Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raia wa Venezuela wadaiwa ‘kuamua ushindi’ wa Ruto

Muktasari:

Wakati wakili Julie Soweto anayemtetea kiongozi wa Umoja wa Azimio, Raila Odinga akidai raia wa Venezuela ndiye aliyeamua nani Rais wa Kenya, mawakili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wameiambia mahakama nyaraka zinazowasilishwa na mawakili wa Odinga ni za kughushi.

Nairobi. Wakati wakili Julie Soweto anayemtetea kiongozi wa Umoja wa Azimio, Raila Odinga akidai raia wa Venezuela ndiye aliyeamua nani Rais wa Kenya, mawakili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wameiambia mahakama nyaraka zinazowasilishwa na mawakili wa Odinga ni za kughushi.

Juzi Ijumaa Septemba 2, 2022 ilikuwa siku ya mwisho kwa mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, wanaoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, katika kesi ya kupinga ushindi wa urais wa mgombea urais kupitia chama cha UDA, Dk William Ruto.

Ruto alitangazwa mshindi na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kwa kupata asilimia 50.49 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Odinga aliyepata asilimia 48.85. Jumatatu mahakama hiyo itatoa uamuzi wake.

Kabla ya wakili Soweto kujieleza mbele ya mahakama, wakili mwenzake, Paul Mwangi alisisitiza kuwa raia wa Venezuela, Camargo Camargo aliacha alama za vidole vyake kwenye fomu hizo.

Hata hivyo, mawakili wa IEBC walikanusha madai hayo ya upande wa walalamikaji ya mkono wa raia huyo wa Venezuela kwenye uchaguzi wa rais.

Kulingana na wakili, Mahat Somane, raia hao wa Venezuela Camargo, Joel Gustavo Rodriguez Garcia na Salavador Javier Suarez walipewa nafasi maalumu ya kuingia kwenye seva, lakini hawakuwa na uwezo wa kusababisha hila.


Nyaraka la kughushi

Mawakili wa IEBC walitoa hoja mahakamani hapo kwamba jopo la mawakili wa Odinga wamekuwa wakitoa nyaraka za kughushi kwa lengo la kuihadaa mahakama hiyo ifute matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, mwaka huu.

Walidai mahakamni hapo kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha uchaguzi ulivurugwa au Chekubati alivunja sheria.

Mawakili hao walisisitiza kuwa majukumu ya Chekubati yameelezwa kwenye Katiba na kwamba, hakukuwa na haja ya kuwashirikisha makamishna wengine katika kazi ya kuhesabu kura au kuhakiki kura.


Raia wa Venezuela waingilia ‘seva’

Wakati mawakili hao wa IEBC wakikanusha hayo mahakamani, juzi wakili wa Odinga, Julie Soweto aliendelea kusisitiza kwa kuonyesha mkanda wa video mahakamani kuwa kulikuwa na utofauti wa fomu zilizopokelewa na IEBC.

Soweto alidai kuwa fomu iliyotoka kwenye kituo cha kura cha Shule ya Msingi Gacharaigo kwenye Kaunti ya Murang’a ilikuwa na jina la raia wa Venezuela, Jose Camargo.

“Tuliambiwa na bwana Eric Gumbo, wakili wa IEBC kwamba hakukuwepo raia wa kigeni katika uchaguzi huu. Tuliambiwa kwamba hawakuweza kuingilia seva za IEBC. Tazama juu kushoto katika fomu hii kuna jina la Jose Camargo. Huyu ndiye mtu aliyefanya maamuzi ya uchaguzi huu. Je, jina hili liliingiaje hapa?’’ alihoji Soweto.

Soweto alihoji kwamba Carmago ndiye aliyekuwa akiingilia fomu zote 34 katika seva ya IEBC.

“Ishara ya kuingilia fomu hizi iliachwa. Kwa baraka za Mungu tulipata kitu. Hili hatukujifanyia ila hivi ndivyo mambo yalivyofanyika,” alidai wakili huyo.

Dhamira ya wakili Soweto ilikuwa kuionyesha mahakama jinsi matokeo ya uchaguzi wa rais yalivyochakachuliwa kwenye mtandao wa IEBC.

