Mwili unaodaiwa kuzikwa kimakosa wafukuliwa, familia yasubiri vipimo vya DNA

Polisi wakiutoa kaburini mwili unaogombaniwa na familia mbili, ambao ulizikwa katika kitongoji cha Dungi Kibosho Kindi, Wilaya ya Moshi, kwa ajili ya kuupeleka kufanyiwa vipimo vya DNA. Picha na Yese Tunuka
Muktasari:
- Septemba mosi mwaka huu, polisi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi Wilaya ya Moshi wakiambatana na madaktari wawili, walifika katika familia ya Shoo kwa ajili ya kufukua mwili huo
Moshi. Mwili unaogombaniwa na familia mbili ambao ulizikwa Kitongoji cha Dungi, Kijiji cha Kibosho Kindi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, umefukuliwa leo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya vina saba (DNA).
Mwili huo unaodaiwa kuwa wa Richard Shoo, (31) aliyefariki Juni 16,2024 na kuzikwa Juni 25, mwaka huu, nyumbani kwao Dungi, umefukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na vipimo vya vinasaba (DNA) baada ya familia ya Jackson Joseph (29) kuibuka na kudai kuwa mwili huo uliozikwa sio wa Shoo na kwamba ni wa kijana wao Jackson.
Septemba mosi mwaka huu, polisi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi Wilaya ya Moshi wakiambatana na madaktari wawili, walifika katika familia ya Shoo kwa ajili ya kufukua mwili huo, lakini ilishindikana baada ya familia kudai kutoshirikishwa na kutaka kuonyeshwa kibali cha Mahakama cha kufukua mwili, ambapo polisi hawakwenda nacho.
Polisi walilazimika kuomba kutumiwa kibali hicho kwa simu ambacho walidai walikiacha ofisini, hata hivyo familia ilikataa na kudai wanahitaji kukiona hali ambayo ilifanya kuahirishwa kwa zoezi hilo.
Leo Septemba 4, 2024, familia zote mbili zilifika mahakamani na amri kutolewa kaburi likafukuliwe ili mwili huo utolewe na kupimwa DNA, kujiridhisha ni mwili wa nani.
Baada ya amri hiyo, saa 9:20, polisi sita wakiongozwa na mkuu wa upelekezi Wilaya ya Moshi, wakiambatana na madaktari wawili na familia ya Jackson Joseph akiwamo mama yake mzazi, walifika nyumbani kwa Shoo kwa ajili ya kufukua kaburi hilo ambako kuliibuka vurugu za baadhi ya wananchi na familia kuonyesha hawajaridhishwa na kinachotaka kuendelea.
Hata hivyo, baada ya mvutano huo uliochukua zaidi ya dakika 30, wananchi hao walitulia lakini wakagoma kutoa vifaa vya kufukua kaburi, hali iliyomlazimu mkuu wa upelelezi wilaya kutoa fedha na kuagiza kwenda kununuliwa kwa chepeo mbili ndipo shughuli ya ufukuaji ikaanza.
Baada ya kaburi hilo kufukuliwa, polisi waliondoka na jeneza lenye mwili wakidai kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kusubibiri taratibu za vipimo vya DNA.
Familia ya Shoo yasimulia
Anna Kimaro, mama mzazi wa Richard Shoo, amesema baada ya kupata taarifa za mwanawe kufariki dunia alifika na kutambua kuwa ndiye na shughuli za maziko zikaendelea.
"Baada ya kuambiwa mwanangu amefariki, nilikuja hapa nikaomba nionyeshwe mwanangu na nilipofunua uso nilimtambua ni mwanangu na alama yake ninayoifahamu usoni ilikiwepo," ameeleza mama huyo.
Baba mzazi wa Richard, Korodius Shoo amesema mwanawe alifariki Juni 16,2024 na kwamba kabla ya kifo alikuwa ameonana naye.
"Mara ya mwisho nilionana na mtoto wangu siku ya Ijumaa na baada ya kupewa taarifa amefariki, tulienda hospitali kuutambua mwili na tuliutazama mwili alikuwa ni Richard Shoo na tulimtambua kwa sura na alikuwa ana alama kwenye jino."
