Mwili wa Mafuru kuwasili Tanzania Jumanne, kuzikwa Dar Ijumaa
Muktasari:
- Lawrence Mafuru amefariki dunia akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ambaye amehudumu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu. Amefikwa na mauti akiwa Hospitali ya Apolo nchini India kwa matibabu.
Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru unatarajiwa kuzikwa Ijumaa, Novemba 15, 2024 katika makaburi ya Kondo yaliyopo Tegeta, jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili Tanzania Jumanne ya Novemba 12, 2024.
Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi nchini Tanzania akihudumu katika sekta binafsi na ya umma, amefariki dunia jana Jumamosi, Novemba 9, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Familia ya marehemu imetoa ratiba ya mazishi wakati huu ambao maombolezo ya msiba yanafanyika nyumbani kwa marehemu Mafuru, eneo la Bunju A, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba, mwili wa Mafuru unatarajiwa kuwasili Tanzania Jumanne saa saba mchana katika Uwanja vya Ndege Julius Nyerere (JNIA) kutokea New Delhi nchini India.
Ratiba hiyo inaonyesha mwili utawasili saa 7:45 mchana na kuondoka uwanjani hapo kuelekea Hospitali ya Lugalo saa 10:00 jioni.
Jumatano itakua ni maombolezo yatakayofanyika nyumbani kwa marehemu Mafuru kabla ya Alhamisi, Novemba 14, 2024 ambapo kutakuwa na shughuli ya kuaga mwili katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa 3:00 asubuhi mpaka saa 8:00 mchana.
Baada ya hapo kutakuwa na msafara wa mwili kuelekea nyumbani kwa marehemu Bunju A na utalala nyumbani kwake kabla ya shughuli za maziko kufanyika Ijumaa.
Ratiba ya siku ya maziko itaanza saa 2:00 asubuhi kwa chai kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu na saa 4:30 hadi saa 5:30 asubuhi msafara wa mwili wa marehemu na waombolezaji utaelekea Kanisa la SDA – Magomeni.
Kanisani hapo itafanyika ibada ya faraja kuanzia saa 6:00 hadi saa 8:00 mchana na msafara utaelekea makaburi ya kwa Kondo, Tegeta na maziko ya kiongozi huyo yamepangwa kufanyika kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka saa 11:00.
Katika eneo ambalo alikuwa anahudumu Mafuru, miongoni mwa kazi zinazofanywa na Ofisi ya Tume ya Mipango, ni kuandaa dira ya maendeleo ya Taifa ya muda mfupi na muda mrefu na kiongozi huo amefariki wakati mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ukiendelea.
Kutokana na kifo hicho, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi akisema,”Mafuru atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka, bidii na ubunifu alipotumikia nafasi mbalimbali ndani ya Serikali. Mwenyezi Mungu aijalie familia yake subra na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.”