PAC yazitimua taasisi mbili za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Muktasari:
- Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) leo imeshindwa kuendelea na kikao chake cha kuhoji taasisi mbili zilizoko chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi baada ya maofisa masuhuli kushindwa kufika kwenye kikao cha kamati hiyo.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imezitimua kwenye kikao taasisi mbili zilizoko chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi baada ya maofisa masuhuli kushindwa kufika kwenye kikao hicho.
Taasisi hizo ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambazo zilifanyiwa ukaguzi maalum na Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza leo Jumanne Januari 17, 2023, Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka amesema taasisi hizo zimekuwa matatizo makubwa ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakijirudia rudia.
Amesema ukaguzi huo ulifanyika kwa hesabu za miaka mitano za taasisi hizo kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2021, ulilenga ni kubaini fedha zilizopotea kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo mikataba mibovu.
Hata hivyo, Kaboyoka amesema aliyefika mbele ya kamati hiyo alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi tu ambaye kisheria siyo ofisa masuhuli anayetakiwa kuwajibika kisheria mbele ya kamati hiyo.
Amesema katika kipindi hiki walitaka kufanya tathmini kuona ni kiasi gani cha fedha kimepotea chini ya wizara hii na akashauri ifike mahali kufanyike mabadiliko ya jumla ya watu wanaochezea fedha za umma kwenye taasisi hizo.
“Tunaomba mwenye mamlaka ya kuchukua hatua achukue hatua. Haya mambo yamekuwa yakijirudia. Pia sisi tunasikia huko mtaani wanasema Bunge si kazi yake kutoa mapendekezo maazimio na kelele hawa ni wasiasa wamezoe kupiga kelele,” amesema.
Kaboyoka amesema taasisi hizo zimekuwa zikifanya kazi kwa mazoea na hivyo leo kamati hiyo imesema haiwezi kupoteza muda wa kuzungumza nao.
“Kuwauliza maswali yale yale, majibu yale yale na matendo hamna,”amesema Kaboyoka baada ya kuwaondoa katika kikao hicho viongozi wa taasisi hizo walioambatana na Naibu Katibu Mkuu wa sekta ya ujenzi.
Aidha, Kaboyoka amesema kamati hiyo haioni haja ya kuwaita tena katika vikao bali wataandaa ripoti yao na kupeleka ndani ya Bunge ili liamue maana haliwezi kuendelea kudharauliwa.