Prime
Nani aliyemuua Aneth Msuya?

Dar es Salaam. Ni nani na yuko wapi aliyetekeleza mauaji ya Aneth Elisaria Msuya?
Hili ni swali linalogonga vichwa vya wadau wa haki za binadamu, ikiwemo haki ya uhai, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam juzi, kuwaachia huru washtakiwa waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji hayo.
Aneth alikutwa amefariki chumbani, nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, asubuhi ya Mei 26, 2016.
Alikuwa ni mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.
Miongoni mwa mambo au viini vya kesi hiyo vilivyokuwa havibishaniwi mahakamani ni pamoja na Aneth alifariki dunia kweli na kwamba alikufa kifo kisicho cha kawaida. Na kwamba kifo chake hakikutokana na sababu za asili kama ugonjwa au majanga.
Hivyo kama kifo chake hakikutokana na sababu hizo, ni dhahiri na kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hasa ripoti ya uchunguzi, kifo chake kilisababishwa na mtu au watu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, chanzo cha kifo cha Aneth kilitokana na kukatwa shingo na kutenganisha koromeo kwa kitu chenye ncha kali.

Mjane wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita akishangilia baada ya kushinda kesi ya mauaji iliyokuwa inamkabili yeye na mwenzake Revocatus Muyella katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Kwa maana hiyo, majeraha hayo yaliyosababisha kifo chake yalifanywa na mtu au watu.
Jamhuri kupitia Jeshi la Polisi, chombo chenye dhamana ya ulinzi wa usalama wa raia na mali zao, iliwashtaki wifi wa marehemu, Miriam Steven Mrita, ambaye ni mke wa Bilionea Msuya na Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray. Wote wawili walishtakiwa kwa tuhuma za mauaji hayo.
Hata hivyo, Mahakama katika hukumu yake iliyosomwa juzi Ijumaa, Februari 23, 2024 na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 103/2018, iliwaachia huru washtakiwa hao wote baada ya kuwaona kuwa hawana hatia kwa mashtaka hayo yaliyokuwa yakiwakabili.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka, ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa washtakiwa hao ndio walihusika na mauaji hayo.
Kwa kuwa mahakama imejiridhisha kuwa waliokuwa wanakabiliwa na shtaka hilo sio waliohusika kutekeleza mauaji hayo, na kwa kuwa kweli Aneth alifariki dunia na alifariki kifo kisicho cha kawaida, bali kilisababishwa na mtu au watu; ndipo swali linapojengeka ama kuibuka, ni nani aliyemuua?
Kuna watu ambao husababisha vifo vyao wenyewe, yaani hujiua, mfano kwa kujipiga risasi, kunywa simu, kujinyonga, kujichoma kisu au kwa kitu chochote cha ncha kali.
Hawa vifo vyao huelezwa kuwsababishwa na vyanzo mbalimbali kama vile migogoro ya kindoa, familia, visasi na sababu nyinginezo.
Hivyo, uamuzi huo wa mahakama na ukweli kuwa kuna watu huwa wanajisababishia vifo vyao, ukweli huu unaongeza maswali mengine kuhusu mauaji ya Aneth.
Je, ina maana hata Aneth alijiua mwenyewe kwa kujichinja? Kama siyo yeye mwenyewe, ni nani na yuko au wako wapi waliomuua?
Je, ni nani wa kufumbua fumbo hilo na kwa namna gani? Jeshi la Polisi linapaswa kufanya nini kumpata au kuwapata wahusika?
Maoni ya wadau
Baadhi ya wadau wa masuala ya sheria na haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi, wameizungumzia hukumu hiyo kwa mrengo tofautitofauti
Wakili, Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Sheria (LHRC), alisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na vyombo vyake vya upelezi ambavyo ni Jeshi la Polisi, wanatakiwa kurudi nyuma na kuaangalia ni wapi hawakufanya vizuri katika upelelezi wao.
Mwananchi lilimtafuta Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai wazungumzie hukumu hiyo, lakini hawakupatikana.
