.

Pia, Marekani ilitoa tamko la peke yake juu ya matukio hayo.

Katika tamko hilo, balozi hizo zilisema: “Tunakaribisha wito wa Rais wa kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kubaini wahalifu waliohusika na kuhakikisha kuna uwajibikaji.”

Kadhalika wametaka ulinzi wa upinzani, ili kuakisi falsafa ya 4R ya Rais Samia na kusisitiza:“Tunatambua kwa wasiwasi mkubwa kwamba matukio haya ya hivi karibuni yanatishia misingi ya kidemokrasia na haki za wananchi wa Tanzania.”

Hata hivyo, mabalozi hao walitoa tamko hilo, muda mchache baada ya taarifa ya kifo cha kada wa Chadema, Ali Kibao aliyechukuliwa akiwa katika usafiri wa umma Septemba 6, mwaka huu na siku moja baadaye amekutwa ameuawa.

Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 17, 202, Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Maofisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi na miaka 60 ya Jeshi la Polisi.

“Hatupo hapa kuelekezwa nini cha kufanya ndani ya nchi yetu, tuna Katiba sheria, miongozo, mila na desturi zetu zinazotuongoza nini cha kufanya kwenye nchi zetu,” amesema.

Rais Samia amesema ameapa kuilinda na kuitetea nchi na kwamba atafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa Watanzania kwa kuwa ni jukumu lake.

Katika wajibu huo, amesema hahitaji kuelekezwa na mtu yeyote cha kufanya kwa sababu Katiba ya Tanzania ina maelekezo ya jinsi ya kuendesha Serikali.

“Wengine wanapotaka kuonyesha huruma yao basi tunawasihi wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya mahusiano kidiplomasia ya kimataifa kama ilivyoelezwa kwenye Vienna Convention on Diplomatic Relation la 1961.

“Lile tamko lililotoka na kuambiwa tufanye moja mbili tatu, sisi tunajua cha kufanya kama Tanzania kama nchi yetu. Na ni imani yangu kwamba tamko lile lililotolewa si maelekezo ya wakuu wa nchi huko walikotoka,” amesema.

Kwa sababu ana namna ya kujua, mkuu huyo wa nchi amesema atawasiliana na wakuu wenzake wa nchi za balozi hizo kujua iwapo tamko hilo ni maelekezo yao na kama sivyo atawasilisha malalamiko yake.

Katika maelekezo yake hayo, amesema mauaji yanatokea katika kila nchi, lakini Tanzania haikuwahi kuwatuma mabalozi wake wakaelekeze nchi hizo cha kufanya.

“Kule kwa wenzetu kulikoendelea kuna mwanasiasa amekosea kuuawa mara mbili, lakini tulichokisikia ni Serikali kutaka kufanywa uchunguzi na wameanza kufanya uchunguzi huo, kwa hiyo si ajabu na kwetu mara baada ya tukio kutaka uchunguzi ufanyike na kazi nimeambiwa inaendelea vizuri sana,” amesema.

Atoa onyo

Katika hotuba yake hiyo, amesema ingawa Serikali yake inaongozwa kwa falsafa ya 4R, haimaanishi kuruhusu uvunjwaji wa sheria, mila, desturi na kuruhusu utovu wa nidhamu.

“Hatutavumilia vitendo vyovyote vya kuleta machafuko na mifarakano nchini. Sasa ni vizuri tusisahau au wale wanaojiandaa na machafuko wasisahau mapito waliyopita. Ni falsafa hii hii ndiyo imewapa ruhusa ya kurudi nchini, tukafumbia macho mengine yote, sasa kama wameshaota mikia sasa sheria zile zile bado zipo,” amesema.

Ameeleza Serikali imefanya juhudi za kurudisha uhuru wa vyama vya siasa, vyombo vya habari, waliokuwa jela walitolewa na waliokuwa na jinai zilifumbiwa macho kwa lengo la kuwa pamoja kujenga nchi.

Ameeleza inakuwa mbaya watu hao hao wanasimama kutoa kauli zinazoirudisha nyuma nchi, akisisitiza atailinda amani ya nchi kwa gharama yoyote.

“Ukimya wangu sio ujinga na wala kuzungumza sana sio werevu hata kidogo, kuzungumza sana ni udebetupu tu haliachi kuvuma lazima litavuma.

“Na anayenyamaza kimya si mjinga ni mtu anayetafakari mambo si mjinga. Kwa hiyo ukimya wangu sio ujinga na kuropoka kwao sio werevu,” ameeleza.

Kwa kuwa aliapa kuilinda na kutetea Katiba, alisema hatakuwa na muhali kwa atakayetaka kuivuruga amani.

“Tumevumiliana sana kwa mambo mengi, lakini kwenye kulinda tunu ya amani na utulivu nieleze, sitakuwa na muhari kwa yeyote atakayejikaribisha katika mambo haya, anayeratibu, anayeshiriki na hata anayetekeleza mipango hiyo miovu,” amesema.

