Mwenyekiti Monduli aamriwa kumlipa fidia Sh250 milioni aliyekuwa RC Morogoro

Muktasari:
- Katika shauri hilo la madai namba 23/2022, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loota Sanare aliomba kulipwa fidia ya Sh200 milioni kwa madhara aliyopata kutokana na maneno ya kashfa anayodai yalitolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph.
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imemuamuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Isack Joseph, kumlipa fidia ya Sh250 milioni baada ya kukutwa na hatia ya kumkashifu na kumtusi aliyewahi kuwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loota Sanare.
Sanare ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) mkoani Arusha aliomba kulipwa fidia ya Sh200 milioni kwa madhara aliyopata kutokana na maneno ya kashfa anayodai yalitolewa na Joseph.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa, Septemba 15, 2023 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aisha Ndossi, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la madai namba 23/2022, ambapo Sanare aliwakilishwa na mawakili, Kapimpiti Mgalula na Judith Reuben huku Isaac akiwakilishwa na mawakili Peres Parpai, Sendeu Nicolas na Yonas Masiaya.
Isaac anadaiwa kutoa maneno hayo Novemba 7, 2022 akiwa Sinoni wilayani Monduli akiwa na watu wengine pamoja na waandishi wa habari ambapo anadaiwa kusema "ndugu yangu Sanare amejiongezea eka moja na pointi kwenye eneo ambalo hajapewa…huu ni wizi imekuwa mambo ya kujirudiarudia kwa kiongozi huyu," amesema
Uamuzi huo umetolewa baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote na kujiridhisha pasipokuwa na shaka yoyote kuwa mwenyekiti huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Kadogoo alitamka maneno ya kashfa dhidi ya Sanare.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Ndossi ametaja viini vya madai hayo ni pamoja na endapo maneno yaliyosemwa na mdaiwa ni ya kashfa na kama ni kweli amedhurika na ana haki ya kulipwa na ameweza kuthibitisha kama kweli mdai alitendewa kitendo hicho.
"Kiini cha madai haya ni video au clip ambayo mdai aliileta mbele ya mahakama na ikapokelewa kama kielelezo kiliwekewa mapingamizi lakini nilisema nitayajibia kwenye hukumu. Tukiangalia uhalisia wa youtube mtu yeyote anaweza kuingia youtube na kudownload na kuangalia," amesema.
"YouTube dunia ina access mahakama ilitegemea kupata mapingamizi zaidi kutoka upande wa wakibu maombi kuwa video haikuwa youtube au haijawahi kuwepo lakini hawakufanya hivyo. Upande wa wadaiwa walitakiwa kuonyesha video hiyo si halisi kwa kuleta mmiliki aseme haikuwa hiyo hawakufanya hivyo video hiyo ni sahihi," ameongeza
Kuhusu kashfa amesema wanaangalia maneno ya kashfa kwenye kamusi inasema ni maneno ya uongo ambayo yanaweza kumletea chuki kwenye jamii au kudharauliwa sehemu anayoishi biashara na shughuli zake.
"Kuhusu mdai ameathirika kiasi gani, kwa kuwa hana uthibitisho kwamba ile video yalikuwa ya uongo au kutengenezwa tunaona maneno hayo yalikuwa ya uongo kwa lengo la kumuumiza mdai hivyo maneno haya yamemuumiza mdai.
Mdaiwa anakiri kuwa mdai alikuwa na nyadhifa mbalimbali kuwa alikuwa Mwenyekiti wa CCM, RC alikuwa ameshajenga hadhi yake japo kwa sasa ni mtu wa kawaida hivyo amepata madhara," amesema Hakimu.
"Mdai atalipwa kama alivyoomba Sh200 milioni na Sh50 milioni kwa kupoteza hadhi yake na gharama ya shauri hilo,"amesisitiza Hakimu Ndossi.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Sanare alishukuru mahakama kwa uamuzi huo na kuomba viongozi waliopewa madaraka kutumia lugha nzuri kwa jamii kwani madaraka waliyonayo ni ya muda.
Sanare ambaye pia ni kiongozi wa mila 'Laigwanan', alisema kabla ya kuwasilisha shauri hilo mahakamani hapo alijaribu kufikisha suala hilo kwa wazee wa mila ambapo Kadogoo aliitwa kwa mara tatu ila hakwenda hivyo kulazimika kupeleka suala hilo mahakamani.