DPP Mwakitalu simu yake ya mkono ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa lakini DCI Kingai, japo alipokea simu, lakini alijibu kwa kifupi tu kuwa alikuwa kwenye kikao.
Hata hivyo, Massawe alisema kwa kuwa bado hajaisoma hukumu hiyo yote na kuona ni namna gani Mahakama imewaelezea hao wahusika, inakuwa changamoto kuizungumzia kwa undani.
Lakini akasema kuna wakati kesi za aina hiyo washtakiwa wanaweza kuwa walihusika, lakini upelelezi ukawa haujakaa vizuri na mtuhumiwa akashinda kesi.
“Wakati hukumu inatoka unajua kabisa hawa sio wahusika, na kwamba, ina maana kuna wahusika wengine sehemu nyingine.
Sasa ndio changamoto ambayo tumekuwa nayo hata kwenye mfumo wetu wa haki jinai, ambao tumekuwa tukiulalamikia siku zote kwamba tunahitaji weledi kwenye upelelezi," alisema Massawe na kuongeza:
"Pia mfumo wetu umejengwa zaidi kwenye mazingira ambayo ni rahisi hata kumbambikia mtu kesi ambaye hahusiki. Ndio maana tunakuwa na kesi za mtu kushtakiwa kwa nia mbaya tu ili kumkomoa mwenzake.
Kwa upande wake, Wakili mwandamizi, Francis Stolla alisema Polisi wanayo fursa ya kufanya upelelezi wa kina tena na kuwafikisha mahakamani watu watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo inaweza kufanyika dhidi ya watu wengine kabisa tofauti na washtakiwa hao.
"Kwa hawa waliokuwa wanashtakiwa kesi yao imeisha", alisema Wakili Stolla.
Alifafanua kuwa kile ambacho Serikali inaweza kukifanya dhidi ya hao walioshinda kesi hiyo, ni kukata rufaa na kama inaweza kuwa na ushahidi mpya, inaweza kuomba iruhusiwe kuwasilisha ili mahakama iweze kuizingatia.
Naye wakili wa Mahakama Kuu, Constantine Kakula, alisema, kisheria kesi ina kuwa na pande mbili.
Upande mmoja wanashinda na upande mwingine wanashindwa, hakuna sare mahakamani kama ilivyo kwenye michezo mfano mpira wa miguu.
"Kwanza kisheria, kwenye kesi kuna pande mbili, upande mmoja watashinda na upande mwingine watashindwa, hakuna draw (sare) mahakamani, mwishowe mahakama itasema mshtakiwa amepatikana na hatia au hajapatikana na hatia" alisema Wakili Kakula na kuongeza:
“Kwa sababu Serikali ndio walikuwa wameshtaki, kazi yao ilikuwa ni kuithibitishia mahakama mashtaka dhidi ya washtakiwa, lakini kama Jaji ameona hawajathibitisha kosa, lazima awaachie huru".
Wakili huyo alisema ni wajibu wa Serikali sasa kukaa na kama kuna maoni ya jaji ambayo hayakuwa sahihi na kama hajaridhika nayo, basi upande wao ukate rufaa.
Alipoulizwa kama Jeshi la Polisi kama linaweza kurudi kufanya upelelezi, Kakula alisema haliwezi kufanya uchunguzi tena kwa sababu walishafanya uchunguzi, ndiyo maana kesi ilifikishwa mahakamani.
"Sheria haiwaruhusu Polisi kufanya uchunguzi kwa kesi ambayo imeshakamilika na kutolewa hukumu," alisema Kakula.
Alisema kuna kesi ambazo Serikali ilishindwa Mahakama Kuu, lakini walipokata rufaa Mahakama ya Rufani, walishinda kesi na moja ya kesi hiyo ni ile iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake.
“Katika kesi ile ya Zombe ambayo ilikuwa ya mauaji, Mahakama Kuu iliwaachia huru washtakiwa wote baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao, lakini DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani na kushinda kesi hiyo, baada ya mshtakiwa mmoja aitwaye Bageni kutiwa hatiani na kuhukumiwa,.
