NEC yaongeza vituo vya kupigia kura 858 kuelekea 2020

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage akizungumza wakati kufungua mkutano wa Tume, Vyama vya Siasa na wadau unaofanyika jijini Dar es Salaam leo
Muktasari:
Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) imeongeza vituo vya kupigia kura 858 kwa lengo la kitatua kero za wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.
Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania imeongeza vituo vya kupigia kura 858 kutoka 36,549 vya mwaka 2015 hadi 37,407 ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage leo Jumanne Machi 5,2019 alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa vyama vya siasa, akisema ongezeko hilo ni matokeo ya uhakiki unaoendelea nchini.
Mbali na kuongeza idadi ya vituo, Jaji Kaijage amesema vituo 6,208 vimebadilishwa majina na vituo 817 vimehamishwa kutoka kijiji/mtaa mmoja kwenda mwingine.
"Vituo 19 vimeongezwa kutoka kata moja kwenda nyingine. Matokeo ya uhakiki wa vituo vya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar yanaonyesha vituo vimeongezeka kutoka 380 bado vituo 407," amesema Jaji Kaijage.
Kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura, Jaji Kaijage amesema mchakato wa kupata vifaa vya kukarabati machine za BVR umekamilika.
"Kinachosubiriwa ni kuvifanyia majaribio ya uandikishaji katika kata mbili za Kihonda katika manispaa ya Morogoro na kata ya Kibuta katika Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe, " amesema.
Akizungumzia lengo la mkutano huo, Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Athuman Kihamia amesema ni kufafanua mabadiliko ya kanuni za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura la 2008.