Nape ataja sababu za kupanda bei vifurushi

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye
Muktasari:
Serikali imesema kupanda kwa bei ya vifurushi vya intaneti katika mitandao ya simu kunatokana na marekebisho ya makosa yaliyofanyika.
Dar es Salaam. Wakati wananchi wakilalamikia kupanda kwa bei ya vifurushi vya mawasiliano na intaneti katika mitandao ya simu, Serikali imesema hatua hiyo ni matokeo ya marekebisho ya makosa yaliyowahi kufanyika.
Katika siku hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la bei ya vifurushi vya mawasiliano na intaneti katika mitandao ya simu, hali iliyoibua malalamiko kutoka kwa wananchi.
Mathalan, katika moja ya mitandao hiyo, kifurushi cha gigabaiti 1.2 kwa siku tatu kiliuzwa Sh2,000, lakini sasa kiasi hicho cha fedha kinawezesha kupata megabaiti 985 tu, zikipungua kwa asilimia 17.9.
Katika mtandao mwingine nchini, kifurushi cha data kilichouzwa kwa Sh1,000 kiliwezesha megabaiti 450 kwa wiki, lakini sasa kwa bei hiyo zinapatikana megabaiti 350 sawa na upungufu wa asilimia 10.
Malalamiko kuhusu ongezeko hilo la vifurushi, yanamuibua Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anayesema mabadiliko hayo yanatokana na mabadiliko yanayofanywa na Serikali.
“Kulikuwa na kelele za kupanda kwa bando duniani kote, lakini ambacho kilitokea, tulikuwa tunafanya marekebisho ya makosa yaliyofanyika,” amesema.
Kila baada ya miaka minne, amesema inafanyika tathmini ya gharama za kusafirisha bando kutoka eneo moja kwenda lingine.
Kulingana na Nape, tathmini ya mwaka 2018 iliweka bei elekezi ya kusafirisha bando kutoka Sh2.03 hadi Sh9.35.
Wakati wa utekelezaji, ameeleza baadhi ya watoa huduma za mtandao walifika hadi Sh45 huku wengine wakishuka hadi Sh0.6.
“Tulipokuja tukasema hatuwezi kuwa na bei elekezi alafu haifuatwi, kwa hiyo aliye juu ashuke na aliyepitiliza chini arudi kwenye bei elekezi,” amesema.
Amesema Aprili mwaka huu, watoa huduma walitaka kulitekeleza hilo kwa mara moja, lakini tasnia ingesikitika.
“Serikali ikasema hii sio namna ya kufanya, kama mnataka kurudi tutafute namna ya kurudi taratibu, kwa hiyo waliokuwa chini wamepanda hadi Oktoba ndiyo zilikuwa kelele za mwisho na sasa tumefikia kwenye viwango stahiki hapa hakuna kupanda,” amesema.
Hata hivyo, amebainisha tathmini ya miaka minne inatarajiwa kufanyika mwaka huu na kuhitimishwa Desemba na ripoti itatoa viwango vipya na matumaini ni kwamba bando litashuka.
“Sababu za kushuka ni kwamba kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, ongezeko la watumiaji wa mtandao wakiwa wanatumia wachache gharama inakuwa kubwa wakiwa wengi inapungua,” amesema.
Pamoja na hayo, amesema Serikali pia inachukua hatua kadhaa ikiwemo kufanya maboresho ya sheria.