Kwa upande wake, wakili wa Mahakama Kuu, Emmanuel Ukashu, alisema katika makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria, jukumu la kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka, ni la upande wa mashtaka na sio vinginevyo
Kisheria upande wa mashtaka unatakiwa kuonyesha kiushahidi madhubuti kwamba huyo mtu amefanya kosa bila kuacha shaka.
“Sasa maamuzi yoyote yanapokuwa yamefanywa na mahakama na kesi imesikilizwa hadi kufikia mwisho na kutolewa hukumu, Jeshi la Polisi halina nafasi tena ya kufanya upelelezi kwa sababu kesi ilishasikilizwa na kutolewa uamuzi" alisema.
Akifafanua zaidi, Ukashu alisema kama Serikali wanaona kuna kitu hakikukaa sawa katika uamuzi uliotolewa na jaji Edwin Kakolaki, wakate rufaa Mahakama ya Rufani.
“Lakini kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa/ washtakiwa kuna fanya mtu au watu katika kesi hiyo kuwa hawana dosari na hivyo mahakama kuwaona hawana hatia na kuwaachia huru" alisema.
Wakili mwingine wa Mahakaka Kuu, Shabani Mlembe alisema Serikali ina nafasi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
“Japokuwa sijapitia nakala ya hukumu, lakini nimeona baadhi ya video zikiwaonyesha ndugu wa Aneth wakisema hawajaridhika na hukumu hiyo.
"Sasa kesi hiyo ingekuwa ya madai ndugu wa Aneth wangekata rufaa wenyewe, lakini kesi hii ni ya jinai na mwenye mamlaka ya kukata rufaa ni DPP, hivyo kwa kuwa ndugu wanadai hawajaridhika na hukumu hiyo, wanaweza kumlazimisha DPP ili akate rufaa Mahakama ya Rufani." alisema Mlembe.
Hukumu ya Mahakama
Mahakama ilifikia hitimisho la kutamka kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa, kwa kuwa ushahidi huo wa kuwahusisha washtakiwa na mauaji hayo, unaacha shaka.
Katíka kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa unategemea zaidi kuthibitisha shtaka hilo kupitia ushahidi wa maelezo ya mshtakiwa wa kwanza Miriam, ya kukiri kosa na ushahidi wa uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Hata hivyo, mahakama iliukataa ushahidi huo wa maelezo hayo ya mshtakiwa wa kwanza baada ya kuyaona kuwa ni batili kutokana na kukinzanzana na mashahidi wawili wa Serikali kuhusiana na jinsi yalivyopatikana na kutozingatia sheria na taratibu.
Baada ya kutupilia mbali maelezo hayo yaliyoonesha kuwa mshtakiwa wa kwanza alikiri kutenda kosa, Mahakama ilibakia na ushahidi wa vinasaba tu ambao ulikuwa unaonesha kuwa mshtakiwa wa pili alikuwepo eneo la tukio la mauaji.
Ushahidi huo ni kuoana vinasaba katika vielelezo viwili vilivyokutwa eneo la tukio la mauaji (ulikokuwa mwili wa Marehemu) yaani kisu na filimbi, pamoja na vinasaba vilivyopatikana katika sampuli ya mpanguso wa mate ya mshtakiwa wa pili, Muyella.
Hata hivyo mahakama ilisema kuwa licha ya ushahidi huo kuonesha kuwa mshtakiwa wa pili alikuwepo eneo la tukio la mauaji, lakini upande wa mashtaka haukuweza kuwasilisha ushahidi unaothibitisha kuwa ndiye aliyetenda kosa hilo.
Jaji Kakolaki alisema kwamba mtu kuwepo tu eneo la tukio hakuwezi kuthibitisha uhusika wake na tukio bila kuwepo ushahidi unaothibitisha kuhusika kwake bila kuacha chembe yoyote ya shaka.