NBC yaingia makubaliano kutoa huduma mahususi kwa wafugaji

Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki ya NBC, Msafiri Shayo (kulia) na Katibu Mkuu wa CCWT, Mathayo Daniel (kushoto) wakisaini hati za makubalino baina ya taasisi hizo mbili zinazolenga kufungua milango kwa benki ya NBC katika kutoa huduma za kifedha zenye upendeleo maalum kwa wafugaji.
Muktasari:
- Makubaliano haya yatawezesha wafugaji na wadau katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo kupata huduma za kifedha kulingana na mahitaji yao.
Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano na Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) ili kutoa huduma za kifedha zilizobuniwa mahsusi kwa wafugaji nchini.
Makubaliano haya yatawezesha wafugaji na wadau katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo kupata huduma za kifedha kulingana na mahitaji yao.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo Alhamisi Septemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na viongozi wa pande zote mbili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki ya NBC, Msafiri Shayo amesema hatua hiyo ni muendelezo wa jitihada za NBC katika kuboresha mnyororo wa thamani wa wakulima na wafugaji nchini kupitia uwezeshaji.
Hata hivyo, amesema lengo ni kuwasaidia wadau hao kuendesha shughuli zao kwa kisasa zaidi, kuongeza vipato na ajira, na hatimaye kukuza uchumi wa taifa.
“Tunatarajia kuongeza upatikanaji wa chakula na lishe kupitia huduma zetu za kifedha, ikiwemo mikopo, ili kuwawezesha wafugaji kuboresha ufanisi wao katika shughuli zao na biashara,” amesema Shayo.
Kwa mujibu wa Shayo, wafugaji watakaojiunga na huduma ya Mfugaji Akaunti watapata faida kama mikopo ya kuendeleza shughuli zao, riba kwa salio la akiba lililo juu ya Sh100,000 kila mwezi na akaunti bure bila makato ya uendeshaji.
Amesema watafaidika pia na bima mbalimbali, taarifa za akaunti bila makato, huduma nafuu za kutoa fedha, huduma za kibenki kwa njia ya simu (NBC Kiganjani), pamoja na kadi ya NBC Visa kwa ajili ya matumizi duniani kote.
Naye Raymond Urassa, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo Wadogo, Lariba na Wakulima kutoka NBC, amesema mpango huo utaongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya mifugo.
“Mikopo itakayopatikana itasaidia kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa, na kuboresha miundombinu ya uwekezaji,” amesema.
Katibu Mkuu wa CCWT, Mathayo Daniel ameishukuru NBC kwa kuangalia kundi hilo muhimu, akisema kuwa huduma hizi zitachochea uzalishaji na ukuaji wa uchumi binafsi na taifa.
“Tunatarajia kuongeza kasi ya uzalishaji na kutoa bidhaa bora zaidi kwa faida ya jamii. Tunawashukuru NBC kwa fursa hii,” amesema Mathayo.