Raia huyo wa kigeni ni mmoja wa Wavenezuela waliokamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKIA kwa madai ya kuwa na mkono kuvuruga uchaguzi. Camargo alikamatwa pamoja na Joel Gustavo, Rodriguez Garcia na Salavador Javier Suarez Julai 21, 2022 wakiwa na vifaa vya uchaguzi. Inasadikika walikuwa wafanyakazi wa kampuni ya teknolojia ya uchaguzi ya Smartmatic International.


Dosari ya hesabu

“Mahali nilipo muhuri wa IEBC unaonekana umepachikwa juu ya muhuri mwingine. Tumeombwa tuonyeshe jinsi takwimu zinavyobadilishwa. Tukiangalia kura zilizopigwa, nambari ya kwanza ni ya Raila Odinga aliyepata 55, Ruto 260, Mwaure moja (David Mwaure wa chama cha Agano) na Wajackoyah sifuri (Profesa George Wajackoyah wa Chama cha Roots).

“Iwapo tutajumlisha jumla ya kura zilizopigwa tunapata 316. Jumla ya kura zote zilizopigwa katika fomu hii ni 321, ikiwa ni tofauti na kile tulichoona. Hii ikimaanisha kwamba tayari hesabu hiyo ina makosa,’’ alisema Soweto.

Juzi pamoja na hoja zingine pia, jopo la majaji saba litatathmini hoja za mawakili wa pande zote tatu na uamuzi wa kesi hiyo utatolewa Jumatatu.


Chekubati ni ‘shujaa’

Mawakili wa watetezi wanaounga mkono matokeo yaliyompa ushindi Dk Ruto walisisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na kwamba, Chebukati ni shujaa.

Jana mawakili wanaoiwakilisha IEBC, walimtetea Chekubati anayedaiwa na upande wa Odinga kufanya kazi bila ushirikiano huku akiwatenga makamishna wenzake wanne.

Mbele ya jopo la majaji, mwanasheria mkuu wa zamani wa Kenya, Profesa Githu Muigai, alisisitiza kuwa Chebukati ni shujaa na alitimiza wajibu wake kama ilivyoagizwa na Katiba.

Profesa Muigai anayeiwakilisha IEBC, alisisitiza kuwa tume hiyo ilifuata maelekezo ya Mahakama ya Juu yaliyotolewa mwaka 2017 wakati matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalipofutwa na uchaguzi kurudiwa.

Alidai mahakamani hapo kuwa IEBC kwenye uchaguzi huu haikurudia makosa ya wakati huo.

Profesa Muigai alidai uchaguzi uliompa ushindi Dk Ruto ulikuwa na makosa ya hapa na pale, ila hakuna sababu ya msingi ya kufuta matokeo yake na hakuna ushahidi, huku akisisitiza Chebukati anashambuliwa bila hoja ya msingi.


Mawakili wapingana

Pia, wakili wa upande wa utetezi, Kamau Karori, alikanusha madai ya mwenzake wa upande wa walalamikaji, Paul Nyamodi, aliyedai Chebukati alijitangaza kuwa ofisa mkuu wa uchaguzi wa Taifa.

Kwa mtazamo wake kauli hizo zilidhamiria kumkashifu mwenyekiti huyo wa IEBC.

Wakili Karori alifafanua kuwa iwapo IEBC ilihitajika kupata ushauri na kauli ya kikao maalumu cha makamishna wote basi ibara ya 138 ya Katiba ingelieleza hivyo.


Zoezi la ukaguzi lakamilika

Kwa upande mwingine, Mahakama ya Juu imeelezea kuwa mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa mtandao wa teknolojia wa IEBC umekamilika.

Juzi Jaji Isaac Lenaola wa jopo la majaji saba aliielezea Mahakama ya Juu kuwa walipokea ripoti kamili ya kikosi cha ufundi na kwamba kila agizo limefuatwa.

Pia, IEBC ilimruhusu Odinga kuona ‘seva’ zake kama ilivyoagizwa na mahakama. Ruhusa hiyo ilikuja siku moja baada ya mawakili wa Odinga kulalamika kunyimwa fursa ya kuingia kwenye ‘seva.’