Mwanafunzi kizimbani akidaiwa kumkata kwa panga mwalimu

Muktasari:
- Wakili wa Serikali, Morice Mtoi amedai mshtakiwa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu alimkata kwa panga kichwani mwalimu Stanford Mgaya ambaye wakati wa tukio alikuwa ofisini akiendelea na majukumu yake.
Sengerema. Mwanafunzi wa shule ya sekondari Tamabu Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Aex Butawantemi (18) anayedaiwa kumkata kwa panga mwalimu wake amefikishwa mahakamani leo Oktoba 4, 2023.
Mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Sengerema, Evor Kisoka, Wakili wa Serikali, Morice Mtoi alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 25, 2023.
Akisoma hati ya mashtaka katika shauri hilo la jinai namba 114/2023, Wakili Mtoi amedai mshtakiwa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu alimkata kwa panga kichwani mwalimu Stanford Mgaya ambaye wakati wa tukio alikuwa ofisini akiendelea na majukumu yake.
Amesema kwa kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume cha sura ya 225 kifungu cha 16 ya kanuni ya adhabu kama ilivyorekesbishwa mwaka 2022, mshtakiwa alimsababishia maumivu makali mwalimu Mgaya.
Mshtakiwa ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Misheni Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema amekana mashtaka dhidi yake na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya dhamana ya Sh2 milioni na shauri hilo kuahirishwa hadi Oktoba 11, 2023 litakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Tukio lilivyotokea
Tukio la mwanafunzi Alex kumjeruhi mwalimu wake Stanford Mgaya kwa kumkata panga kichwani na mkono lilitokea Sepetemba 25, 2023 wakati mwalimu huyo akiwa ofisini akitekeleza majukumu yake.
Kabla ya kumshambulia wake, mwanafunzi huyo anadaiwa kuingia ofisini na kumwelza kuwa alienda ili wamalizane kuhusu adhabu aliyopewa yeye na wenzake wengine 16 kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Hali ya kiafya ya mwalimu Mgaya aliyelazwa Hospitali Teule Wilaya ya Sengerema imeimarika na tayari ameruhusiwa kurejea nyumbani tangu Septemba 27, mwaka huu.