Mwalimu mkuu jela miaka 30 kwa kumbaka, kumlawiti mwanafunzi

Muktasari:
- Nkunguu alifikishwa mahakamani hapo Machi 21,2024 akituhumiwa kumbaka kisha kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita, katika Kijiji cha Nampangala wilayani Bunda Machi 8 2024.
Bunda. Mahakama ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masahunga iliyopo wilayani Bunda, Vicent Nkunguu baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo.
Mbali na kutumikia kifungo cha miaka 30, Nkunguu pia ameamuriwa na Mahakama hiyo kumlipa binti huyo fidia ya Sh2 milioni.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano, Aprili 23,2025 na Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Betron Sokanya baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

Aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masahunga wilayani Bunda, Vicent Nkunguu (39) akitoka mahakamani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya Sh2 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumlawi mwanafunzi (16) wa darasa la sita shuleni kwake. Picha na Beldina Nyakeke
Nkunguu alifikishwa mahakamani hapo Machi 21,2024 na kusomewa mashitaka mawili ya kumbaka kisha kumlawiti mwanafunzi huyo wa darasa la sita shuleni hapo, katika Kijiji cha Nampangala wilayani Bunda.
Katika kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshtakiwa, upande wa mashitaka uliwaita mashahidi watano akiwemo muathirika na daktari aliyemfanyia uchunguzi wa kitabibu mwanafunzi huyo, na kuwasilisha kielelezo kimoja, huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi watatu, mshtakiwa mwenyewe, mkewe na mwalimu mwenzake bila kielelezo chochote.
Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, siku ya tukio, Machi 8, 2024, mwanafunzi huyo alikwenda nyumbani kwa mwalimu huyo kama alivyoombwa na mke wa mwalimu ili kusaidia kuwapikia watoto, kwani siku hiyo usiku (mke wa mwalimu) alikuwa anakwenda kanisani.
Baada ya kupika, mwanafunzi huyo, watoto watatu na mshtakiwa kwa pamoja walipata chakula cha usiku kisha wakaingia vyumbani kulala, ambapo mwanafunzi huyo alilala na mtoto wa miaka minne katika chumba kimoja.
Akiwa amelala alishtuka kumuona mtu akiingia chumbani humo na alimtambua kuwa ni mshtakiwa kwani taa zilikuwa zinawaka.
Mshtakiwa alikuwa amejifunga taulo la rangi ya maziwa na singlend nyeupe na mwanafunzi huyo alipomuuliza kuwa alikuwa anataka nini, mshtakiwa alimjibu kuwa hawezi kulala mwenyewe na anataka akalale naye.
Mwanafunzi huyo alikataa, hivyo ilimlazimu mshtakiwa kumvuta kwa nguvu huku akimziba kwa mkono mdomoni ili asipige kelele.
Baada ya kumfikisha chumbani kwake, mshtakiwa alimtupa kitandani na kumvua nguo kisha na yeye akatoa taulo lake na kuamza kumlawiti kwa takriban dakika tano kabla ya kumbaka kwa takriban dakika 10.
Alipomaliza kufanya uhalifu huo, mshtakiwa alimtaka mwanafunzi huyo kwenda kunawa sehemu zake za siri huku akimtishia kumuua endapo angemwambia mtu yeyote juu ya tukio hilo.

Siku iliyofuata mke wa mshitakiwa alifika nyumbani asubuhi akiwa na mtoto wake mdogo ambaye alimkabidhi mwanafunzi huyo ili akamlaze kitandani.
Mwanafunzi huyo alipojaribu kumueleza mwanamke huyo juu ya tukio lililotokea usiku alishindwa kufanya hivyo kwani muda wote mshtakiwa alikuwepo, huku akizidi kumtishia kumuua endapo angesema.
Baadaye mke wa mshtakiwa aliondoka nyumbani kwenda kwenye shughuli zake za ushonaji na mwanafunzi huyo pia aliaga ili aondoke kwenda kwao, lakini mshtakiwa alimzuia.
Jioni, mshtakiwa aliingia ndani akiwa na kopo jeupe na kisu kisha akatumia kile kisu kufungua kopo lile na kumlazimisha mwanafunzi huyo anywe, lakini alikataa na mshtakiwa alimkaba na kumbana ukutani kisha akaanza kumnywesha kwa nguvu, akisema hiyo ni dawa ya kuzuia mimba.
Mshtakiwa huyo alipomaliza kumnywesha dawa hiyo, alimwambia mwanafunzi huyo kuwa sasa anaweza kwenda kwao,
Hivyo mwanafunzi huyo alitoka nyumbani kwa mshtakiwa akiwa anatapika na jinsi muda ulivyokuwa ukienda alizidi kuchoka kisha akaamua kwenda kwa kaka yake aliyekuwa akiishi jirani na kwa mshtakiwa.
Alipofika kwa kaka yake, mwanafunzi huyo alieleza juu ya kilichotokea huku akizidi kutapika ndipo walipoamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Mshtakiwa ambaye alikuwa shahidi wa kwanza katika utetezi wake alikana kutenda makosa hayo, huku akiungwa mkono na shahidi wa pili, mkewe, ambaye aliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio alilala nyumbani yeye na mume wake na sio kweli kuwa hakuwepo nyumbani.
Hata hivyo alipohojiwa maswali ya dodoso, shahidi huyo (mke) maelezo yake yalitofautiana na ya mshtakiwa (mumewe) kuhusu nguo ya ndani ya mshtakiwa aliyovaa siku hiyo na kuhusu mtoto mdogo, ambapo mshtakiwa hakusema lolote juu ya uwepo wa mtoto huyo siku ya tukio,
Hakimu Sokanya baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, ametupilia mbali utetezi wa mshtakiwa na amekubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa umethibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa bila kuacha mashaka yoyote.
"Hivyo basi kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa, Mahakama hii imejiridhisha pasipo shaka kuwa Vicent Nkunguu alimbaka binti huyu kinyume na vifungu 130 (1)(2) na 131 na kulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.”
Kabla ya kutoa adhabu, Wakili wa Serikali, Ishihaka Mohamed aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Alipotakiwa kusema chochote baada ya kuelezwa kuwa Mahakama hiyo imemkuta na hatia, Nkunguu amesema licha ya ukweli kuwa yeye hajafanya vitendo hivyo, lakini anaiomba mahakama hiyo imuachie huru ama kumpunguzia adhabu kwani anategemewa na mke na watoto pamoja na wazazi wake.
Akitoa adhabu, Hakimu Sokanya amesema amezingatia maelezo ya upande wa mashitaka na shufaa ya mshtakiwa pamoja na matakwa ya sheria.
"Hivyo Mahakama hii inamuhukumu mshtakiwa Vincent Nkunguu kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa yote na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja", amesema Hakimu Sokanya na kuongeza:
"Pia Mahakama hii inamuamuru mshtakiwa kumlipa fidia muathirika ya Sh2 milioni, Kwa mujibu wa kifungu cha 131 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 na kifungu cha 348 (1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20,” amesema.
Katika kesi hiyo, Nkunguu aliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Leonard Magweyega ambaye hata hivyo hakuwepo mahakamani wakati wa hukumu.