Mauaji ya Kibao

Mkuu huyo wa nchi, pamoja na kueleza kuhuzunishwa na kulaani tukio la kifo cha Kibao, lakini ameshangazwa namna wananchi walivyoonyesha hisia kali ilhali kwenye mauaji ambayo aghalabu hutokea yakiwemo ya albino hawaonyeshi hali hiyo.

“Katika hali ya kushangaza kifo hicho kimeleta hisia kali pia kwa wawakilishi wa baadhi ya mataifa ya nje wanaoiwakilisha nchi zao hapa kwetu. Nataka niungane nao na niseme kwamba kwa sababu yoyote ile mauaji haya hayakubaliki,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, alisema ndiyo maana Serikali ililaani na kutaka vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kama inavyofanyika katika mataifa yote duniani.

“Lakini kuna vifo vinasemwa muda baada ya muda, watoto maalbino wanakatwa mikono, watoto wadogo wanauliwa wanakatwa sehemu nyeti wanatupwa sijui huyu kamuua huyu.

“Hadi leo asubuhi IGP (Camilius Wambura) kanipa ripoti huko Dodoma watu watatu wameuliwa lakini yanapotokea haya yanatokea kwenye maeneo yetu lakini kimya mpaka polisi iibuke iseme wengine hawasemi.

“Lakini inashangaza kifo cha ndugu yetu Kibao kimeibua wimbi kubwa kulaani, kusikitika, kulaumu, kuita Serikali ya wauaji hii si sawa, kifo ni kifo. Tunachopaswa kufanya Watanzajia wote tukemmeane tusimame imara kukemea mambo haya,” amesema.

Wavunjifu wa amani

Katika hotuba yake hiyo, alisema alisikiliza sauti za wanasiasa mbalimbali wote wakitoa taswira ya mipango ya uvunjifu wa amani inayopangwa na baadhi ya vyama vya siasa.

“Nayaunganisha haya na kikao cha Septemba 11, mwaka huu kilichofanywa na chama kimoja cha siasa kule Nguleli mkoani Arusha.

Kikao ambacho kimeazimia kuwatumia na kuwachochea vijana kwa kuzusha tuhuma dhidi ya jeshi la polisi, kufanya siasa chonganishi kwenye misiba na kushusha molari kwa jeshi la polisi ili washindwe kufanya kazi yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao,” amesema.

Ameeleza kwa sababu ya ukubwa wa intelejensia ya nchi, ndiyo maana imewezekana kupata taarifa za kikao hicho, akisisitiza naye anayo.

“Kwa hiyo nataka niwaambie vikao vyote vinavyokwenda kupanga uovu huu, uovu tutaupata. Kumepangwa sijui kushusha moto mpaka Samia aseme sijui basi nime-surrender naondoka, hiyo Serikali Serikali ya samaki?” amehoji.

Matukio mengine aliyoyazungumzia, ni mauaji yanayohusisha upigaji ramli na vuguvugu la uchaguzi, akisema yanapaswa yakome.

“Wananchi wanakata tamaa kuona matukio haya yanahusishwa sio tu na waganga wa kienyeji bali hata watu mashuhuri kama viongozi wa dini na hata wazazi na watoto.

“Lakini yanapotokea kule chini jamii ipo kimya kama Tanzania haitokei kitu, lakini vyombo vya ulinzi wakiibua ndiyo sasa watu wanaibuka eeeyeye yeye… lakini kabla ya kuibuka hakuna anayelaani,” amesema.


Mafunzo kwa askari                                                                              

Amesema askari wanatakiwa kupatiwa mafunzo kazini, ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza nchi nyingine ziongezwe ili wakajifunze wenzao wanavyofanya.

Sambamba na hayo ametaka mafunzo ya ndani pia yaendelee, akisisitiza mabadiliko ya fikra yanategemea mafunzo ya mara kwa mara.

Hata hivyo, alieleza bado kuna changamoto katika utendaji wa jeshi hilo na kwamba Tume ya Haki Jinai imeshapendekeza namna ya kufanyia kazi.

Mambo mengine aliyozungumzia ni ajali za barabarani akisema zinasababisha vifo vya wananchi wengi na kwamba zinapaswa kudhibitiwa.

Kadhalika, amelitaka jeshi hilo kuendana na teknolojia za sasa ili kudhibiti uhalifu wa mtandaoni hasa kuelekea chaguzi na wizi kwa njia ya mtandao.

“Miongoni mwa uhalifu unaongezeka kwa kasi ni kutoa taarifa za uzushi na uongo na kutuma picha za utupu na unyanyasaji. Kutokana na kukua kwa teknolojia ya akili bandia taarifa za uzushi zinatarajiwa kuongezeka,” amesema.

“Hatusemi tufungie mitandao ya kijamii au tuwafunge midomo wananchi kutoa maoni yao, lakini hatuwezi kufumbia macho uhalifu unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii. Uhalifu ni uhalifu.

