Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Oryx yazindua mwongozo wa usalama wa LPG

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoite Araman(kulia) Meneja miradi nishati safi ya kupikia Jennifer Mosha, Skauti Mkuu Tanzania Rashid Mchata(wa pili kushoto) pamoja na Kamishina Mkuu wa Skauti Tanzania Abubakari Mtitu wakikata utepe kuzinduzi Kitabu cha Mwongozo wa matumizi salama nishati safi ya kupikia ya LPG. Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 15, 2025 jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas, Peter Ndomba, kikilenga kuwa rejea ya kudumu kwa watumiaji wa gesi ya LPG, licha ya kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Dar es Salaam. Kampuni ya Oryx Tanzania imezindua Kitabu cha Mwongozo wa Matumizi Salama ya Gesi ya LPG na kusaini makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu na Chama cha Skauti Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha elimu ya matumizi salama ya gesi ya kupikia kwa wananchi kupitia mtandao wa vijana wa Skauti nchini.

Akizungumza leo Jumatano, Julai 15, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho na utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman amesema mwongozo huo ni nyenzo muhimu ya kujifunzia na kufundishia matumizi sahihi ya gesi ya LPG, huku ushirikiano na Chama cha Skauti ukilenga kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi.

Amesema pamoja na kampuni kutekeleza wajibu wake kwa wanahisa, wafanyakazi na Serikali, pia inaamini wananchi ni wadau wake wakuu, ndiyo maana imeamua kuwekeza katika utoaji wa elimu ya usalama ili kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.

"Tunataka kuona Watanzania wengi zaidi wakitumia gesi ya LPG kwa usalama. Hatuwezi kuwafikia mamilioni ya watumiaji peke yetu, ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania ambacho kina mtandao mpana wa vijana wenye uwezo wa kuifikisha elimu hii kwa jamii," amesema Araman.

Amefafanua kuwa kupitia makubaliano hayo, Oryx Gas itawajengea uwezo wakufunzi wa Skauti kwa mfumo wa kumfundisha mkufunzi, ambao utawawezesha kuwafundisha vijana wengine na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu matumizi salama ya gesi ya LPG.

Araman amesema kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas, Peter Ndomba, kikilenga kuwa rejea ya kudumu kwa watumiaji wa gesi ya LPG, licha ya kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali.

"Ni muhimu kuwa na nyenzo ambayo mtu anaweza kuishika mkononi, kuisoma mara kwa mara na kuirejea kila anapohitaji kujifunza matumizi salama ya gesi," amesema.

Ameongeza kuwa kitabu hicho kitapatikana katika nakala zilizochapishwa na pia kwa njia ya kidijitali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas na mtunzi wa kitabu hicho, Peter Ndomba amesema wazo la kuandaa mwongozo huo lilitokana na uongozi wa kampuni baada ya kubaini kuwa pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, elimu ya usalama ni muhimu kwa kila mtumiaji wa gesi.

"Tunataka kuhakikisha kila anayechagua kutumia gesi yetu anafanya hivyo kwa usalama. Kitabu hiki kitampa mtumiaji uelewa mpana kuhusu matumizi salama ya gesi ya LPG na baada ya kukamilika kwa taratibu za hatimiliki, kitatumika pia kama nyenzo ya kufundishia katika taasisi mbalimbali, ikiwamo shuleni," amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta amesema makubaliano hayo si tukio la kusaini mkataba pekee, bali ni mwanzo wa ushirikiano utakaowawezesha vijana kupata maarifa, ujuzi na fursa zitakazochangia maendeleo ya taifa.

Mchatta amesema Chama cha Skauti kinaamini kuwa vijana wenye maarifa, maadili na nidhamu ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuwajengea uwezo katika matumizi ya nishati safi, usalama na hata fursa za kiuchumi.

"Tutahakikisha ushirikiano huu unatekelezwa kwa ufanisi ili vijana wetu wawe mabalozi wa elimu ya matumizi salama ya gesi na kuchangia kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya LPG," amesema.

Naye Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abubakar Mtitu amesema makubaliano hayo yanaendana na dhamira ya Skauti ya kuitumikia jamii kwa kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Amesema chama hicho kitaendelea kutumia mtandao wake wa vijana nchini kueneza elimu ya matumizi salama ya gesi ya LPG sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hatua itakayochangia ustawi wa jamii na uhifadhi wa mazingira.