Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ole Sabaya asomewa maelezo upya, akana

Ole Sabaya asomewa maelezo upya, akana

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, jana ilikubali maombi madogo ya upande wa Jamhuri ya kufanya marekebisho madogo ya jina la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, baada ya kuandikwa Sayaba badala ya Sabaya kwenye maelezo ya mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha yanayomkabili na wenzake wawili.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, jana ilikubali maombi madogo ya upande wa Jamhuri ya kufanya marekebisho madogo ya jina la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, baada ya kuandikwa Sayaba badala ya Sabaya kwenye maelezo ya mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha yanayomkabili na wenzake wawili.

Malumbano ya kisheria yalidumu kwa saa mbili kuhusiana na makosa hayo na kusababisha kesi kuahirishwa kwa muda ili hakimu aweze kutoa uamuzi mdogo.

Malumbano hayo yalitokana na upande wa Jamhuri kupitia Wakili wake Mwandamizi, Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka kuomba marekebisho madogo ya hati hiyo baada ya kubaini makosa ya kiuchapaji.

Baada ya kuahirisha kesi hiyo kwa zaidi ya nusu saa, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, anayesikiliza kesi hiyo alitoa uamuzi mdogo na kusema kwakuwa maombi ya marekebisho madogo hayatakiuka haki ya mshtakiwa wa kwanza, yanakubaliwa.

Alisema wakili wa mshtakiwa wa kwanza anapewa mwongozo wa nafasi kwa mshtakiwa kutoa ushahidi wake wa msingi tena, kuhusu jambo hilo la jina.

Baada ya mahakama kuridhia hati hiyo ilifanyiwa marekebisho hayo madogo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula aliwasomea washtakiwa hao makosa yao upya.

Washtakiwa wengine ni Sylvester Nyengu na Daniel Mbura, ambapo walikana kuyatenda.

Baada ya kuwasomea upya mashitaka hayo, Hakimu Amworo alimtaka Wakili Mosses Mahuna kumuongoza mshtakiwa huyo na kumuuliza swali kutokana na kipengele hicho kilichorekebishwa cha usahihi wa jina lake la tatu hasa baada ya kueleza mahakama hawana nia kuita shahidi yeyote kutokana na marekebisho hayo.

Awali kabla ya kuanza kwa shauri hilo, wakili Kweka aliomba kabla ya kuendelea kuhoji wanaomba kuwasilisha maombi madogo yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili Chavula.

Wakili Chavula alidai kuwa wanaomba kuwasilisha maombi hayo madogo chini ya kifungu namba 234(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 na kuomba kufanya marekebisho madogo ya hati hiyo baada ya kubaini kwamba kuna makosa ya kiuchapaji yaliyojitokeza wakati wa uchapaji wa jina la tatu la mshtakiwa wa kwanza.

“Ukiangalia jina la tatu la mshtakiwa wa kwanza kwenye eneo la maelezo ya kosa linatofautiana na jina la tatu linaloonekana juu kabisa kwenye hati ya mashtaka, ukiangalia juu anasomeka Sabaya lakini ukiangalia kwenye maelezo ya kosa kuanzia kosa la kwanza hadi la tatu jina hilo linaonekana kuandikwa Sayaba,” alieleza

“Lakini si hapo tu, hata ukiangalia kwenye sehemu ya maelezo binafsi ya mshtakiwa utaona jina la tatu limeandikwa Sabaya, hata ukiangalia kwenye facts, ambazo tulizitoa kwa mahakama na wenzetu na hata wakati wa usomaji mshtakiwa wa kwanza amekuwa akitambulika kwa jina la Sabaya na hata wakati wanasomewa maelezo ya awali wanasomewa maelezo ya awali alikubali jina lake la tatu ni Sabaya,” alisema.

“Mazingira yote haya yanaonyesha kwamba hilo jina la Sayaba, ni makosa ya uchapaji na marekebisho yake kwa namna yoyote ile kwa kuzingatia merits ya kesi ilivyo kama ambavyo nimeeleza mahakama kuanzia usomaji wa maelezo ya awali, hakuna injustice yoyote inaweza kutokea kwa sababu ya marekebisho ama masahihisho hayo,” alidai.

