Rais Samia afanya uteuzi abadilisha msemaji wa Serikali

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea taarifa ya kamati ya kuunda mkakati wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma Juni 15, 2024. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Mobhare Matinyi aliyekuwa msemaji wa Serikali amepangiwa majukumu mengine

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, akimteua Thobias Makoba kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kabla ya uteuzi, Makoba alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Makoba anachukua nafasi ya Mobhare Matinyi ambaye amepangiwa majukumu mengine.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni 15, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, Rais amemteua Balozi John Simbachawene kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Sharifa Nyanga, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema kabla ya uteuzi huo, Balozi Simbachawene alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais - Ikulu.

Rais Samia amemteua Nkoba Mabula kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia utalii.

Kabla ya uteuzi, Mabula alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais - Ikulu.

Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba atakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia maliasili.

Rais Samia amemteua Dk Habib Kambanga kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi, alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais - Ikulu.

Pia, amemteua Ally Mketo kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, awali alikuwa Ofisa Tawala Mwandamizi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe. Mketo anachukua nafasi ya Onesmo Kisoka ambaye amestaafu.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mary Caroline Levira ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Anachukua nafasi ya Jaji Gerald Ndika ambaye amemaliza muda wake.

Amemteua Dk Leonard Akwilapo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Dk Akwilapo ni Katibu Mkuu mstaafu na Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) anayechukua nafasi ya Profesa Maurice Mbago aliyemaliza muda wake.

Rais Samia amemteua Dk Noel Mbonde ambaye ni Mkurugenzi mstaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha.