Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwaselela alivyotatua kero ya uzio Kituo cha Afya Iyela

Muktasari:

  • Kituo cha Afya Kata ya Iyela kimeanza kutoa huduma tangu mwaka 2023

Mbeya. Kilio cha wagonjwa na watoa huduma za afya katika Kituo cha Afya Kata ya Iyela mkoani Mbeya juu ya muingiliano wa shughuli za wananchi huenda kikabaki historia baada ya changamoto ya uzio kupatiwa ufumbuzi.

Hii ni baada ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela kukabidhi vifaa vya ujenzi huku akielekeza ujenzi kuanza Jumatatu ya wiki ijayo.

Imeelezwa kuwa, kituo hicho kilichoanza kutoa huduma tangu 2023 kimekuwa na muingiliano wa shughuli za wananchi wanaotumia eneo hilo kama njia hali iliyowapa wakati mgumu wagonjwa na wahudumu wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza leo Jumatatu, Mei 25, 2026, wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, ikiwa ni matofali 5,000 na saruji mifuko 100, Diwani wa Kata ya Iyela Absalum Mwambepo amesema kutokana na kukosekana na uzio, hali ilikuwa si shwari.

Muonekano wa Kituo cha Afya cha Kata ya Iyela, ambacho wananchi wamekuwa wakipita ndani ya eneo hilo na kusababisha kero kwa wagonjwa na watumishi kutokana na kukosekana kwa uzio, ambapo leo vifaa vya ujenzi wa uzio huo vimekabidhiwa.

Amesema eneo hilo limekuwa sehemu ya njia ya watu kupita, kutupa takataka hovyo na kupiga kelele wakati kina maama wanapojifungua na kuweka sintofahamu kwa muingiliano wa shughuli za nje na ndani.

“Lakini, changamoto nyingine hapa ni vyoo vya nje kwa ajili ya wanaoleta wagonjwa na pia hakuna njia ya ndani ya kuunganisha majengo, wanaohama eneo moja kwenda lingine wanajikuta wanaloa kipindi cha mvua,” amesema.

“Kituo hiki kinafanya kazi kubwa, tangu kianze kazi 2023 hadi leo tumepata watoto waliozaliwa hapa ni 1,877, hivyo utaona kwa muda mfupi tunahudumia kata nyingine tofauti” amesema diwani huyo.

Kwa upande wake, Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Dk Hapynes Mringi ameshukuru upatikanaji wa vifaa hivyo akieleza kuwa kilio kilikuwa cha muda mrefu na kwamba hali hiyo itawapa ngvu na hamasa katika kutoa huduma bora.

“Tumshukuru MNEC na Serikali kwa jumla kwa kutusaidia kumaliza kilio hiki cha muda mrefu, sisi watumishi tunaahidi kuendelea kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi,” amesema Dk Hapynes.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, akizungumza na wananchi waliofika katika Kituo cha Afya cha Kata ya Iyela wakati wa kukabidhi vifaa vya ujenzi wa uzio kwa ajili ya kuimarisha usalama wa wagonjwa na watumishi.

Akikabidhi vifaa hivyo, MNEC Mwaselela amewataka vijana wa hamasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhamishia hamasa zao katika ujenzi wa msingi kuanzia Jumatatu, akiahidi kufuatilia kuhakikisha uzio unakamilika.

Amesema akiwa kiongozi wa chama na wananchi, ameamua kujitolea kumaliza changamoto hiyo akieleza kuwa CCM ya sasa ni ya vitendo, akitupia kijembe kwa baadhi ya wanasiasa na makada wa chama hicho wanaonuna kwa kazi zake.

“Sina tabia ya ubinafsi kwa sababu wakati fulani kinachotutesa ni ubinafsi na uchoyo, wapo watu tukifanya maendeleo wananuna, sasa sielewi wanataka nini, wengine ni wa familia yetu humu ndani, lazima tuanze kukemeana tabia ya kukwamisha maendeleo.

“CCM ya sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni ya vitendo, ndio maana mimi kama mwakilishi nimekuwa mbele kutekeleza mambo mengi, nimefanya hivyo Mbeya Vijijini, Rungwe na leo Iyela,” amesema Mwaselela.

Kigogo huyo ameongeza hadi Julai 1, 2026 anahitaji kumaliza kilio cha michango ya wanafunzi wanaolipia mitihani ya ndani, ikiwa ni kufungua mfuko maalumu wa wadau kuchangia na tayari shule ya Msingi Iyela utekelezaji umeshaanza.

Mmoja wa wananchi Ainess Mbwawa amesema imekuwa ni kero kubwa kwa wagonjwa na wananchi wanaofika kituoni hapo kupata huduma kuingiliana na shughuli nyingine za kijamii.

“Hata wale wanaokuja na wagonjwa tunakuwa hatuna tofauti na wapita njia, muda mwingine vyombo vya moto vinafika hadi malangoni bila kujali kuna wazazi wanajifungua au mgonjwa aliyezidiwa,” amesema Ainess.