Akijibu hoja hiyo, Wakili anayemtetea Sabaya, Mosses Mahuna alidai mshtakiwa namba moja alikutwa na kesi ya kujibu mahakamani hapo kwa hati hiyo ya Julai 16, 2021 na alikutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi yao na mshtakiwa alianza kujitetea.

Alidai kuwa mshtakiwa alianza kujitetea na wakati wa utetezi wake aliainisha upungufu uliopo ndani ya hati hiyo iliyomkuta ana kesi ya kujibu, ikiwemo kukosewa kwa jina hilo katika maelezo ya mashtaka matatu yanayomkabili na wenzake wawili.

“Na makosa hayo ya uchapaji tunaambiwa yako kwenye maelezo ya makosa yote matatu, hati ambayo imethibitishwa na mashahidi 11 na mawakili wanne wa Serikali, wakati hiyo ni miongoni mwa vitu muhimu sana katika kesi na tumeanza kujitetea.

“Mheshimiwa kifungu namba 234(1) kilichorejewa na Wakili Chavula kinaweka mazingira na Wakili hajatueleza lakini anaiomba mahakama kwa ajili ya marekebisho madogo, lazima hati ielezwe ni “defective in substance or formal” lazima hilo lieleweke kuanzia mwanzo wakati wa maombi hayo.

“La mwisho ambalo ni la msingi zaidi ni endapo mahakama itaona ni vyema kufanya hayo marekebisho je, inaweza kufanya hivyo bila kutokutenda haki? Au zikifanyika zisije kumkosesha haki mshitakiwa wa kwanza na tulivyotangulia kueleza kesi ya Jamhuri ilishafungwa na alishajitetea na kueleza mapungufu ya hati, ikiwemo hilo jina la Sayaba.”

Akijibu hoja hizo, Wakili Chavula aliieleza mahakama kuwa mawakili kama maofisa wa mahakama makosa waliyoyaona walipaswa kuieleza mahakama kama wakili wa mshitakiwa wa pili waliieleza mahakama juu ya kurekebishwa jina la mteja wao, hivyo walipaswa kufanya jukumu lao.

“Tunasikitika kuona kwamba tunacheza game ya hide and seek na hatukutegemea kuyakuta hayo kutoka kwa Wakili kama msomi aliyetoka kuzungumza, hasa kwenye haki za kijinai na usawa mbele ya sheria na ni suala la kikatiba, msomi kusema tuliyaona toka mwanzo tukaamua kukaa kimya, hatukutegemea na wanapaswa kuona aibu juu ya hili.

“Kifungu 234 (1) alichokinukuu mwenzetu cha kwanza sheria inasema wakati wowote wa shauri ndo sharti la kwanza,kwa hiyo inawezekana ikawa hata wakati wa kusoma hukumu sheria haijaweka ukomo,” alidai na kuongeza:

“Hivyo hoja ya mwenzetu kusema kwamba eti kwa sababu yuko kwenye kuhojiwa Mahakama haipaswi kujielekeza huko, ni hoja ambayo kisheria haina miguu ya kusimama, sheria inasema ni wakati wowote. Na wakati anasomewa maelezo ya awali na mashtaka aliitwa jina la Sabaya, kama aliona kuna jina tofauti alitakiwa akanushe toka awali.

“Na hata tulipomsomea mashtaka alikanusha mashtaka lakini hakuiambia mahakama anayeshtakiwa siyo mimi ni mtu mwingine na yeye anakiri mbele ya mahakama kwamba aliona hilo na anaamua kukaa kimya.”

Akiwasilisha hoja ya nyongeza, Wakili Kweka aliieleza mahakama kuwa maombi yao yana mashiko na kwa sababu suala hilo liko ndani ya mamlaka ya mahakama hiyo kisheria wanaomba iruhusu ombi hilo na kupewa ruhusa ya marekebisho hayo madogo.

