Mwalimu, ofisa wa halmashauri wakabiliwa na kesi ya mauaji Serengeti
Watumhumiwa wa kesi ya mauaji ya Rhoda Mobe wakiingia katika mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa ajili ya kesi yao kutajwa. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Washtakiwa hao kwa pamoja wanatuhumiwa kumuua kwa kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake Rhoda Mobe (42) aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti Mkoa wa Mara.
Musoma. Kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa watatu Mwita Maginga( 47) mkazi wa Tarime, Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi jijini Mbeya na Simon Ruhinda (55) ambaye ni muhudumu wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imeahirishwa kwa mara nyingine huku sababu ikielezwa kuwa ni kutokukamilika kwa upelelezi.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanatuhumiwa kumuua kwa kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake Rhoda Mobe (42) aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti Mkoa wa Mara.
Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Eugenia Rujwahuka ambaye ameiahirisha hadi Machi 17 2026 itakapokuja kutajwa tena.
Akizungumza mahakamani hapo leo Jumanne Machi, 3,2026 Hakimu Rujwahuka amesema kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwa vile upelelezi haujakamilika, hivyo inaahirishwa hadi tarehe tajwa itakaporudi tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, hakimu huyo ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili hatua zingine ziendelee ikiwa ni pamoja na kupangwa kwa tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo katika mahakama yenye mamlaka ya kufanya hivyo.
"Wakili shida ni nini, upelelezi bado tu tangu Desemba, haya hii kesi itakuja tena hapa mahakamani Machi 17, washtakiwa mtarudi mahabusu," amesema Rujwahuka akiahirisha kesi hiyo.
Awali, wakili wa Serikali, Martha Mbosori alisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo kuomba kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo.
"Hii kesi inahusisha upelelezi wa kina, hivyo upelelezi hadi sasa bado haujakamilika, ikikupendeza mheshimiwa hakimu tunaomba kupangiwa tarehe nyingine," amesema.
Rhoda ambaye alikuwa ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara anadaiwa kuuawa Oktoba 23,2025 usiku baada ya kuvamiwa nyumbani kwake kijijini hapo.
Watuhumiwa hao watatu kwa pamoja wanadaiwa kumuua Rhoda kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake baada ya kumvamia nyumbani kwake.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197 ambapo wote wamerudishwa mahabusu kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana, sambamba na mahakama hiyo ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.