Ngoma mbichi kesi ya Luongo anayedaiwa kumuua mkewe, kumchoma moto

Mshitakiwa Hamisi Luogo (katikati). Picha na Maktaba
Muktasari:
- Luongo anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe aitwaye, Naomi Marijani na inadaiwa kuwa baada ya kumuuua alimchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara, Hamisi Luongo maarufu kama Meshack (41).
Luongo anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe aitwaye, Naomi Marijani na inadaiwa kuwa baada ya kumuuua alimchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Wakili wa Serikali, Adolf Verandumi, leo Januari 13, 2023 ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Verandumi ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga, anayesikiliza shauri hilo.
" Kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hili bado unaendelea hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Verandumi.
Hakimu Ngimilanga baada ya kusikiliza upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo leo, mshtakiwa huyo hakuweza kuletwa mahakamani hapo na badala yake kesi hiyo imeahirishwa kwa njia ya video Conference akiwa gerezani.
Kwa kawaida kesi nyingi ambazo zipo katika hatua ya kutajwa zinazowakabili washtakiwa ambao makosa yao hayana dhamana kwa mujibu wa sheria ikiwemo kesi ya mauaji, unyang'anyi wa kutumia silaha washtakiwa huwa hawapelekwi mahakamani na badala yake kesi hizo huahirishwa kwa njia ya video conference.
Hata hivyo, upelelezi wa kesi hizo, unapokamilika na kuanza kusikilizwa, washtakiwa hao hupelekwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya mauaji namba 5/2022.
Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole, Wilaya ya Kigamboni, ambapo alimuua mkewe aitwaye Naomi Marijani.