Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neema mpya Lindi, Mtwara Serikali ikiachia Sh669 bilioni

Muktasari:

  • Ujenzi wa barabara ya Mnivata - Newala - Masasi kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti utazifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi.

Mtwara. Katika kuhakikisha inatekeleza ahadi ya kuifungua kiuchumi mikoa ya Lindi na Mtwara na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja, Serikali imetangaza kupeleka Sh669 bilioni.

Fedha hizo zinakwenda kutumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja lengo likiwa ni kuboresha usafiri na kuifungua mikoa hiyo kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega leo Jumanne Mei 27,2025 ambapo amesema barabara na madaraja hayo yatajengwa kupitia barabara za Mtwara –Mingoyo (Mnazi mmoja)-Masasi  itakayogharimu Sh401 bilioni huku barabara za Mtwara Tandahimba-Newala-Masasi itajengwa kwa Sh268 bilioni hadi kukamilika kwake.

Ulega ambaye yuko ziarani katika mikoa ya Kusini, amesema kutolewa kwa fedha hizo ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ili kuhakikisha inafunguka kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kiuchumi.

“Wananchi wa mikoa ya Kusini, ninawaletea salamu hizi za Rais wetu (Samia Suluhu Hassan). Hizi barabara zikikamilika kutakuwa na taa za barabarani takribani 4,800 kutoka Mtwara hadi Masasi. Kusini kutang’ara kwa mwanga nyakati za usiku na kutapendeza. Kwenye barabara nzuri, uchumi unafunguka na kwenye mwanga kwa saa 24, biashara zinafanyika muda wote,” amesema Ulega.

Ziara hiyo ya Ulega ni utekelezaji wa maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuitaka Serikali kuangalia maendeleo ya ukarabati wa barabara na miundombinu mingine ya ujenzi iliyoharibiwa wakati wa mvua za masika na kimbunga cha Hidaya kuanzia mwishoni mwa mwaka 2024 na mwanzoni mwa mwaka 2025.

Kuhusu mchanganuo wa fedha hizo, Ulega amesema katika Sh230 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti (m84) ili kuzifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi kupitia usafirishaji wa abiria na mazao.

“Kazi kubwa inafanywa katika mikoa ya Kusini inalenga kufungua fursa za kiuchumi kwa haraka ili mazao ya biashara na chakula yapate thamani kwa kufika katika masoko kwa urahisi pamoja na kupunguza gharama na muda wa usafiri,” amesisitiza Ulega.

Kuhusu faida nyingine za miradi hiyo ya ujenzi, mbunge huyo wa Mkuranga, amewambia wananchi wa mikoa ya Kusini kwamba, makandarasi waliopewa zabuni ya kujenga barabara hiyo watatakiwa pia kuboresha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho, nyumba za madaktari na mambo mengine kwa mujibu wa mkataba.

Amewataka makandarasi wanaojenga barabara ya Mnivata-Masasi kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wazawa wa maeneo barabara inakopita kwa kushirikisha ofisi za Serikali za Mtaa na Kata za Wilaya.

Amesisitiza kuwa licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara, miradi hiyo inapaswa kuzalisha ajira kwa wazawa na kuacha ujuzi ili uweze kuwasaidia katika majukumu mengine ya kijamii na kiuchumi.

Ulega ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia ameshatoa kibali cha ukarabati wa barabara ya Mtwara hadi Mingoyo (Mnazi Mmoja) na Mingoyo hadi Masasi ambapo takribani Bilioni 152 zitatumika katika barabara hiyo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John ameeleza mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya China WuYi umegawanywa katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ya Mnivata - Mitesa (km 100) unatekelezwa kwa muda wa miezi 36 na sehemu ya pili ya Mitesa - Masasi (km 60) na ujenzi wa Daraja la Mwiti (m 84) unatekelezwa kwa muda wa miezi 30.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tandahimba Ahmad Katani ameishukuru Serikali kwa mradi wa barabara hiyo kwani ni barabara ya kiuchumi kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Korosho.