Aliieleza mahakama kuwa hati ya mashtaka ni lazima iwe na vitu sita, ikiwemo mahakama na namba ya kesi ili kujua mtu anafikishwa mahakama gani na ina mamlaka na katika suala hili ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, maelezo ya makosa, maelezo ya mashtaka, kusainiwa na tarehe hati ilipoletwa mahakamani ambapo viko katika hati hiyo.

Baada ya uamuzi huo mdogo, Wakili Mahuna alimuuliza mshtakiwa huyo swali moja ambapo mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo

Wakili Mahuna: Shahidi baada ya hati kurekebishwa nitakuuliza swali moja unijibu kwa ufupi na ufasaha

Kwenye maelezo yako ya awali ulisema kuna mtu anaitwa Sayaba, hapa mahakama kwa mashtaka yote matatu yanakutaja wewe Lengai Ole Sabaya, kwa ufupi una lipi la kueleza mahakama kutenda makosa hayo?

Shahidi: Mheshimiwa hakimu nayakanusha mashtaka yote yaliyotajwa, sijahusika na ninashangaa kwanini majina yangu yako wakati kwa namna yoyote sihusiki nayo na siyafahamu.

Baada ya swali hilo Mawakili Ngemela, Kahunduka, Gwemelo walimhoji mshtakiwa huyo ambapo sehemu ya mahojiano baina yake na Wakili Ngemela ni kama ifuatavyo:

Wakili: Shahidi hapa mahakamani alikuja mtu anaitwa Bakari Msangi, katika ushahidi wake alisema katika Sh 10,000 alinunua mapapai manne unakumbuka hivyo?

Shahidi: Ndiyo nakumbuka

Wakili: Sasa kuna sehemu yoyote katika ushahidi wake alisema baadhi ya mapapai aliyokuwa amenunua yaliibwa?

Shahidi: Hakuwahi kusema.

Wakili: Shahidi kuna mtu alikuja hapa mahakamani (Magdalena Mallya, shahidi wa nane wa Jamhuri) ulimsikia akisema kwamba ulimuelekezea bastola kichwani na mdomoni na ulimtukana.

Shahidi: Nilimsikia hapa mahakamani akisema hivyo.

Wakili: Sasa kuna shtaka lolote linalokukabili kuhusu jambo hilo alilokuwa akilalamikia hapa mahakamani?

Shahidi: Sina shtaka hilo mheshimiwa.

Wakili: Shahidi kuna mashahidi wawili (2, 4) ambao walisema kwamba tukio lilitokea lakini pamoja na vitu vilivyofanyika kuna mashine mbili za EFD’s na nyaraka ziliibwa.

Shahidi: Nakumbuka aliyesema hivyo ni shahidi namba mbili, nne na sita.

Wakili: Na kadiri ya ushahidi wao walisema hizo EFD’s zilichukuliwa kwenye duka la nani?

Shahidi: Kwa mujibu wa maelezo yao walisema zimechukuliwa duka waliloliita Shaahid Stores.

Wakili: Na kadri ya maelezo yao inaonekana tukio hilo mashine za EFD’s zilikuwa zimechukuliwa.

Shahidi: Walidai hivyo.

Wakili: Bila shaka hizo EFD’s na vitu vingine sijui nyaraka ni mali si kweli?

Shahidi: Ndiyo ni mali.

Wakili: Sasa kama ni kweli wizi huo wakati unafanyika si ni kweli kwamba zingekuwa katika hati ya mshtaka nazo zingejumuishwa?

Shahidi: Kama ziliibiwa pamoja zilipaswa kuwa kwenye hati hiyo kwani ni mali yao na wanadai kuibiwa.

Wakili: Ni kweli kwamba katika mashahidi walioletwa hakuna shahidi hata mmoja aliona Sh 2,679,000 milioni zikichukuliwa katika tukio hilo.

Shahidi: Hakukuwepo na aliyeshuhudia kwa mujibu wa ushahidi wao wenyewe.