Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nape akubali lawama ‘bao la mkono’

Muktasari:

Amekubali kulaumiwa kwa kauli yake 

Dar es Salaam. Baada ya kuingia katika malumbano makali na wafuasi wake wa akaunti yake ya Twitter kwenye mitandao ya kijamii, mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ametoa ya moyoni.

Amekubali kulaumiwa kwa kauli yake ya “bao la mkono”, lakini akataka asihusishwe na sakata la kufungiwa kwa mtandao wa kijamii wa Jukwaa la Jamii, maarufu kwa jina la Jamii Forums.

Tangu juzi, waziri huyo wa zamani wa habari, amekuwa akilumbana na watu wanaofuatilia akaunti yake ya Twitter baada ya kutuma ujumbe unaoonyesha tatizo la kufungiwa kwa Jamii Forum.

“Hili la JF linafikirisha! ukizuia watu kusema wayawazayo unaweza kukutana nao... kimya kimya,” aliandika Nape katika akaunti yake juzi na kuibua mashambulizi kutoka sehemu tofauti.

Wafuasi walimtaka asijihusishe na masuala ya uhuru wa vyombo vya habari kwa madai kuwa ndiye mwanzilishi wa sheria zinazokandamizi vyombo vya habari.

Akizungumza na Mwananchi jana mjini Dodoma, Nape alisema baada ya watu kuona ameweka ujumbe huo walianza kumshutumu kwa mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumtuhumu kuwa ndiye aliyehusika kutunga sheria hiyo inayotaka mitandao ya jamii ambayo haijasajiliwa kusitisha usambazaji wa taarifa.

Lakini, Nape aliwajibu kuwa hahusiki na Sheria ya Makosa ya Kimtandao wala kanuni zake zilizosababisha Jamii Forums kufungwa kwa kuwa ilitungwa hata kabla ya yeye kuwa mbunge na baadaye waziri.

“Watu hawakuishia kunituhumu na utunzi wa sheria hii ambayo kiukweli ilipotungwa sikuwa mbunge na wengine ndio wakaja na hili neno bao la mkono,” alisema katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi wa CCM alipozungumza na Mwananchi jana.

Alisema baada ya kuona upotoshaji kuhusu kauli ya bao la mkono ndipo alipoandika tena kauli hiyo iliyoibua utata wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Nilaumuni kwa bao la mkono lakini sio kwa hili la JF’,” Nape ameandika katika akaunti hiyo na kuibua mjadala mwingine.

Nape alitoa kauli hiyo ya “bao la mkono” Juni 22, 2015 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema, Mwanza wakati akiwa katika msafara wa katibu mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa ni CCM kujiandaa kushinda uchaguzi kwa njia yoyote, hata isiyo halali kutokana na kufananishwa na bao la mkono lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Argentina, Diego Maradona katika mechi ya soka ya Kombe la Dunia, mchezo ambao wachezaji hawaruhusiwi kutumia mikono isipokuwa kwa makipa tu.

Wakati huo, Nape alilazimika kutoa ufafanuzi kujaribu kuiweka sawa kauli yake katika kipindi ambacho joto la uchaguzi lilikuwa linapanda hivyo kufanya iwe shida kwa wapinzani kumuelewa.

Kadhia hiyo ndiyo imemkumba tena jana baada ya kurudia kauli hiyo ya “bao la mkono” na kulazimika kurudi Twitter kufafanua.

“Naomba turudishe visu vyetu kwenye ala: namaanisha nilaumiwe kwa kuasisi usemi wa ‘bao la mkono’. Simjui na siamini kama kuna aliyefunga bao la mkono mwaka 2015. Mimi mwenyewe nilibanwa Mtama kampeni nzima na kuponea chupuchupu,” ameandika Nape kwenye akaunti yake jana mchana.

Lakini ufafanuzi huo bado haujakubalika kwa wafuasi wake, na hadi jana saa 12:40 jioni, watu 520 walikuwa wameupenda na wengine 86 kuutuma tena kwenye akaunti zao ujumbe huo.

Lakini waliochangia maoni yao ndio walioonyesha kukerwa, wakimtuhumu kuwa alitoa ufafanuzi ili kurekebisha mambo baada ya twiti yake ya kwanza kuonekana kuwa na madhara.

“Brother, wewe ni mtu jasiri tena mpiganaji, ila kwa sasa nakuona ukiwa na sura mbilimbili; ya woga na jasiri. Woga unaposti post zako kwa mafumbo sana yenye maana zaidi ya moja. Ujasiri, unapolitetea jimbo bungeni. Kwa nini tu usiwe upande mmoja?” anahoji mtu wa kwanza kutoa maoni katika twiti hiyo.

