Mwandishi Mkuu MCL ashauri Serikali kubadili msimamo uraia pacha

Muktasari:
- Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeendesha mjadala wa Twitter Space yenye mada ‘una maoni gani kuhusu suala la uraia pacha Tanzania’, na kushirikisha wadau mbalimbali.
Dar es Salaam. Mwandishi wa Habari Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, Elias Msuya ameshauri Serikali kutazama upya msimamo wake kuhusu zuio la uraia pacha, akisema uraia pacha utasaidia kufungua milango kwa Watanzania na fursa za Taifa kunufaika kiuchumi.
Msuya ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Mei 31, 2023 wakati wa mjadala wa Twitter Space ya Mwananchi Communications Limited (MCL) yenye mada ‘una maoni gani kuhusu suala la uraia pacha Tanzania.’
Mjadala huo unafanyika ikiwa ni siku moja imepita tangu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dk Stergomena Tax kuelezea Bunge jana Jumanne, Mei 30, 2023 Serikali inakamilisha mchakato wa kutoa hadhi maalum kwa Diaspora.
Jumatatu ya Mei 29, 2023 Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Mhandisi Hamad Masauni aliliambia Bunge hadi kufikia Mei 2023, Watanzania 66 waliukana uraia wa Tanzania na kupewa uraia wa Mataifa mengine.
Akichokoza mada kwenye mjadala huo, Msuya amesema, “suala la uraia pacha halina muafaka duniani, lakini nimefutilia nikagundua kwamba mataifa mengi yanaunga uraia pacha kuliko yanayopinga uraia pacha duniani, hatua hiyo inamaanisha, mataifa mengi yameanza kuona umuhimu wa uraia pacha.”
“Kuna hofu watu wakiwa na uraia pacha kupora rasilimali za Tanzania kupeleka nje ya nchi. Kuna watu wanamilikishwa ardhi ni wageni lakini hawana uraia pacha, sasa hoja ya kupora mbona inaonekana bila hata kuwepo uraia pacha?
“Uraia pacha utatoa fursa, wananchi wakafute maisha na kuleta uwekezaji na fursa za maisha, matokeo yake ni kwamba nchi itaenndelea.”
“Watanzania wanapokwenda kuishi nje ya nchi wanakuwa huru kuleta utajiri wanaoupata na kama nchi tunajikuta tunaongeza mapato ambayo yanapatikana kupitia fedha zinazoletwa na watu waliokwenda nchi nyingine.”