“Kama ambavyo mhalifu angekamatwa kufanya uhalifu nje ya mitandao ya kijamii, vivyo hivyo afanywe yule atakayefanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii,” amesema.

Kadhalika, mkuu huyo wa nchi alisisitiza kuongezwa uwezo na ujuzi wa kuwabaini wahalifu wanaotumia majina bandia au anga la nje ya Tanzania.


Utapeli mitandaoni

Kuhusu utapeli, ametaka liangaziwe kwa karibu zaidi kwani kwa kadri wananchi wanavyohamasika kufanya miamala kwa njia ya mtandao na ndivyo wahalifu nao wanavyobuni mbinu za kuiba.

Kwa kuwa mwelekeo wa Serikali ni kuongeza matumizi ya fedha kidigitali, alisema ni vema jeshi hilo kuhakikisha linaimarisha mbinu za kudhibiti uhalifui huo.

Mkuu huyo wa nchi, alisema matukio ya uhalifu wa mtandaoni yameongezeka kwa asilimia 36.1 kutoka 1,006 mwaka 2022 hadi 1,369 Desemba mwaka jana.

“Miongoni mwa uhalifu unaongezeka kwa kasi ni kutoa taarifa za uzushi na uongo na kutuma picha za utupu na unyanyasaji. Kutokana na kukua kwa teknolojia ya akili bandia taarifa za uzushi zinatarajiwa kuongezeka,” amesema.

Amelitaka jeshi hilo, liwasilishe mkakati na bajeti ya kukabili uhalifu wa mtandao ili Serikali ione namna itakavyowezesha kukomesha hilo.

Amesisitiza suala la utapeli kwa njia ya mtandao liangaziwe kwa karibu kwa kuwa kwa kadri wananchi wanavyohamasika kufanya miamala kwa njia ya mtandao na ndivyo wahalifu nao wanavyobuni mbinu za kuiba.

Ameeleza takwimu za hivi karibuni zinaeleza Sh5 bilioni zimetapeliwa kwa watanzania kwa njia ya mtandao na kati ya hizo Sh288 milioni zimeokolewa na jeshi la polisi.

Maelekezo ya uchaguzi

Kuelekea uchaguzi, amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha nchi inabaki kuwa moja na salama kwa kuwa uchaguzi utapita na taifa litabaki.

“Jeshi la polisi liwe macho katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Jeshi la Polisi lihakikishe yeyote anayejaribu kuhatarisha amani ya nchi yetu kwa kisingizio cha chaguzi hizo anachukuliwa hatua haraka na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Rais Samia amesema jeshi la polisi halipaswi kuhusishwa au kuhisiwa kuhusika na ukiukwaji wa sheria na haki inazozisimamia.

“Nilikuwa naona leo kuna clip kule Mwanza, kuna mhalifu kakamatwa polisi wanataka kuondoka naye, raia wamezuia gari wanasema haliondoki mpaka OCS aje ndiyo aondoke na huyu mtuhumiwa sasa hiyo ifanyieni kazi vizuri,” amesema.

Amelitaka lisimamie maadili ya askari ili jeshi litoe huduma stahiki na kuongeza imani ya wananchi kwa chombo hicho.

Ametaka kasi ya kuikumbatia Tehama katika jeshi hilo iwe kubwa na anasubiri bajeti ilia one namna atakavyosaidia.

Amesisitiza askari kujengewa uwezo stahiki ili wasipitwe na teknolojia, huku akidokeza juu ya umuhimu wa mifumo kusomana.

Ajali za barabarani

Jambo jingine alilolizungumzia Rais Samia ni ajali za barabarani amesema: “Zinapaswa kutazamwa kwa ukaribu sana tena kwa dharura. Inasemwa vyanzo vikubwa vya ajali za barabarani ni makosa ya kibinadamu asilimia 93.9, ubovu wa vyombo vya usafiri asilimia 4.1 na sababu za kimazingira ukiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara ni asilimia mbili.”

Hata hivyo, amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23 kuna ongezeko la vifo 100 kutokana ajali za barabarani, akisema mwaka 2022 zilikuwa ajali 1,720 na vifo 1545, huku mwaka 2023 ajali 1,733 na kugharimu maisha ya watu 1,645.

Alichokisema Masauni

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amemshukuru Rais Samia kwa kuliwezesha jeshi hilo.

Kutokana na kuliwezesha jeshi hilo, Waziri Masauni amesema askari wa jeshi hilo wamekuwa na molali ya kulinda usalama wa nchi.

“Nakumbuka mwaka jana kwenye sherehe zilizofanyika Dar es Salaam ulikuja na leo pia umekuja labda niseme yale yote uliyoyaelekeza katika mkutano wa mwaka uliopita kwa kiwango kikubwa sana yametekelezwa. Hili linadhihirisha Wizara na vyombo vyake hususani jeshi linakwenda vizuri sana,” amesema.