Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Njia za kukabiliana na baridi kali nchini

Muktasari:

  • Siku moja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza kuhusu mwelekeo wa kipupwe kinachoatarajiwa kuwa baridi kali chini ya nyuzi joto 4°C, tahadhari za kiafya zimetolewa kwa watu waishio kwenye mikoa tajwa.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza kuhusu mwelekeo wa kipupwe kinachoatarajiwa kuwa baridi kali chini ya nyuzi joto 4°C, tahadhari za kiafya zimetolewa kwa watu waishio kwenye mikoa tajwa.

Mwelekeo huo ulitarajiwa kuanza Juni hadi Agosti mwaka huu katika mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi ikuhusisha Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro.

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Elisha Osati alisema baridi inapokuwa kali kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko kwenye njia ya hewa na mapafu na kurahisisha wadudu kusafiri.

Alisema hali hiyo inapotokea inasababisha kifua, mafua, homa hata homa ya mapafu ambayo huwasumbua zaidi watoto kutokana na kushindwa kuhimili mabadiliko hayo.

“Ni kipindi ambacho watu wanapaswa kuwa makini na kuongeza uangalizi kwa watoto, hasa wadogo kabisa, wahakikishe muda wote wamevaa nguo ambazo zinakinga miili yao dhidi ya baridi na ambazo zitasaidia pia kuhifadhi joto.

Ngozi pia ni vyema ikapakwa mafuta ya mgando ili kuikinga na baridi, hili pia linapaswa kuzingatiwa hata na watu wazima kwa sababu baridi haichagui iingie kwa nani na wakati gani,” alisema Dk Osati.

Dk Osati alisema kutokana na hali hiyo ya hewa inashauriwa kuviepuka vyakula vya baridi na vilivyopoa baada ya kupikwa muda mrefu.

“Kipindi hiki vyakula viliwe vikiwa na moto, vikipoa kuna uwezekano wa wadudu kuingia na vikiwa na mafuta vikipoa yale mafuta yataganda, hivyo havitakuwa sahihi katika wakati huu wenye baridi,” alisema.

Dk Osati alisema kundi jingine linalopaswa kujihadhari zaidi katika kipindi hiki ni wenye matatizo ya pumu, kifua, magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yanayohusisha mfumo wa upumuaji.

Alisema, “Ikitokea mtoto amebanwa na kifua huna sababu ya kusubiri, mpeleke kwenye kituo cha afya kwa ajili ya uangalizi wa wataalamu.”

Walichosema TMA

Juzi Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti na Matumizi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a alisema hali ya joto kiasi na baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi nchini huku akitaja mikoa mitano itakuwa na kiwango cha baridi kati ya nyuzi joto 4 hadi 14, huku maeneo yenye miinuko yakitarajiwa chini ya nyuzi joto nne.