"Tulifuata taratibu zote ikiwamo kufika polisi na baadaye kwenda Hospitali ya Mawenzi ambapo alifanyiwa uchunguzi ndipo tukakabidhiwa mwili."
Aidha amesema enzi za uhai wake, kijana wake alikuwa akijishughulisha na shughuli ndogondogo ikiwamo kubeba mizigo katika Soko la Manyema mjini Moshi na kwamba waliambiwa chanzo cha kifo chake ni kupigwa.
"Nilipewa taarifa na wafanyabiashara wa Soko la Manyema kuwa mwanangu amepata matatizo na amefariki na nilipouliza matatizo gani niliambiwa amepigwa na mwili ulichukuliwa na polisi ukapelekwa Mawenzi,familia tulienda kuutambua pale," amesema.
Baba mdogo wa marehemu, Jubileti Shoo amesema baada ya kupata taarifa za kifo cha kijana wao kutoka kwa kinamama wa Soko la Manyema, familia yote ilitoka kwenda kujiridhasha na walipouona mwili waliutambua ni wa kijana wao.
"Tulienda familia nzima Mawenzi kutambua mwili na tulifuata taratibu zote, na tuliukagua mwili na kujiridhisha ni mtoto wetu maana alikuwa hajaharibika, lakini pia tulimcheki kwenye jino lake lilikuwa limemeguka kidogo na kuna mguu wake tuliufahamu, hivyo tukatambua ni kijana wetu, kwani tuliangalia pia kucha, mikono tukajiridhisha.

Zoezi la kufukua mwili unaodaiwa kuzikwa kimakosa katika Kijiji cha Kibosho Kindi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya vina saba (DNA).
"Tunashangaa huyu anayedai ni mwili wa kijana wake ametokea wapi maana tulikaa karibu mwezi mzima ndipo akajitokeza mtu kudai tumezika mwili wa kijana wake, tunashindwa kuelewa."
Naye Upendo Shoo amesema: "Nilimtambua Richard kuanzia kwenye miguu mpaka usoni na alama ya pengo aliyokuwa nayo na usoni alikuwa ana alama, mtu hawezi kumsahau mtoto wake, nilimtambua kabisa ni yeye"
"Kwa sasa Serikali imeamua, sisi hatuna kipingamizi, wao wachukue mwili wakapime kama ni wa kwetu wataturudishia mwili wetu".
Mama wa Jackson naye afunguka
Mama mzazi wa Jackson Joseph, Agness Joseph amesema alipata taarifa za kijana wake kuuawa na alipofuatilia polisi alipewa taarifa kuwa mwili ulishachukuliwa na kwenda kuzikwa.
"Huyu mtoto wangu alifariki Juni 16, 2024 akazikwa hapa kwa mazingira ya kutatanisha Juni 25,2024, mimi nilipata taarifa wiki mbili zilizopita nikaanza utaratibu wa kwenda polisi na hospitali, nikamkosa."
Mama huyo ambaye ni mkazi wa Mailisita Wilaya ya Hai, amesema: "Nilipomkosa nikatulia kidogo, ndipo nikapigiwa simu kuwa Jackson amefariki ila ametupwa mtaroni, tukafuatilia polisi tukaambiwa mbona mtu wenu alishafariki Juni 16 na amezikwa sehemu ambayo inaitwa Dungi na alichukuliwa na baba yake nikawaambia siyo."
"Polisi wakafanya utaratibu baba wa huyu kijana Shoo akaja polisi na kuhojiwa na jina la marehemu lilikuwa limeandikwa Jackson Joseph akaulizwa mbona ulichukua mwili wa mtu," amesema Agness.
Amesema baada ya kubaini alizikwa Kibosho walifanya taratibu za kutafuta vibali mahakamani na Septemba mosi wakaenda kwa ajili ya kufuukua lakini familia ilikataa.
Agness amesema walifika Jumapili kwa ajili ya kufukua mwili wakakataa na leo wameenda mahakamani wakasema kibali kilishatolewa, hivyo mwili ufukuliwe ukapimwe DNA.
Amesema alionana na kijana wake Jackson Juni 4, mwaka huu na kwamba taarifa za kifo chake alipewa na watu kuwa aliruka ukuta akavunjika miguu ndipo wananchi wakamshambulia na kumuua.