Mwandishi wa habari aamriwa kumlipa DED Sh2 bilioni

Muktasari:
- Alloyce Nyanda, mwandishi wa habari na mtangazaji ameshindwa kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza (sasa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo), Aaron Kagurumjuli, kwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao yake ya kijamii.
Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza imemwamuru mwandishi wa habari na mtangazaji, Alloyce Nyanda ‘Mtozi’ kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Aaron Kagurumjuli Sh2 bilioni kama fidia kwa kumdhalilisha kwa njia ya mtandao.
Hukumu hiyo imesomwa leo Ijumaa Aprili 11, 2025, saa tatu asubuhi na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Boniventure Lema.
Wakati hakimu akisoma hukumu ya kesi hiyo ya madai namba 6166/2024, mdai Kagurumjuli alifika kortini akiwa na mawakili wake, Erick Mutta na Godfrey Mlingi.
Si Nyanda wala wakili wake aliyekuwapo mahakamani. Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hukumu hiyo, Nyanda amesema yuko safarini mkoani Dodoma akiahidi akifika Mwanza atazungumzia uamuzi huo.
“Sikuwa na taarifa yoyote, siko Mwanza niko Dodoma nikifika Mwanza nitazungumza na wakili wangu. Nikishafika Mwanza tutalizungumzia,” amesema Nyanda.
Katika hukumu, Hakimu Lema amesema Nyanda kupitia akaunti za mtandao wa kijamii alichapisha taarifa za udhalilishaji zinazomhusu Kagurumjuli alipokuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Kinondoni kwa nyakati tofauti. Sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.
“Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote za mdai na mdaiwa, Mahakama imejiridhisha kuwa Alloyce Nyanda alimdhalilisha Aaron Kagulumjuli kupitia akaunti za mitandao yake ya kijamii,” amesema hakimu.
Kutokana na hilo amemwamuru Nyanda kumlipa Kagulumjuli fidia ya Sh2 bilioni kwa udhalilishaji alioufanya, kuomba msamaha kwa yale aliyoyachapisha ambayo ni ya uongo, aliyosema yanaleta fedheha na ni ya udhalilishaji.
Pia ameamuru Nyanda, wakala wake au mtu yeyote anayehusiana naye asichapishe taarifa ambazo amezichapisha, kwa nyakati nyingine yoyote kuanzia sasa na wakati ujao na kuziondoa taarifa hizo ambazo amezichapisha zinazomhusu mdai.
Mahakama imemuamuru mdaiwa kumuomba radhi mdai kupitia majukwaa aliyotumia kumdhalilisha kuanzia sasa na kulipa gharama za shauri ambazo mdai aliziingia wakati wa uendeshaji wa shauri hilo.
Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili wa mdai, Mutta ameishukuru mahakama kwa kutenda haki, akisema wameanza ufuatiliaji wa utekelezaji wa amri za mahakama.
Mutta amesema kama Nyanda atashindwa kutekeleza amri ya mahakama watafuata njia za utekelezaji wa hukumu kwa kuomba kukamata mali zake na kama hatakuwa na mali za kukamata, watamkamata yeye kama mfungwa wa madai.
“Utekelezaji wa adhabu unafahamika, sisi tutaomba utekelezaji haraka iwezekanavyo, kwa hiyo yeye pia anatakiwa alipe haraka iwezekanavyo na pia ana haki zake za msingi ambazo atazitekeleza kimahakama,” amesema.
Amesema kabla ya kuchukua uamuzi wa kwenda mahakamani mteja wake alitoa nafasi kwa mdaiwa ili kumalizana nje ya mahakama kwa kumtaka aombe radhi, lakini hakufanya hivyo.
“Tumeshatoa nafasi ya makubaliano nje ya Mahakama, tulimuomba Alloyce Nyanda aombe msamaha alikaidi kwa hiyo hatuna nafasi hiyo tena, kwa sasa kipaumbele chetu ni kuona namna gani uamuzi wa Mahakama unatekelezwa,” amesema.