Lakini Nape aliliambia Mwananchi jana kuwa watu wasitake kumuwekea maneno mdomoni ambayo hakusema wala kumaanisha kwa maslahi yao.

Juzi, Jamii Forum walisitisha huduma zao, kutokana na tangazo la Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) lililosema kuwa ni kosa kisheria kutoa huduma ya maudhui ya mtandaoni bila kuwa na leseni.

Kanuni ya maudhui ya kimtandao ya mwaka 2018, inawataka wachapishaji wa maudhui kwa njia ya blogu, na majukwaa ya mtandaoni kusajiliwa na TCRA na kupata leseni, kulingana na gharama zilizoainishwa.

Jana, TCRA ilitoa ufafanuzi ikisema wanaoweka maudhui kwenye mitandao ya kijamii na wale wanaoweka jukwaa kwa ajili ya mijadala wote wanatakiwa kusajiliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema huwezi kutoa huduma bila kuzalisha maudhui, huku akitoa mfano wa moja ya televisheni nchini inayotoa huduma kupitia uzalishaji wa maudhui yake.

Kilaba alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku mbili baada ya Jamii Forums kulalamika kuhusishwa katika kanuni hizo wakati haizalishi maudhui kama blogu zinavyofanya.

”Ni maudhui mitandaoni, sasa maudhui yanaweza kuwa ya redio, televisheni, blogu, au yanaweza kuwa ya kuchati,” alisema Kilaba.

“Mtoa huduma anaweza kuingia kwenye kundi la mzalishaji wa maudhui, kwa mfano mtumiaji wa mwisho amepost kwako na wewe ni unayetoa huduma, sasa ukiamua kukipokea maana yake umekikubali. ITV anatoa huduma lakini ana provide TV content (maudhui ya televisheni), Vodacom anatoa huduma lakini anazalisha maudhui ya data, vifurushi vya mawasiliano.”

Juzi mkurugenzi mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Melo alisema hawajui watakuwa nje ya huduma hizo hadi lini na kwamba hawajasajili mtandao wao kwa sababu hawazalishi maudhui bali wanatoa huduma.

Kilaba alisema katika jambo hilo hakuna mtoa huduma aliyekataliwa kujisajili endapo atakuwa na sifa, badala yake wametakiwa kukamilisha taratibu.

TCRA ilianza usajili huo Machi 13 na mwisho ni Juni 15 (Ijumaa wiki hii) na imesema itachukua hatua dhidi ya wote watakaoendelea na huduma bila ya kusajiliwa.

Kuhusu nafasi ya kutunza faragha ya mtoa taarifa za kiuchunguzi, Kilaba alisema kanuni hizo zimeweka wazi kwamba, mtoa taarifa huyo anatakiwa kupeleleke taarifa hizo kwa mmliki wa chombo husika mtandaoni badala ya kukiwasilisha mwenyewe.

“Wewe kama ni raia mwema unaweza kuniletea mimi au ukampelekea mwenye blogu, yeye ndiyo ataitoa kwenye blogu ila asikutaje jina au jukwaa lake,” alisema.

Kuhusu umiliki wa akaunti yenye wafuasi wengi, alisema ni muhimu kufanya uchambuzi wa kila mfuasi aliyeko katika akaunti yako ili kuepuka michango ya uchochezi. .

Wakati huohuo, Chama cha Wamiliki wa Blogu (TBN) kimesema mwitikio wa usajili ni mzuri kwa wanachama wake.

Katibu mkuu wa TBN, Krants Mwantepele alisema licha ya kukosa takwimu, baadhi ya watoa huduma wakubwa katika orodha ya wanachama wake 130, wameshajisajili, lakini hakutaka kuzungumzia Jamii Forums.

Wanachama wa TBN ni pamoja na wamiliki wa blogu, wamiliki wa televisheni za mitandaoni na redio za mtandaoni. Baadhi ya waliojisajili hadi sasa kutoka TBN ni Muungwana Blog, Dar24, Milard Ayo na Mwanaharakati Mzalendo ambao huzalisha maudhui mbalimbali ya michezo na burudani.

Laibukia bungeni

Katika hatua nyingine, sakata la Jamii Forums liliibuliwa jana mjini Dodoma na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ambaye aliomba chombo hicho kijadili suala hilo kisha kutoka na mapendekezo.

Kubenea alianzisha mada hiyo jana mara baada ya maswali na majibu bungeni, akiomba kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili suala hilo.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alikataa kuahirisha kwa kuwa waliofungiwa wana sababu zao.